CCM yafungua pazia la wagombea jimbo la Ushetu

Kipenga chapulizwa Jimbo la Ushetu, ni la Marehemu Kwandikwa

Muktasari:

  • CCM imewaalika wanachama wake wanaotaka kugombea ubunge katika jimbo la Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga, baada ya jimbo hilo kubaki wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa.

Kahama. Kufuatia hatua ya Tume ya Uchaguzi (NEC) kutangaza tarehe za uchaguzi wa viti vya ubunge katika majimbo mawili ya Konde Kaskazini Pemba na Ushetu mkoani Shinyanga, CCM Wilaya ya Kahama nayo imefungua milango kwa wanachama wake kuwania nafasi hiyo.


Uchaguzi katika Jimbo la Ushetu unatarajiwa kufanyika Oktoba 9 kufuatia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa kufariki dunia Agosti 2, 2021 katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.


Hivi  karibuni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dk, Wilson Mahela akiongea na Waandishi wa habari jijini Dodoma alisema kuwa ratiba ya uchaguzi huo ipo tayari imekamilika.


Mkurugenzi wa uchaguzi wa CCM Wilaya ya Kahama Emanuel Mbamange amebainisha hayo leo Agosti 30, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari wilayani hapa kuhusu uchukuaji wa fomu, akisema zitarudishwa Septemba 1 sasa kumi jioni.


Mkurugenzi huyo ambaye ni Katibu wa CCM wilaya amesema, baada ya hapo mchakato wa vikao vya ndani vya chama utaendelea hivyo, Septemba 13, ndipo famu za Serikali zitakapotolewa kwa wagombea.


Aidha Mbamange amesema, kwa sasa wagombea hawaruhusiwi kufanya kampeni zozote zile na kuwataka wawe watulivu katika kipindi chote hiki nakwamba uchaguzi wa kura za maoni wa kumpata mgombwea utakuwa wa wazi.


Ametaja sifa za mgombea atakayepitishwa, akisema ni mwenye kadi ya chama na anayejua kusoma na kuandika.