CCM yabariki vigogo Dawasa kuwekwa kando

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Mapinduzi (CCM), Amos Makalla akiwa na Mjumbe wa Halmashauri ya Taifa ya chama hicho, mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba 'Gaddafi' wakikagua mradi wa tenki la maji la Bangulo wilayani Ilala.
Muktasari:
- Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema chama hicho kinaunga mkono uamuzi wa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aliyewasimamisha kazi vigogo wa mamlaka hiyo.
Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeubariki uamuzi wa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso wa kuwasimamisha kazi vigogo wawili wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa).
Kimesema Waziri Aweso asingechukua uamuzi huo, chama hicho kingechonganishwa na wananchi kuhusu hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili Julai 7, 2024 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla wakati akikagua mradi wa maji wa tenki la Bangulo wilayani Ilala litakalokuwa na ujazo wa lita milioni tisa.
Juni 30, 2024 akiwa katika ziara katika mkoa wa Dar es Salaam, Aweso aliagiza bodi ya Dawasa kuwasimamisha kazi Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo, Kiula Kingu na mkurugenzi wa uzalishaji na usambazaji maji, Shaaban Mkwanywe ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za utendaji usioridhisha.
Mbali na hao, wengine waliowekwa kando katika ziara hiyo ya Aweso ni Meneja wa Dawasa-Kinyerezi, Burton Mwalupaso, Mhandisi wa Kibamba, Regan Masami na kumuondoa kwenye nafasi yake Meneja wa Dawasa-Kibamba, Elizabeth Senkele wote kwa makosa ya kushindwa kuwajibika.
Kutokana na uamuzi huo, bodi ya wakurugenzi ya Dawasa ilimteua Mkama Bwire, kuwa kaimu ofisa mtendaji mkuu wa mamlaka hiyo. Kabla ya uteuzi huo, Bwire alikuwa mhandisi wa maji katika halmashauri ya Mji wa Kibaha.
"Dawasa fanyeni kazi Bwire nakufahamu tangu nikiwa Naibu wa Waziri wa Maji wakati ukiwa Tabora, sasa umeletwa mjini chapa kazi," amesema.
Makalla amesema katika ziara ya Waziri Aweso hivi karibuni mkoani Dar es Salaam, alikuwa anauliza maswali ya msingi kwa watendaji wa Dawasa lakini anapewa majibu mepesi.
"Alikuwa anauliza maji Ruvu yapo au hayapo anajibiwa yapo, ukienda kwenye tenki la Chuo Kikuu anauliza maji yanaingia, anajibiwa hayaingii. Sasa kwa nini kule maji yapo, hii maana yake mtu anapowajibishwa hakuna huruma.
"Inaonekana ni uzembe wa kiufundi na watu kutotimiza majukumu yao, naomba sana CCM ina dhamana na wananchi, hakuna sehemu chama hiki kitakwepa kuhusishwa na matatizo ya watu kwa sababu tulikwenda kunadi Ilani," amesema Makalla.
Amesema hakukuwa na namna kwa watendaji wa Dawasa wasichukuliwe hatua za kusimamishwa kazi na Waziri Aweso, akifafanua kati ya vigogo hao mmoja ni ndugu yake na baadhi ya watu wanajua.
"Sikutaka hata kupokea simu yake, kwa sababu ni sahihi alichokifanya waziri (Aweso), kwa hiyo msituchonganishe na wananchi waliotuamini, tunataka waendelee kutuamini fanyeni kazi kwa bidii.
"Tumbua tumbua iliyofanywa na Aweso imetusaidia, maana maji yapo hongera sana waziri," amesema Makalla ambaye leo ameanza ziara ya kukagua uhai wa CCM sambamba na miradi ya maendeleo katika wilaya tano za Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, amewapongeza Dawasa kwa kutekeleza mradi huo utakaochukua maji katika mtambo wa Ruvu Juu ambapo wananchi takribani 400,000 watanufaika baada ya kukamilika kwake Desemba mwaka huu.
"Maeneo yote korofi ikiwemo Kinyerezi, Kipunguni na Mwanagati yatapata maji kwa uhakika, tunaishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayoendelea kufanya ndio maana chama kinapita kuangalia mambo yanayohusu wananchi hasa maji.
"Dawasa chapeni kazi, mradi ukamilike kwa wakati mwakani tuna jambo letu, tunataka tutambe na tuwaambie CCM ndiyo chama kinachotekeleza," amesisitiza.
Awali, Mkurugenzi wa Miradi wa Dawasa, Ramadhani Mtindasi amesema ujenzi wa mradi huo unaendelea vizuri na utagharimu Sh36 bilioni ukinufaisha wananchi wa maeneo mbalimbali yakiwemo ya Mwanagati, Kipunguni, Majohe Mzinga na Kitunda.