CCM yaanza usaili makada 178 wanaotaka ubunge Eala

Baadhi ya wanachama wa CCM wakiwa kwenye kikao cha usahili mbele ya Sekretarieti ya Halmashauri kuu ya Taifa mkoani Dodoma. Picha na Merciful Munuo.

Muktasari:

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza usaili kwa wanachama wa Tanzania Bara walioomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea nafasi za Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala).

Dodoma. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza usaili kwa wanachama wa Tanzania Bara walioomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea nafasi za Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala).

Usaili huo umeanza leo Jumapili Septemba 4, 2022 jijini Dodoma ambapo walioomba nafasi hizo wamejitokeza kwa wingi kufanyiwa uhakiki na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wakiwa na nyaraka muhimu zinazohusu sifa za kugombea nafasi hiyo.

Baada ya mchakato huo wa usaili kukamilika majina ya wagombea yatapelekwa mbele ya Kamati kuu ya Chama hicho ambapo mchujo utafafanyika kwa ajili ya kupata majina ambayo yatapelekwa bungeni kupigiwa kura na wabunge.

Wanachama 178 wa chama hicho walichukua fomu za kuomba kuwania nafasi hiyo baada ya dirisha la uchukuaji fomu kufunguliwa Agosti Mosi, 2022 na kufungwa rasmi Agosti 10 Mwaka huu.

Wakati CCM ikiendelea na mchakato wa kuwapata wagombea, ACT-Wazalendo na CUF tayari wameshateua wanachama wao watakaoviwakilisha vyama vyao kuwania nafasi hizo.

ACT-Wazalendo kimewapitisha Ado Shaibu na Pavu Abdallah kukiwakilisha chama hicho kuwania nafasi hizo.

Kwa upande wa Chama cha CUF, kimepeleka majina 12 katika ofisi ya katibu wa Bunge, baada ya baraza kuu la uongozi la chama hicho, kuyapitisha.

Majina yaliyopitishwa na baraza hilo ni Adui Seif Kondo,Mashaka Ngole, Mneke Said,Muhamed Ngulangwa, Queen Lugembe, Sonia Magogo, Thomas Malima, Zainab Abdul na Zainab Amir wote kutoka Tanzania Bara,

Wengine ni Mohamed Habib Mnyaa, Husna Mohamed Abdallah na Anderson Emmanuel Ndambo wote kutoka Zanzibar.