Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM yatahadharisha wananchi kumaliza kesi za ubakaji, ulawiti majumbani

Kenani Kihongosi, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, akizungumza na wananchi wa Tawi la Moivo, Shina namba saba, wilayani Arumeru, leo Ijumaa Juni 5, 2026.

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi (CCM) imekemea vitendo vya ubakaji na ulawiti, ikisisitiza kuwa ni uhalifu unaoharibu maisha ya watoto na familia na hivyo wananchi waache tabia ya kuficha wahalifu au kumaliza kesi hizo kwa makubaliano ya kifamilia.

Arumeru. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekemea vitendo vya ubakaji na ulawiti wa watoto na kuwataka wananchi kuacha tabia ya kuficha wahalifu au kumaliza kesi hizo majumbani kwa kupokea fedha, mifugo au makubaliano mengine ambayo yanadhoofisha juhudi za Serikali za kulinda watoto.

Kimesema Serikali imeweka sheria nzuri, lakini baadhi ya wazazi na walezi wanaficha wahalifu wa matukio hayo, jambo linalofifisha juhudi za kupambana na vitendo hivyo.

Maelekezo hayo yametolewa leo Ijumaa, Juni 5, 2026 na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi alipokuwa akizungumza na wananchi wa Tawi la Moivo-Shina Namba 7 wilayani Arumeru mkoani Arusha, baada ya wananchi kueleza wasiwasi wao kuhusu ongezeko la vitendo vya ubakaji, ulawiti na matumizi ya dawa za kulevya.

Kihongosi amesema CCM haitavumilia vitendo hivyo kwa kuwa vinaathiri afya ya akili ya watoto, kuharibu mustakabali wao na kuingiza huzuni katika familia na jamii.

Amesema pamoja na Serikali kuweka sheria kali dhidi ya wahalifu wa makosa hayo, mafanikio ya mapambano hayo yanategemea ushirikiano wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla, ikiwemo kutoa taarifa na ushahidi kwenye vyombo vya sheria.

“Kwenye taarifa mmetoa changamoto ya ukatili wa watoto ikiwemo ubakaji na ulawiti, ambapo nakiri haya matendo hayakubaliki. Ni matendo ambayo chama tunayakemea kwa nguvu zote kwa sababu unapomlawiti au kumbaka mtoto unamuathiri kisaikolojia, unamharibia malengo yake na kuleta simanzi ndani ya familia.

“Kama chama tunakemea matendo ya namna hii, tunayalaani na ndiyo maana mara zote Serikali imeweka sheria kali katika matendo haya kwamba ukibaka unaenda jela miaka 30 endapo ushahidi utakuwa umejitosheleza, lakini ukilawiti pia sheria iko wazi,” amesema.

Kihongosi amewataka wazazi na walezi kuwa walinzi wa watoto wao na wa watoto wa jamii kwa ujumla badala ya kukaa kimya wanapoona viashiria vya ukatili.

Aidha, amekosoa tabia ya baadhi ya wananchi kuficha wahalifu kwa kuogopa kutoa ushahidi au kukubali kumaliza kesi kwa makubaliano ya kifamilia.

“Mtoto anabakwa, taarifa inapelekwa polisi, lakini baadaye mashahidi wanapotea au familia zinamalizana kwa kupeana ng’ombe na fedha. Mnafifisha juhudi za Serikali katika kupambana na vitendo hivi. Tusinyooshe kidole kwa Serikali peke yake wakati sisi wenyewe hatutimizi wajibu wetu,” amesema.

Kihongosi amesema katika mambo hayo jamii haipaswi kuwa na aibu wala kigugumizi, bali ikemee vitendo hivyo.

“Nimekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha. Hapa jamii zetu matukio haya yanapotokea, watu wanaoficha wahalifu ni ninyi wananchi, siyo Serikali. Mtoto amebakwa, wewe una taarifa umeenda kuripoti kituo cha polisi, ukiitwa ukatoe ushahidi unaingia mitini. Wengine mnamalizana kifamilia, mnapeana ng’ombe, pesa na kesi inabadilika,” amesema.

“Mnafifisha juhudi za Serikali katika kupambana na haya mambo. Kama kweli tumedhamiria, tusinyooshe kidole kwa Serikali peke yake. Sisi kama chama, Serikali yetu na wananchi tuungane kwa dhamira ya dhati kwamba jambo limetosha, hatulitaki. Tusimame, tuache tamaa ya kupokea vitu vidogo na tulinde ustawi wa watoto wetu,” amesema.

Awali, mkazi wa Moivo, Vicky Alex, alihoji hatua zinazochukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa ubakaji na ulawiti baada ya baadhi yao kuonekana wakirejea mitaani licha ya kuripotiwa polisi.

“Watoto wetu wanabakwa na kulawitiwa, na mara nyingi tunaambiwa dawa za kulevya zinachangia hali hii. Tunapeleka taarifa polisi na tunakuwa tayari kutoa ushahidi, lakini baadaye tunawaona watuhumiwa wakirudi mtaani. Serikali inatusaidiaje kukomesha hali hii?” amehoji.

Naye Agness Lembris amesema matumizi ya dawa za kulevya yameendelea kuwa changamoto kubwa katika eneo hilo, akidai kuwa baadhi ya watuhumiwa hukamatwa lakini huonekana tena mitaani muda mfupi baadaye.

“Balozi na viongozi wa vitongoji wanatoa taarifa kwa polisi, watu wanakamatwa, lakini baadaye wanarudi mtaani na kuendelea na vitendo vyao. Tunataka kujua nini kifanyike ili kukomesha kabisa tatizo hili kwa ajili ya kulinda kizazi cha sasa,” amesema.

“Tunatafuta mwarobaini kuhusu suala la dawa za kulevya. Suala hili limekuwa sugu katika Kata ya Moivo. Kiongozi anaweza kuwa na taarifa na uthibitisho kabisa, anatoa taarifa polisi, mtu huyo anachukuliwa hatua.

Polisi watamchukua, lakini jioni mtu yule unamuona yuko mtaani kwa kejeli na matusi. Hali hii ya dawa za kulevya itaisha lini na tufanye nini kutokomeza? Kwa sababu kizazi cha sasa hatuna kabisa mwarobaini huo. Ni nani atauleta? Tunaomba majibu,” amesema.