CCM, Chadema hapatoshi mkataba uwekezaji bandari

Dar /Mtwara. Mjadala wa makubaliano ya uendelezaji na uwekezaji wa bandari nchini kati ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai, umezidi kushika kasi kwa vyama vya CCM na Chadema kurushiana vijembe na kutaka wananchi wasikubali upotoshaji.
Vyama hivyo vinadai kuna upotoshaji unafanywa na makada wa pande hizo mbili ili makubaliano hayo yaonekane yanafaa au hayafai kulingana na msimamo wa pande husika.
Vijembe hivyo wamerushiana kwa nyakati tofauti kupitiana mikutano ya hadhara walioifanya watendaji wakuu wa vyama hivyo, katika mikoa ya Dar es Salaam na Mtwara.
Serikali ya Tanzania na Dubai ziliingia mkataba Oktoba 25 mwaka jana kwa ajili ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari (IGA).
Bunge limeshapitisha azimio la kuridhia ushirikiano huo kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya DP World inayomilikiwa na Serikali ya Dubai.
Makubaliano hayo yalibainisha maeneo mahususi ya ushirikiano ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu, maeneo maalumu ya kiuchumi, maeneo ya maegesho na utunzaji mizigo na maeneo ya kanda za kibiashara.
Jana, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo aliongoza timu ya ujumbe wa chama hicho kufanya mkutano wa hadhara, uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, uliokuwa na lengo la kutoa darasa kwa wananchi kuhusu mkataba huo.
Naye Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alikuwa Ukonga jijini Dar es Salaam, akihutubia mkutano wa hadhara aliozungumzia mkataba huo akimtaka Rais Samia Suluhu Hassan kutumia mamlaka yake, kutokuruhusu kuendelea kwa hatua nyingine ya utekelezaji.
Juzi Chongolo alikuwa mkoani Mbeya ambapo aliongozana na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa na mwanachama mkongwe, Stephen Wasira walieleza uzuri wa makubaliano hayo.
Katika mkutano huo, Silaa alikuwa akiuchambua mkataba huo kipengele kwa kipengele.
Chongolo alisema kinachofanyika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/25, akiwashangaa wanaohangaika na kutumia nguvu kubwa ya kuhamisha masuala ya msingi ili ionekane suala hilo linafanywa na mtu mmoja (Rais Samia).
“Hatuna hofu wala shaka na kwamba jambo hili ni utekelezaji wa ilani ya CCM,wanaongaika kulifanya suala la bandari liwe la Samia, wameshindwa kusoma alama za nyakati.Tumewagundua na tumewajua pamoja na njia wanazozitumia,” alisema Chongolo.
Silaa ndiye alipewa jukumu la kuuchambua mkataba huo huku akiwaeleza wananchi kuandika pembeni ili wanapokuja aliowaita wapotoshaji wawe na maswali ya kuwauliza.
Aliwaambia wananchi wa mikoa ya kusini mchakato huo umefuata taratibu kikatiba na kisheria, zikiwemo za kimataifa na suala hilo limehusisha watalaamu mbalimbali.
“Mkataba huu ni sahihi, unakwenda kulinda maslahi ya Watanzania wakiwemo wa wananchi wa Mtwara. Tumekuja hapa kwa maelekezo mahususi ya kutoa majibu kuhusu mkataba huu,” alisema Silaa ambaye pia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mitaji na Uwekezaji
Naye Profesa Kitila alieleza namna mwekezaji DP World alivyopatikana akisema Serikali ilikaribisha kampuni takribani saba kuwekeza kwenye bandari nchini.
Kwa mujibu wa Profesa Kitila, kampuni saba za kutoka mataifa ya China, India, Denmark Ufaransa na Falme za Kiarabu ikiwemo ya DP World ziliwasilisha mapendekezo yao ya uwekezaji.
“Si kweli kwamba tulimchukua mtu mmoja (DP World), bali baada ya uchambuzi wa kina kwa kuzingatia vigezo vya utalaamu, uzoefu na upana wa mtandao ndani ya bara la Afrika, Serikali ikajiridhisha DP World anafaa zaidi kuliko wengine,” alisema
“Kwa hiyo haya yanayoendelea inawezekana wenzetu waliokosa nafasi wamenuna, kwenye biashara kuna kununiana. DP World amepatikana miongoni mwa kampuni saba zilizowasilisha maombi Serikalini,” alisema Profesa Kitila.
Naye Wasira alisema wamekwenda kujibu uongo unaosemwa kuhusu mkataba wa makubaliano ya ushirikiano na uwekezaji wa bandarini nchini.
“Ni uongo wa kutungwa wanaosema bandari zote zimeuzwa, tumekuja kujibu uongo unaofanana na giza. Uhusiano wa giza na mwanga ni mbaya, mwanga ukija giza linapotea tumekuja kazi yetu kukimbiza giza,” alisema.
Alisema Serikali haiwezi kuuza nchi wala bandari, akisisitiza ziara yao inakwenda kujibu fitina ambazo sio za nje pekee hadi ndani ya Taifa.
Alisema fitina ya kiuchumi adui yako anaonekana na wengine wapo ndani ya CCM waliokaa kama bundi wanaonufaika na ufanisi mdogo wa bandari.
“Nawapa ujumbe maana tunajuana na kuheshimiana, ipeni nafasi nchi isonge mbele tusitangulize matumbo mbele. Hakuna mpinzani wako anayeweza kukusifia kwa mazuri unayofanya na wewe ukazubaa na kusema ni kweli,” alisema
Mnyika ang’aka
Naye Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika, aliwahutibia wakazi wa Ukonga na viunga vyake akisema pamoja na kelele zilizopigwa na wananchi kuhusu mabaya yaliyomo katika mkataba huo, anaishangaa CCM na Serikali kuendelea na msimamo wa kuutekeleza.
“Chadema tukiwa chama kinachowakilisha Watanzania, tunasisitiza Rais Samia asipeleke hati Dubai kuruhusu kuanza kwa mkataba huo. Kwa kauli ya CCM wanampa kibali Rais aruhusu hati ya kuridhia mkataba ipelekwe Dubai ili mchakato kuanza,” alisema.
Mnyika alimtaka Rais kurudisha bungeni mkataba huo ili ufutwe kutokana na kasoro zilizopo.
Hata hivyo, Mnyika aliitaka Serikali ieleze baada ya mkataba na Kampuni ya Kuhudumia Makontena (TICTS) kuisha ni kampuni gani inayofanya kazi ya kuendesha bandari ya Dar es Salaam, maeneo ya makontena na bandari kavu kadhaa.
Lakini, alisema kwa sasa wanaendelea kuelimishana kwa kufanya mikutano ya hadhara na wananchi ili kuhakikisha watawala wanaamua na isipofanyika hivyo, itatafutwa hatua za ziada dhidi yao.
“Hao hao wanaotetea bandari hivi sasa ndiyo hao tukiwaambia msipandishe kodi kwenye mafuta wanapandisha hali ya maisha inazidi kuwa ngumu. Watu hawa wanaotuongezea ugumu wa maisha hawapaswi kuaminiwa wanapaswa kuondolewa madarakani,” alisema.
Ijumaa iliyopita, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitoa maazimio ya kamati kuu ya chama hicho kuhusu mkataba huo wa ushirikiano ikiwemo kufanyika kwa mikutano ya hadhara kuanzia Julai 28 mwaka huu, wakianzia mkoani Kagera.
Mikutano hiyo ni mwendelezo wa operesheni ya +255 katiba mpya na sasa itaongezwa okoa bandari zetu.