Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCWT yawaonya wafugaji Moshi kuingiza mifugo kwenye mashamba

Muktasari:

  • Malalamiko ya wakulima wa Kata ya Mabogini Moshi kuhusu mifugo kuharibu mazao na madai ya kushambuliwa na kuumizwa yameifanya CCWT kuonya dhidi ya vitendo vya kuvunja amani.

Moshi. Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Kanda ya Kaskazini, kimekemea vitendo vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya wafugaji vya kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima kwa nguvu na kuwashambulia wananchi wanaojaribu kuzuia uharibifu wa mazao, kikisisitiza kuwa vitendo hivyo ni makosa ya jinai na vinahatarisha amani.

Kauli hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya wakulima wa Kitongoji cha Sanya Line A, Kijiji cha Mabogini, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wanaodai mifugo imekuwa ikiingia mashambani na kuharibu mazao yao, huku baadhi ya wananchi wakijeruhiwa katika makabiliano na wafugaji wanaodaiwa kutoka wilaya za Kiteto na Simanjiro kutafuta malisho.

Kwa mujibu wa wakulima hao, changamoto hiyo imeendelea kwa takribani miaka mitano, ambapo mifugo huingia mashambani hasa kipindi cha mazao, na kusababisha hasara kubwa kwa wakulima.

Baadhi ya wananchi kitongoji cha Sanya Line A kata ya Mabogini wilaya ya Moshi wakilalamikia adha ya mifugo kuvamia mashamba yao.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sanya Line A, Thomas Ngonyani, amesema baadhi ya mifugo hiyo inaonekana kutoka nje ya Wilaya ya Moshi kutokana na chapa zilizopo kwenye miili ya ng'ombe kutofanana na zile zinazotumika katika eneo hilo.

Akizungumza leo Jumatatu, Julai 20, 2026 kuhusu mgogoro huo, Naibu Katibu wa CCWT Kanda ya Kaskazini, Elifuraha Ndure amesema chama hicho hakitavumilia vitendo vinavyoweza kuvuruga uhusiano kati ya wakulima na wafugaji.

“Kitendo cha kuingiza mifugo kwenye shamba la mtu kwa makusudi na kumshambulia anayelalamika ni kosa la jinai. Hatuwezi kuruhusu vitendo vinavyohatarisha usalama na amani ya wananchi,” amesema Ndure.

Amesema ikiwa mfugaji anahitaji eneo la malisho, anapaswa kufuata taratibu zilizowekwa na kuzungumza na viongozi wa maeneo husika badala ya kutumia nguvu.

Sehemu ya shamba la ekari mbili inayodaiwa kuvamiwa na mifugo katika kata ya Mabogini wilaya ya Moshi.

Kuhusu madai ya baadhi ya wakulima kuwa wafugaji hujigamba kuwahonga viongozi na kushinda kesi kirahisi mahakamani, Ndure amevitaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua dhidi ya yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo vya rushwa.

Naye Mwenyekiti wa CCWT Kanda ya Kaskazini, inayojumuisha mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, Rumay Bajuta amesema kila Mtanzania ana haki ya kuhamia eneo lolote nchini, lakini anapaswa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

“Kuhama si kosa, lakini mfugaji anapofika eneo jipya anatakiwa kuripoti katika ofisi ya kijiji na kwa maofisa mifugo. Kulisha mifugo kwenye shamba la mtu au kumshambulia anayepinga ni uhalifu unaopaswa kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava alisema Serikali inafahamu changamoto hiyo na kwamba baadhi ya mifugo hutoka maeneo ya nje ya wilaya, ikiwemo Simanjiro, na kuingia Moshi bila kufuata taratibu za uhamishaji.

Amesema Serikali imekuwa ikitumia kamati za usuluhishi zinazowashirikisha wakulima na wafugaji kutafuta suluhu ya migogoro hiyo, huku akisisitiza kuwa matukio ya kushambuliwa kwa wananchi yanapaswa kushughulikiwa kama makosa ya jinai.

CCWT Kanda ya Kaskazini imesema itakutana na viongozi wa wilaya pamoja na wafugaji waliopo katika maeneo yenye migogoro ili kutoa elimu kuhusu uzingatiaji wa sheria za vijiji na taratibu za uhamishaji wa mifugo, kwa lengo la kuzuia migogoro na kuimarisha mahusiano kati ya wafugaji na wakulima.