Chadema yasusia uchaguzi Ushetu

Tuesday September 14 2021
chademapic

Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Shinyanga Emmanuel Ntobi

By Suzy Butondo

Shinyanga. Chama cha Chadema Mkoa wa Shinyanga, kimesema hakitashiriki uchaguzi mdogo wa marudio katika Jimbo la Ushetu.

Mbali na uchaguzi kwenye jimbo hilo ambao unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wake, Elias Kwandikwa, Chadema pia kimetangaza kutoshiriki uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Ndembezi kwenye Manispaa ya Shinyanga.

Kwandikwa, ambaye alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) alifariki dunia Agosti 2, mwaka huu.

Soma zaidi:CCM yampitisha Msuya kugombea Udiwani Kileo Mwanga

Akizungumza leo Jumanne Septemba 14, 2021 Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi amesema Baraza la Uongozi mkoa limejadili na kukubaliana kutekeleza azimio la chama la kutokushiriki uchaguzi wowote wa marudio hadi pale watakapopata Tume Huru ya Uchaguzi.

Ntobi amesema hakuna mchakato wowote wa ndani ya chama uliofanyika ama unaofanyika kuhusu uchaguzi mdogo kwa jimbo wala kata kama ambavyo Katiba ya chama ya mwaka 2006 toleo la 2019 ibara za 7.3.9(a), 7.4.10(a), 7.4.10(r) na 7.7.16(p) zinavyotaka.

Advertisement

Soma zaidi:Cherehani, Habib kugombea ubunge Ushetu na Konde

"Tunawasihi wanachama wetu kuendelea  kuelimishana kuhusu madai ya Katiba mpya, Tume huru ya uchaguzi na kuendelea kujisajili kidigitali na kutumia Chadema digitali kwa kuwa kesho yetu ni nzuri kuliko jana," amesema Ntobi.

Tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza nafasi mbili za ubunge katika majimbo ya Konde mkoa wa Kaskazini Pemba na Ushetu, Shinyanga.


Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera amesema uchaguzi huo mdogo wa marudio umepangwa kufanyika Oktoba 9,2021.

Advertisement