Polisi wamsaka aliyejiuzulu ubunge Konde

Polisi wamsaka aliyejiuzulu ubunge Konde

Muktasari:

  • Wakati aliyekuwa mbunge mteule wa jimbo la Konde, Sheha Mpemba Faki akieleza sababu nne zilizomfanya kujiuzulu nafasi hiyo, ikiwemo kupokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa watu anaodai ni wapinzani, Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba imesema haijapokea taarifa za vitisho hivyo na kumtaka akaripoti.

Dar/Zanzibar. Wakati aliyekuwa mbunge mteule wa jimbo la Konde, Sheha Mpemba Faki akieleza sababu nne zilizomfanya kujiuzulu nafasi hiyo, ikiwemo kupokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa watu anaodai ni wapinzani, Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba imesema haijapokea taarifa za vitisho hivyo na kumtaka akaripoti.

Siku chache zilizopita, mteule huyo alijiuzulu kabla hajaapishwa na Spika wa Bunge, ikiwa zimepita siku 14 tangu alipochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Julai 18 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Agosti 2 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, Faki aliandika barua ya kujiuzulu na alieleza uamuzi huo umetokana na changamoto za kifamilia.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Jumatano Agosti 4, 2021 kutoka Zanzibar, Mteule huyo alisema licha ya kuwa kujiuzulu kwake kumewavunja moyo watu wengi, lakini anaamini ataendelea kuishi kwa amani.

“Vitisho vya wahafidhina vya kunitoa uhai ni vingi na vinakuja kwangu moja kwa moja, ingawa nilikuwa siogopi kiasi cha kuvumilia lakini familia yangu na wazazi wamenishauri kuacha ubunge,” alieleza Faki ambaye kitaaluma ni mwalimu wa shule ya msingi Haruni.

Faki alieleza tangu kuteuliwa kwake amekuwa akifanyiwa ushirikina waziwazi, huku wengine wakimfuata mchana wakidai maisha yake yatakuwa mafupi kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake waliongoza jimbo hilo.

Alisema jambo jingine linalofanya ajiuzulu ni ubaguzi, kwakuwa yeye sio mzaliwa wa jimbo hilo bali alifahamika zaidi kutokana na utumishi wake serikalini uliomsaidia kupewa ridhaa na kupeperusha bendera kwenye uchaguzi mdogo.

“Napo pia wamekuwa wakinifuata kuniambia ilikuwaje na akashinda jimbo hili wakati sio mzawa wa eneo hili na hawataki kuniona na kwa kweli niliona nichukue uamuzi huu bila hata kukishirikisha viongozi wa chama changu,” alisema.

Faki alibainisha kwamba uamuzi wake CCM haujawafurahisha na amepewa barua inayomtaka kuandika sababu kimaandishi zilizomfanya kusaliti nafasi hiyo licha ya kuaminiwa na wanachama wake.

Alisema licha ya kupewa vitisho hivyo hakuripoti kwenye kituo chochote cha Polisi na kwamba wakati wapinzani wakimfanyia hivyo walionekana wazi kupitia vyombo vya habari.

Polisi wanena

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Kaimu Kamanda wa polisi wa Mkoa huo, Jerome Ngowi alisema taarifa za Faki kutishiwa maisha wameziona kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari na wanamtafuta ili awasaidie katika uchunguzi.

“Zipo taarifa kwenye mitandao alisema hata baadhi ya watu wamemfuata uso kwa uso anawafahamu, tukimpata itatusaidia kwenye uchunguzi,” alisema,

Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alisema hajapokea taarifa za Faki na kueleza kwamba kama alifanyiwa hivyo alipaswa kwenda kuripoti Polisi.

Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la vyama vya siasa nchini, John Shibuda alisema majibu yaliyotolewa na mteule huyo ni sawa na mti mkavu uliopinda, kwamba hakuna mwanasiasa yeyote anayeweza kukuambia suala hilo.

“Wanaoweza kutoa majibu sahihi ni CCM wenyewe kwa sababu baba mzazi anamjua mwanawe na mtu wa pembeni hawezi kujua, masuala yote ya Konde ni sawa na siri ya mtungi aijuaye kata, waulizwe,” alisema Shibuda.

ACT-Wazalendo

Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema hana taarifa za wanachama au viongozi wake kumtishia Faki na Jumapili watakuwa na kikao cha Kamati Kuu.

Katibu wa CCM Wilaya ya Micheweni, Hasan Khatib Hasan alisema Faki alitoa malalamiko yake baada ya kujiuzulu hivyo walishindwa kuchukua hatua za kisheria kwa watu wanaodaiwa kumpa vitisho hivyo.

“Tunakusanya taarifa za mwisho na tumemuambia aandike barua ya kujieleza” alisema.