CCM yatoa maagizo waliotajwa ripoti za CAG, Takukuru

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiongoza kikao Maalum cha kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa leo April mosi, 2023 Ikulu Jijini Dar es salaam.

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan ameongoza kikao cha kamati kuu ya chama hicho na kujadili masuala mbalimbali ikiwemo ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2021/22 na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Dar es Salaam. Chama tawala nchini Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka Serikali kuwachukulia hatua kwa waliohusika kwenye ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2021/22 na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

 Chama hicho kimetoa wito huo leo Jumamosi, Aprili 1, 2023 mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati kuu ya chama hicho, kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.

Ripoti hizo za CAG na Takukuru ziliwasilishwa Ikulu, Dar es Salaam, Machi 29, 2023 na kubainisha ubadhirifu wa fedha katika maeneo mbalimbali serikalini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jioni, ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Sophia Mjema amesema kamati kuu imesikitishwa na kuwepo baadhi ya maeneo mengine ambayo bado yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuondoa upungufu, udhaifu uliobainishwa, ikiwa ni pamoja na mifumo ya malipo na ukusanyaji wa mapato kutokusomana.

Amesema kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa umma wasiokuwa waadilifu, hali inayosababisha serikali kukosa mapato na kupata hasara, uwepo wa mashirika ya umma yanayojiendesha kwa hasara na vitendo vya ubadhirifu wa mali na rasilimali za umma, kama vile kuongeza bei za manunuzi ya Serikali.

“Kamati Kuu imeielekeza Serikali kuchukua hatua thabiti kwa wahusika wote waliobainika kuhusika katika ukiukaji wa sheria na kusababisha ubadhirifu wa mali na rasilimali za nchi,” alisema Mjema na kuongeza:

“…imetoa maelekezo kwa Serikali kuwafuatilia watu wote wanaotumia dhamana za uongozi vibaya na kushindwa kuweka maslahi ya nchi na uzalendo mbele katika nafasi walizoaminiwa kutumikia watu, badala yake wanaweka maslahi binafsi.”


Mjema amesema kamati kuu ya CCM, imeipongeza Serikali kwa kuratibu na kufanikisha vema ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris aliyetembelea nchi yetu kwa siku tatu kuanzia Machi 29 hadi 31, 2023.

Amesema ziara hiyo imeongeza uimara wa ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani na kufungua milango zaidi ya mahusiano yenye faida kwa maendeleo na ustawi kwa pande zote mbili, hususan katika maeneo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kukabiliana na magonjwa, uchumi, uwekezaji na ajira.

Mjema amesema kamati kuu imezipongeza Serikali zote mbili za CCM ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Samia na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Rais Hussen Ali Mwinyi kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 kwa vitendo, kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Watanzania wote.