Ni mnyukano wa Sugu, Msigwa Chadema

Muktasari:

  • Siku chache baada ya Chadema kutangaza mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu katika kanda nne kati ya 10 za chama hicho, baadhi ya makada wameanza kupigana vikumbo kuchukua fomu kuwania uenyekiti.

Mbeya. Unaweza kusema hii ni habari njema kuhusu kuanza rasmi kwa mtifuano wa kuwania ‘ubosi’ wa kanda nne kati ya 10 za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katika kanda hizo, tayari wagombea wameshaanza kuchukua fomu na wengine wanajiandaa kufanya hivyo kabla ya dirisha kufungwa ifikapo Aprili 22, 2024.

Hii inaelezwa kuwa ni hatua muhimu katika mchakato wa demokrasia wa chama na Watanzana wengi wanatarajia kuona ushindani wa heshima na uwazi.

Uchaguzi wa kanda nne za Victoria, Nyasa, Serengeti na Magharibi za Chadema unatarajiwa kufanyika Mei, mwaka huu.

Kanda hizo zinaundwa na mikoa ya Katavi, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera, Tabora, Kigoma na Mara.

Hata hivyo, duru za siasa zinaeleza mchuano mkali unatarajiwa kuwa katika kanda ya Nyasa ambako mwenyekiti anayemaliza muda wake, Mchungaji Peter Msigwa anatetea nafasi hiyo na atachuana na mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu 'Sugu'.

Mchuano huo unanoga zaidi baada ya makada wanawake wa Chadema kutoka mikoa mitatu nao kujipanga kumchukulia fomu Mchungaji Msigwa, wakilenga kumwezesha kutetea nafasi hiyo kwa miaka mitano mingine.


Taarifa ambazo Mwananchi Digital imezipata, fomu ya Msigwa itachukuliwa leo jioni Aprili 16, 2024 katika ofisi za kanda za Chadema zilizopo mkoani Mbeya, kisha kesho itapelekewa mbunge huyo wa zamani wa Iringa Mjini.

Mwananchi lilimtafuta mratibu wa mchakato huo, Christina Kananda aliyesema wameamua kumchukulia fomu Msigwa kutokana na utendaji kazi bora alioufanya ndani ya miaka mitano ya kuiongoza kanda hiyo.

"Leo jioni tutamchukulia fomu na kesho alfajiri tutampelekea mkoani Iringa. Ttumekodi gari ya coaster tupo takribani 30 kutoka majimbo ya Mbeya Mjini, Lupa na mikoa ya Songwe na Rukwa. Kuna wenzetu wengine zaidi 15 watajiunga nasi kutoka Njombe watakuwa na gari lao," amesema Kananda.


Kananda amesema Mchungaji Msigwa ameiweza kanda ya Nyasa kwa kuhakikisha anajenga chama hicho kwa kufanya ziara katika majimbo 31 yaliyopo katika kanda hiyo yenye mikoa mitano.

"Kanda ya Nyasa tunamhitaji Msigwa kuliko yeye anavyotuhitaji sisi na tuna imani naye kubwa katika kuiongoza kanda yetu," amesema Kananda.


Msigwa afunguka

Akizungumza na Mwananchi Digital kuhusu kupelekewa fomu kesho Aprili 17, 2024, mjumbe huyo wa kamati kuu amesema hatua hiyo inaonyesha mapenzi makubwa kwake na imani walioinyesha makada hao dhidi yake.

"Ni heshima kubwa kwangu kama watu wanasafiri umbali mrefu kukuletea fomu, nitaipokea kwa unyenyekevu mkubwa na wameona mchango wangu kwao sitowaangusha. Kipaumbele changu kitakuwa kuhakikisha chama kinashinda katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongaji, udiwani na ubunge," amesema  Mchungaji Msigwa.


Sugu: Nitachukua fomu

Kwa upande wake, Sugu amesema ndani ya siku zijazo atakuchukua fomu kuwania nafasi hiyo kabla ya dirisha la uchukuaji na urejesha wa mchakato huo kufungwa Aprili 22.

"Leo jioni nitajua nitachukua lini fomu kabla ya dirisha kufungwa, lazima nitakuchukua kabla ya dirisha kufungwa.Nikichukua fomu nitasema, kwani nagombea na vipaumbele vyangu kwa umma.

"Nina sababu nzuri za kuwania kiti hiki ndio maana naungwa mkono...Tupo vizuri watu wasubiri," amesema Sugu aliyewahi kuongoza Mbeya Mjini kwa miaka 10.


Magharibi

Katibu wa kanda ya magharibi, Ismail Kangeta amesema hadi sasa makada wawili wameonyesha nia ya  kuchukua,  akiwemo wakili mwandamizi, Ngasa Mboje na Emmanuel Anthony.

Mboje amesema amewahi kuwa makamu mwenyekiti wa kanda hiyo mwaka 2016-2019, nafasi iliyompa fursa ya uzoefu wa kiuongozi, hiyo ameamua kuwania uenyekiti ili kuongeza nguvu katika kuiimarisha kanda ya magharibi.

"Niliwahi pia kukaimu nafasi mwenyekiti wa kanda baada ya Kasugu Bilago kufariki dunia mwaka 2018, nilitumikia nafasi hiyo hadi mwaka 2019, sasa narejea tena nikitaka kuimarisha kanda na umoja ndani ya magharibi," amesema Mboje.

Wakili mwingine Peter Madeleka amesema alitingwa na majukumu, lakini ameliona tangazo la kuchukua na kurejesha fomu, hivyo atapanga ratiba kwenda kuangalia hizo fomu.


Serengeti

Katibu wa kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami amesema hadi sasa hakuna kada aliyejitokeza kuchukua fomu, akisema watajitokeza kwa kuwa muda bado upo.

Mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini, mkoani Mara na mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, John Heche ni miongoni mwa majina yanayotajwa kuwania kiti hicho, amesema bado anatafakari kama atagombea au la.


Victoria

Katika kanda ya Victoria inayoongozwa na mbunge wa zamani wa Nyamagana mkoani Mwanza, Ezekiah Wenje amesema leo atachukua fomu kutetea nafasi yake  na anatarajiwa kuchuana na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Pambalu anayetajwa kuitaka nafasi hiyo kwa mara kwanza.

Alipotafutwa Pambalu amesema kesho Jumatano Aprili 17, 2024 atachukua fomu akisema yupo mbioni kumaliza muda wake wa kuongoza Bavicha, lakini amegundua kanda ya Victoria yenye mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera inahitaji mabadiliko ya kisiasa.

"Ninaamini katika mabadiliko, hivyo nagombea ili kuleta mabadiliko ya kisiasa kuendana na matukio yanayofuata ya kiuchaguzi," amesema Pambalu.