Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCTV zilivyowaumbua Polisi Kenya mauaji ya mwanablogu Ojwang

Muktasari:

  • Video zilinasa matukio yote kuanzia Ojwang anafikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Nairobi saa 3:25 usiku wa Juni 7, 2025 akiwa katika gari aina ya Subaru na kuuawa kwa kipigo ndani ya mahabusu.




Moshi. Wiki iliyopita inaweza kuwa siku mbaya kwa Jeshi la Polisi Kenya, baada ya ushahidi wa video za usalama (CCTV) katika kesi ya mauaji ya mwalimu na mwanablogu, Albert Ojwang, kuwaumbua polisi waliodaiwa kujaribu kuficha mauaji hayo.

Video hizo zilinasa matukio yote kuanzia Ojwang anafikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Nairobi saa 3:25 usiku wa Juni 7, 2025 akiwa katika gari aina ya Subaru na kuuawa kwa kipigo ndani ya mahabusu, wakatoa mwili usiku huohuo kumpeleka hospitali.

Baada ya kuibuka kwa taarifa za kifo hicho, Polisi Kenya walitoa taarifa kwa umma wakieleza Ojwang alikamatwa Juni 7, 2025 na maofisa kutoka Kurugenzi ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa madai ya kuchapisha taarifa za uongo.

Mwanablog huyo alidaiwa kusambaza taarifa kupitia mtandao wake wa X akidai Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi (DIGP), Eliud Lagat alikuwa ana genge ‘la mafya’ likiwahusisha maofisa 12 wa Polisi na kwamba anachunguzwa kwa ufisadi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, Ojwang alifikishwa kituoni saa 3:35 usiku na kuwekwa mahabusu lakini katika ufuatiliaji (routine cell inspection), saa 7:39 usiku alipatikana akiwa hajitambui na mara moja aliwahishwa Hospitali ya Mbagathi.

Alipofikishwa hospitali hapo, ilibainika amefariki dunia na kulingana na polisi, walidai uchunguzi wa awali unaonesha alijibamiza mwenyewe ukutani akiwa mahabusu; kutokana na mazingira ya tukio hilo, maofisa watano waliokuwepo walisimamishwa kazi.

Miongoni mwa waliosimamishwa ni mkuu wa kituo (OCS) na wote waliokuwa zamu siku hiyo na wajibu wa uchunguzi wa tukio hilo ukakabidhiwa kwa Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA), iliyokuja kubaini mambo mazito.

Polisi katika taarifa yao ya awali walidai mfumo wa CCTV siku hiyo ulikuwa haufanyi kazi, lakini walikuja kuumbuliwa na wataalamu wa IT wa IPOA waliofanikiwa kurejesha video zote zilizokuwa zimefutwa ili kupoteza ushahidi.

Baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa mwili wa Ojwang uliothibitisha aliteswa kwa kupigwa na kunyongwa shingo, Julai 11, 2025 IGP Douglas Kanja, kupitia Bunge la Seneti aliomba radhi wananchi wa Kenya kuwa taarifa ya awali ilipotosha.

IGP Kanja aliliambia bunge hilo sio kweli kuwa kwa alijipiga kichwa ukutani, hivyo anaomba kuondoa taarifa yake ya awali na kuahidi kuwachukulia hatua maofisa wa polisi waliompa taarifa potofu kuwa Ojwang alijiua mwenyewe.

 “Kulingana na ripoti tuliyopokea kutoka IPOA, ni kweli madai ya kujigonga kichwa chake ukutani hayakuwa ya kweli; hivyo, naomba radhi kwa niaba ya Jeshi la Polisi na taifa kutokana na taarifa hiyo,” alisema IGP Kanja ndani ya bunge.

Kupatikana kwa video hizo ambazo awali zilifutwa (deleted) kumeibua hitaji la uwepo wa CCTV katika vituo vya polisi katika nchi za Afrika ikiwamo Tanzania, ili kulinda haki jinai na kupata ushahidi pale polisi wanapokiuka maadili ya kazi yao.

Kesi ya mauaji hayo inayowakabili watu sita wakiwamo maofisa wanne wa polisi inahusisha picha za kutisha za CCTV zinazofichua uzembe mkubwa wa polisi, ukosefu wa hatua za haraka za kimatibabu na jaribio la makusudi la kuficha ukweli.


Ushahidi wa CCTV

Maelezo yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Julai 20, 2026 katika Mahakama Kuu ya Kibera Jijini Nairobi, yanaeleza ushahidi wa mashahidi utaonesha kifo cha Ojwang hakuwa amejidhuru mwenyewe bali aliuawa.

OCS wa Kituo Kikuu cha Polisi Nairobi, Samson Talam na maofisa wenzake James Mukwana na Peter Kimani pamoja na raia John Gitau, Jim Ambao na Britan Njue walikuwa pamoja na marehemu katika mahabusu ambayo aliuawa.

Naibu DPP, Gikui Gichuhi aliieleza Mahakama:“Upande wa mashtaka utaonesha hii ni kesi ya matumizi mabaya ya madaraka ya maofisa wa polisi, ambao walikuwa na wajibu wa kikatiba wa kulinda maisha Ojwang na wananchi wengine.”

“Tutaonesha kifo chake kilisababishwa na kipigo na kwamba mauaji yake yalipangwa. Pia, tutaonesha kulikuwa na njama za makusudi za maofisa wa Polisi kuingilia ushahidi kwa kufuta video za CCTV zilizonasa matukio.”


Ushahidi wa Mtaalamu

Mmoja wa mashahidi aliyetoa ushahidi wake, Alon Okwako, ambaye ndiye aliyesaidia kufunga mfumo wa CCTV kituoni hapo, alieleza Juni 9, 2024, aliitwa kushughulikia mfumo huo baada ya mofisa wa IPOA kufika kituoni hapo.

Baada ya kupewa nywila ya mfumo huo wa CCTV, alikagua kifaa kinachotunza kumbukumbu (DVR), alibaini ilikuwa imezimwa, mfumo wa umeme umechomolewa na kifaa kinachofamika kama Hard Drives kikiwa kimeondolewa.

Allieleza Mahakama kumbukumbu zote zilizorekodiwa kati ya Juni 6 na 7, 2025 zikiwa zimefutwa na kwamba kufutwa huko kwa DVR kwa vyovyote vile kulifanywa kwa makusudi na mtu mwenye nafasi ya kuingia kwenye mfumo.

Shahidi namba 2 ambaye utambulisho wake ulifichwa na kupewa utambuzi wa D.A.N ambaye ni mtaalamu wa CCTV ambaye alishiriki kufunga kamera zaidi ya 20 kituoni hapo, alielezea nini alikipitia baada ya mauaji ya mwanablogi huyo.

Alieleza Juni 8, 2024 alielekezwa na bosi wake ambaye amepewa utambulisho wa A.A kwenda kumuona OCS na alimkuta anamsubiri ambapo alimtaka kupakua (retrieve) video zilizorekodiwa Juni 6 na 7, 2025.

Kulingana na ushahidi wake, baada ya kuwaeleza kuwa hawezi kufuta video moja moja kwa tarehe hizo labda kama Hard drive itakuwa formatted (kufutwa), OCS huyo (Tallam), alimwagiza kufuta kila kitu kwenye kifaa hicho cha CCTV.

Kwa kutumia neno la siri la mfumo huo na Tallam, alifuta kumbukumbu zote ambapo OCS huyo alimlipa Ksh3,000 (Sh60,000).

Shahidi huyo alieleza siku iliyofuata, aliitwa tena kituoni hapo ili kuondoa hard drives za mfumo huo na kuweka nyingine ambapo alikwenda na hard drives mbili na kulipwa Ksh20,000 (Sh400,000).

Upande wa mashitaka ulimwita pia shahidi ambaye alipewa utambulisho wa A.A.A ambaye ni Ofisa wa Polisi aliyekuwa akifanya kazi chini ya OCS, ambapo anasema alipofika ofisini alimkuta OCS akizungumzia kifo cha mshukiwa mahabusu.

Kutokana na mazingira hayo, alishauri mfumo wa CCTV uangaliwe ambapo yeye, OCS na Inspekta Nganga walipitia video zilizokuwa zimenasa matukio yote.

Alieleza katika video hizo ambazo zilichezeshwa mahakamani, zinamuonesha ofisa wa polisi aliyemtambua kuwa ni Kimani akizungumza na watu wawili, wakizungumza karibu na mlango wa chumba cha mahabusu.

Baadaye aliongezeka mtu mwingine anayeonekana akikimbia kuelekea katika mahabusu aliyokuwepo Ojwang na baadaye watatu hao walionekana kubeba kitu kilichoonekana ni kizito kuelekea kilipo chumba cha mwisho cha mahabusu.

Kulingana na shahidi huyo, OCS alimtambua mmoja wa watu hao kuwa ni Mukwana, kabla hajamwagiza kumuita mtaalamu wa mfumo wa CCTV na kumtaka afute kumbukumbu zote za Juni 6 na 7, 2025.

Shahidi huyo alimnukuu OCS akisema:“Hii kamera inatuletea shida, futa kila kitu,” ambapo upande wa mashitaka ulikuwa umeeleza kulikuwa na jitihada kubwa za kuficha ni kitu gani kilitokea usiku Ojwang alipoingizwa mahabusu.

Hata hivyo, wataalamu kutoka IPOA walifanikiwa kurejeshwa kumbukumbu zilizofutwa, ambazo zinaonesha siku anafikishwa kituoni alikuwa ni mzima wa afya na aliposhushwa katika gari aina ya Subaru alipewa simu na kupiga.

Wataalamu hao waliongozwa na Mkuu wa Idara ya Uchunguzi wa Kisayansi wa IPOA, Joseph Mutua ambaye katika ushahidi wake alichezesha video hizo zinazoonesha tangu Ojwang anafikishwa kituoni na kutolewa akiwa mfu.

Katika video hizo, saa 4:56 usiku zinaonesha mmoja wa watuhumiwa, John Ngige akitoka katika mahabusu huku mikono yake ikionekana kuwa na damu huko Brian Muriuki akionekana akiwa ameshika mkanda au kamba.

Kulingana na CCTV hizo, saa 7:20 usiku, maofisa wanne wakiwa wamevaa gloves, wakiongozwa na OCS Samson Tallam, wanaonekana wakiwa wamembeba mtu ambaye hakuwa anajigusa, kutoka mahabusu na kumtoa hadi nje.

Saa 7:35 usiku, video za CCTV kutoka hospitali ya Mbagathi zinaonesha maofisa wa polisi wakiwasili hospitalini hapo na mwili wa Ojwang, wakasimama dakika kadhaa nje kisha kumwingiza hospitali na baadae kuondoka na mwili huo.

Katika shauri hilo, kuna maelezo ya ungamo kutoka kwa PC James Mukwana aliyoyaandika mbele ya maofisa wa IPOA akielezea kila kitu kinachofanana na video hizo za CCTV akidai agizo la kumfunza adabu Ojwang lilitolewa na OCS.

Kulingana na maelezo hayo, OCS alimwambia suala la kumfunza adabu Ojwang ni maelekezo ya DIGP Eliud Lagat, ambapo waliotekeleza kipigo hicho ni mahabusu wengine waliopewa jukumu hilo la kumshikisha adabu Ojwang.

Kutokana na tuhuma hizo, Juni 16, 2025, aliamua kujiweka pembeni ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo. Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa katika kikao cha Mahakama Kuu kitakachofanyika Desemba chini ya Jaji Diana Mochache.