Cherehani, Habib kugombea ubunge Ushetu na Konde

Cherehani, Habib kugombea ubunge Ushetu na Konde

Muktasari:

  •  Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imewateua Emanuel Cherehani na Mbarouk Amour Habib kuwa wagombea ubunge katika majimbo ya Ushetu na Konde.

  

Dodoma. Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imewateua Emanuel Cherehani na Mbarouk Amour Habib kuwa wagombea ubunge katika majimbo ya Ushetu na Konde.

Katika kikao kilichofanyika leo Ijumaa Septemba 10, 2021 mkoani Dodoma kilichoongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Rais Samia Suluhu Hassan, Cherehani ameteuliwa kugombea ubunge Ushetu Mkoa wa Shinyanga.

Cherehani ameteuliwa kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa aliyefariki dunia Agosti 2, 2021 jijini Dar es Salaam.

Naye Habib ameteuliwa kugombea ubunge Konde, Mkoa wa Kaskazini Pemba baada ya aliyekuwa mbunge mteule wa jimbo hilo kujiuzulu.


Taarifa iliyotolewa leo na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi,  Shaka Hamdu Shaka imeeleza kuwa kamati hiyo imekaa kikao cha kawaida chini ya mwenyekiti wao na kujadili juu ya uchaguzi mdogo wa wabunge ambapo kampeni kwa upande wa mkoa wa Shinyanga zitaanza rasmi Septemba 25, 2021.


Aidha tarifa hiyo imeeleza kampeni katika jimbo la zitazinduliwa Septemba 24, 2021 huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Naibu katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar,  Abdalla Juma Sadala.

Imeandikwa na Salim Abubakary, Mwananchi