Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema Njombe yataka viongozi kuimarisha chama

Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Mkoa wa Njombe, Baraka Kivambe

Muktasari:

  • Katika uchaguzi huo, wajumbe wa mkutano mkuu watawachagua viongozi wa kitaifa akiwamo mwenyekiti na makamu wenyeviti wa Bara na Zanzibar.

Njombe. Wajumbe wa mkutano mkuu wa Chadema Mkoa wa Njombe watakaoshiriki kwenye uchaguzi mkuu wa chama hicho Januari 21, wametakiwa kuchagua viongozi ambao wanaweza kukiimarisha chama hicho badala ya kukibomoa na kushindwa kufikia malengo.

Katika uchaguzi huo, wajumbe wa mkutano mkuu watawachagua viongozi wa kitaifa akiwamo mwenyekiti na makamu wenyeviti wa Bara na Zanzibar.

Viongozi wanaochuana katika nafasi ya uenyekiti ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti (Bara), Tundu Lissu, kada wa chama hicho, Odero Charles Odero na Romanus Mapunda.

Katika nafasi ya umakamu mwenyekiti Bara wanaochuana ni Ezekia Wenje na John Heche.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Januari 15 mjini hapa, Katibu wa Chadema Mkoa wa Njombe, Baraka Kivambe amesema kutokana na kuwepo kwa wagombea wenye uwezo mkubwa katika nafasi za juu, ni muhimu wajumbe kutumia akili zao zote ili kumchagua viongozi bora na siyo kuchagua kwa mihemko.

"Sisi Chadema tunaamini hakuna mtu aliyekuwa maarufu kuliko taasisi, mimi Kivambe katibu wa mkoa leo naweza kuondoka, lakini taasisi itabaki. Hivyo, siwezi kusema pasipo mimi taasisi haiwezi kwenda hapana," amesema Kivambe.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Njombe, Seth Vegula amesema kwa sasa chama hicho kinamuhitaji mwenyekiti jasiri ambaye atahakikisha chama hicho kinafikia malengo yake ya kushinda katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu.

"Chadema kwa sasa inahitaji viongozi ambao wataleta mabadiliko na fikra mpya na kutuwezesha kushinda kwenye uchaguzi mkuu," amesema Vegula.

Kada wa Chadema mkoani humo, Okoka Mbwilo amesema kwa namna hali ilivyo ya kisiasa hapa nchini kuna kila sababu ya kupata kiongozi ambaye atawaunganisha wanachama na siyo kuwagawa.

"Tunahitaji mabadiliko ambayo yatatusaidia kukiunganisha chama chetu na siyo kukivuruga," amesema Okoka.