Vijana 4 wauawa tukio la uporaji wa ng’ombe

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya akionyesha ng'ombe walioibiwa katika Kijiji cha Mbatamila wilayani Tunduru. Polisi imefanikiwa kuwapata ng’ombe 159 kati 200 walioibwa kwa James Magese mkazi wa kijiji hicho. Picha na Joyce Joliga

Muktasari:

  • Ni miezi miwili tangu wapotee wakichunga ng’ombe. Baadhi ya ng’ombe waliokuwa wakiwachunga wakutwa zizini, mmiliki atokomea.

Songea. Vilio na simanzi vimesikika kwa wafugaji wa jamii ya Kisukuma wakiwalilia vijana wao wanne wanaodaiwa kuuawa na miili yao kufukiwa kwenye kaburi moja.

Habari zilizopatikana kutoka kwa mzazi wa mmoja wa vijana hao, miili ya vijana hao ilikuwa imefukiwa kwenye shimo na juu yake kuwekwa kinyesi cha ng’ombe katika Kijiji cha Mbatamila wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.

Taarifa za mzazi huyo ambazo zimeungwa mkono na uongozi wa kijiji lilipotokea tukio hilo, pia zilibainisha kukamatwa kwa baadhi ya ng’ombe waliokuwa wameibwa.

Mapema, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya licha ya kukiri kukamatwa kwa ng’ombe 159 kati ya 200 waliokuwa wameibwa.

Alipoulizwa kuhusu tukio la kufukuliwa kwa miili hiyo, Chilya alisema upelelezi wa suala hilo umeshakamilika na taarifa rasmi itatolewa kesho.

“Sisi tunafuatilia na taarifa kamili tunaitoa Ijumaa kuhusu hicho ambacho kimekuwa kimelalamikiwa. Upelelezi umeshakamilika kila kitu kimekamilika, Ijumaa tuna press release (taarifa kwa vyombo vya habari.),” alisema Kamanda Chilya, jana.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro naye alipoulizwa alisema suala hilo linashughulikiwa na kamanda wa polisi wa mkoa.


Ilivyobainika

Akizungumza na Mwananchi juzi, James Magese aliyepoteza watoto wake wanne, pamoja na kuwashukuru polisi kwa kukomboa ng’ombe wake 159, amelitaka jeshi hilo liwakamate wahusika wa tukio hilo.

“Ombi letu tunaomba Serikali itusaidie, haki itendeke,” alisema Magese.

Alisema waliouawa katika tukio hilo ni mtoto wake wa kwanza Didi Magese, wa pili Msanika Magese na wa tatu Leonard Madumila pamoja na Amos ambaye ni mtoto wa ndugu yake.

Alisema wamekamata vielelezo kwenye zizi la muuzaji na msafirishaji mkubwa maarufu wa ng’ombe (jina limehifadhiwa).

Alisema miili ya watoto wake ilikatwakatwa kisha wauaji wakapora ng’ombe wake.

Kwa mujibu wa Magese, vijana wake waliondoka Sumbawanga mkoani Rukwa Julai 13, 2022 na tangu wakati huo hawakuonekana tena na ilikuwa akiwapigia simu hawapatikani.

“Mwanzoni nilidhani ni kwa sababu wapo porini ndiyo maana hawapatikani, lakini kumbe wameuawa.

“Didi nimemsomesha kwa gharama shule ya sekondari Iyunga, Mbeya, kamaliza kidato cha nne na kuuawa,” alieleza kwa uchungu.

Baada ya vijana hao kutoonekana, Magese akishirikiana na ndugu zake walianza kuwafuatilia hadi Tunduru mkoani Ruvuma ambako walibaini viashiria vya kuuawa kwao walipoona mifupa miwili ya binadamu, fimbo na nguo ya mmoja wa vijana hao.

“Tulifuatilia fimbo hiyo tulisikia harufu kali ilitoka, ndipo tulimpigia simu mwenyekiti wa kijiji tukamjulisha kupotelewa na watoto wetu, naye akatueleza tusifanye chochote, tusubiri tutoe taarifa polisi ili tufuate utaratibu wa sheria,” alisema.

Alifafanua kuwa baada ya kumfuata mwenyekiti kilometa 20 kutoka kwenye zizi walilotambua viashiria vya mauaji, waliongozana naye hadi Kituo kikuu cha Polisi Wilaya ya Tunduru kilomita 76 na kutoa walipokuwa.

“Uongozi (wa polisi) ulituambia turudi na mwenyekiti kijijini kwa kuwa utaratibu ni mrefu ikiwa pamoja na kupata kibali cha kwenda kufukua miili na kisainiwe na hakimu.

“Tukalala kwa mwenyekiti na kesho yake majira ya saa 11 alifajiri, tulianza kufukua na kubaini kuwepo kwa vichwa vitatu na miili minne ya vijana, kichwa kimoja hakipo na walimtambua mmoja wa watoto kwa nguo zake.

“Tukakusanya yale mabaki na kuyaweka kwenye mifuko tofauti na kuondokana nayo kuelekea Tunduru hadi sasa hatujakabidhiwa, tumeambiwa vipimo vimesafirishwa kwenda Dar es Salaam, tusubiri vipimo,” alisema Magese.

Baadaye alisema walikubaliana kutawanyika kutafuta ng’ombe walioibiwa na walipofika porini kenye kambi ya mfugaji (jina limehifadhiwa) iliyopo Kijiji cha Mtyangimbole wilaya ya Songea walipokuta baadhi ya ng’ombe.

“Tukasema hatutaweza kukubali kurudishiwa ng’ombe 19 hadi pale mfugaji huyo atakapokamatwa kwani ndiye mtuhumiwa kwa sababu vielelezo vya ng’ombe vimekamatwa kwake, atueleze watoto wako wapi?

Naye Magese Nguku mmoja wa wafugaji hao alisema alijitahidi kupeleleza kwa kutembelea maeneo ya wafugaji akijifanya kutafuta malisho, alifika Kitongoji Kakonko na walielekezwa makambi ya mifugo yalipo.

“Tulimwomba kiongozi wa kijiji atunze siri na kisha tukampa barua na akatupa kibali kutafuta ng’ombe wetu. Huku ndipo tulipobaini kuwepo zizi lililokuwa na ng’ombe wetu na tuktoa taarifa polisi,” alisema.

Babu wa marehemu hao, Daud Magese, alisema kwa sasa wanasubiri majibu ya vipimo vya vinasaba walivyopelekwa Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbatambila, Mohammed Ally alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa tayari mifupa ya vijana wanne na mafuvu ya vichwa vitatu vya wafugaji vimekabidhiwa kwa polisi wa Wilaya ya Tunduru kwa uchunguzi zaidi.

“Huu ni unyama na ukatili mkubwa, nawapa pole wazazi waliopoteza watoto wao, kwani baada ya kuwafukia, wauaji waliweka vinyesi vya ngombe juu ya kaburi ili kusijulikane, lakini Mungu hakupenda, amewaumbua. Naamini Jeshi la Polisi litasaidi kuwakamata hao wauaji na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Alifafanua kuwa wafugaji hao wamefuata taratibu zote za kisheria na walikuwepo kihalali kijijini hapo na hawajawahi kuwa na rekodi yoyote ya kihalifu.

Wafugaji watambua ng’ombe

Tayari wafugaji zaidi ya 200 kutoka mikoa mbalimbali nchini ambao wamewahi kuibiwa ng’ombe kwa vipindi tofauti, wameweka kambi Kijiji cha Mtyangimbole kwenye zizi la Serikali ambapo ng’ombe waliokamatwa wamehifadhiwa, wakisubiri taratibu za kisheria ili wakabidhiwe mifugo yao.

Chilya alisema ng’ombe hao walipatikana kufuatia taarifa iliyotolewa na Magese aliyegundua kuibiwa mifugo yake zaidi ya 200, punda wawili pamoja na kondoo.