CCM yazungumzia kauli ya Membe

CCM yazungumzia kauli ya Membe

Muktasari:

  • Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema yuko njiani kurudi mahali fulani akishamaliza kusikiliza uamuzi wa shauri lake lililopo mahakamani Oktoba 12, mwaka huu.

Lindi. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema yuko njiani kurudi mahali fulani akishamaliza kusikiliza uamuzi wa shauri lake lililopo mahakamani Oktoba 12, mwaka huu.

Licha ya Membe kutoweka wazi mahali atakaporudi lakini inaonekana atarejea Chama cha Mapinduzi (CCM) alikovuliwa uanachama Februari 28, 2020 kwa madai ya kukiuka maadaili na mwenendo usioridhisha tangu mwaka 2014

Jana akiwa kwenye mkutano wa ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Membe alisema anamuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan na yupo tayari kumpigia kampeni katika Uchaguzi Mkuu 2025.

Hata hivyo, Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Kanali Ngemela Lubinga alisema kama alivyoondoka, akiomba kurejea atajadiliwa.

“Akiomba vikao vinavyohusika vitamjadili, vinaweza kumpokea au kumkataa. Aliondoka na anataka kurudi, basi kuna taratibu na kanuni. Ataomba, atajadiliwa, akionekana ana sifa za kurudi basi atarudi. Asipofikia kiwango atakataliwa,” alisema Lubinga alipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu.

Julai, 2020 Membe alijiunga na chama cha ACT Wazalendo na baadaye aliteuliwa kuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu akichuana na John Magufuli (CCM) na Tundu Lissu (Chadema) na wagombea wengine.