Chadema mtegoni ikitakiwa na msajilli iweke Rais katika ofisi

Sunday September 12 2021
chadema pc

Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeitaka Chadema hadi Januari iwe imeweka picha ya Rais katika ofisi za viongozi wake.

Chama hicho imetakiwa kufanya hivyo kuwa ni taasisi ya umma na ni utamaduni kwa ofisi hizo kuwa na picha ya Rais.

Hayo yalibainishwa juzi na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza wakati akifanya ukaguzi wa chama hicho kuangalia jinsi kinavyotekeleza Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi.

Nyahoza alisisitiza kwamba ofisi za vyama vya siasa ni ofisi za umma, hivyo, ni vizuri wakaendeleza utamaduni wa kuwa na picha ya Rais kwenye taasisi za umma.

“Hii ni ofisi ya umma, ni vizuri kukawa na picha ya Rais ukutani, si unaweka picha ya katibu mkuu. Huu ni ushauri tumewapa, tutapita Januari kuona kama wamelifanyia kazi,” alisema Nyahoza alipozungumza na wanahabari.

Akizungumzia suala hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema Msajili amekuta mambo katika chama hicho yamekaa vizuri ndiyo maana akagundua hakuna picha ya Rais.

Advertisement

“Tumempokea Msajili, wamepitia taarifa zote walizozihitaji wamekuta mambo yako vizuri, ni mambo madogo madogo ndiyo yanahitaji kufanyiwa kazi. Kama angekuta mambo makubwa, asingekumbuka kuangalia picha ya Rais,” alisema Mwalimu.


Apongeza Chadema Digital

Baada ya ukaguzi huo, ofisi ya msajili imekipongeza chama hicho kwa kuanzisha mfumo wa Chadema Digital ambao unakiwezesha kuandikisha wanachama na kukusanya ada kidijitali.

Hata hivyo, imekitaka chama hicho kufanyia kazi changamoto mbalimbali ambazo ameziona kwenye ukaguzi uliofanywa na ofisi yake kabla ya Januari 2022.

Nyahoza alisema katika ukaguzi huo, wamebaini Chadema inafanya vizuri katika utunzaji wa kumbukumbu za fedha na kuwa ndiyo maana mwaka wa fedha uliopita ilipata hati safi.

Licha ya mfumo wa Chadema Digital kukiwezesha kuwatambua wanachama na kukusanya ada kidijitali, Nyahoza alisema chama hicho kinakabiliwa na tatizo la uwekaji kumbukumbu za mali za chama kwa kuzingatia matakwa ya kanuni za utunzaji wa kumbukumbu hizo, pia haridhishwi na ukusanyaji wa mapato ya chama.

“Tumebaini hili ni changamoto kwao, hawarekodi namba za mali za chama. Namba ya mali za chama lazima zirekodiwe katika orodha ya mali, kama ni kiti basi unaandika namba ya kiti na unaainisha aina ya kiti hicho, kama ni cha mezani au ni sofa,” alisema Nyahoza.

Alisema pia wamelibaini katika chama hicho kiliandaa bajeti na kuanza kuitumia kabla Kamati Kuu haijaidhinisha matumizi hayo kwa mujibu wa katiba yao, suala ambalo pia lilibainishwa na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).

Akizungumzia ukaguzi huo, Mwalimu alisema chama hicho kina mifumo imara ya utunzaji wa kumbukumbu na sekretarieti yao ina wataalamu wenye sifa.

“Mfumo wetu hauruhusu mtu kushika fedha. Fedha zote zinakwenda benki. Hili ni jambo ambalo hata wao (timu ya msajili) wamelipenda na tumeonyesha kwa vitendo,” alisema Mwalimu.

Hata hivyo, Mwalimu aliongeza kuwa bado wana kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha Chadema kinakuwa chama cha kidijitali na kinakuwa cha mfano hapa nchini.

Imeandikwa na Irene Meena na Peter Elias

Advertisement