Kujiuzulu mbunge wa Konde kwahusishwa na hoja ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa

Wednesday August 04 2021
mbungepic

Sheha Mpemba Faki

By Tuzo Mapunda
By Jesse Mikofu

Dar/Zanzibar. Siku moja baada ya mbunge mteule wa jimbo la Konde, Sheha Mpemba Faki kujiuzulu nafasi hiyo, suala hilo limewaibua wanasiasa wananasiasa wanaodai uamuzi unatokana na shinikizo la kisiasa kunusuru Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) visiwani Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Agosti 2 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, Faki aliandika barua ya kujiuzulu akieleza kufikia uamuzi huo kutokana na changamoto za kifamilia.

Faki alichaguliwa katika uchaguzi mdogo uliofanyika Julai 18 ambapo CCM ilishinda jimbo katika uchaguzi uliolalamikiwa na vyama vya upinzani.

Mteule huyo amejiuzulu kabla hajaapishwa zikiwa zimepita siku 14 tangu alipochaguliwa katika uchaguzi uliohusisha pia Chama kikuu cha upinzani visiwani humo, ACT Wazalendo ambacho kilipoteza jimbo hilo.

Soma zaidi:Mbunge mteule ajiuzulu, CCM yasikitika

Wakizungumza Dar es Salaam na Mwananchi jana kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Zanzibar Juma Duni Haji.

Advertisement

Walisema sababu zilizotolewa na mbunge mteule huyo ni propaganda tu na hazina ukweli wowote isipokuwa maamuzi hayo ni matokeo ya uporaji wa matokeo ya uchaguzi wa jimbo la Konde ambalo ni ngome ya upinzani.

“Na kwa namna nyingine kujiuzulu kwake ni jambo la heri, nawapongeza kwa sababu ingeleta shari na wangeendelea kushikilia jimbo hilo ambalo ukweli hawakushinda yangetokea maafa makubwa zaidi,” alisema Mbatia.

Mabatia alieleza kwamba walichokifanya ni kufungua koki kwa haraka kwa sababu baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi, kauli za viongozi wa juu wa CCM na ACT wa Zanzibar walionesha wazi SUK inaenda kuvunjika.

Soma zaidi hapa: NEC: Jimbo la Konde lipo wazi

“Wamefungua meza ya mazungumzo kufikia muafaka wa kitaifa, hivyo tunahitaji Katiba Mpya pamoja na tume huru ili kuthibiti masuala kama haya ambayo yanaonekana kuliingiza taifa katika hasara ya kurudia tena uchaguzi,” alisema Mbatia.

Juma Duni Haji alisema licha ya kuziona taarifa za kujiuzulu kwa mbunge huyo bado asingeweza kuzungumza chochote hadi Tume ya Taifa ya Uchaguzi itangaze kama jimbo lipo huru.

Alisema jana walitarajiwa kufanya kikao kufikia msimamo wa chama hicho.

“Kwa sasa hatuna cha kusema ngoja kwanza kamati kuu ikae kisha itatoka na maazio yake,” alisema Duni Haji

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Zanzibar imekiri kupokea barua ya kujiuzulu kwa mbunge mteule na kuwa taratibu zingine zitaelezwa baadaye.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi wa NEC visiwani humo, Hamidu Mwanga licha ya kutaka uvumilivu kwanza katika suala hilo, alisema Tume ilitarajiwa kutoa ufafanuzi jana kuhusu nini kinatakiwa kufanyika baada ya hatua hiyo.

“Tuvute subira kidogo mpaka kesho (leo). Tumepokea barua leo kwa hiyo tungevumilia kwanza kisha tume itakuwa imepata neno la kusema nini kinatakiwa kufanyika,” alisema Mwanga.

Alipoulizwa kuhusu gharama zilizotumika katika Uchaguzi uliopita, Mwanga alisema ni ngumu kufahamu kwa sababu uchaguzi huo ulihusishwa na baadhi ya kata ambazo zipo kwenye majimbo ya Tanzania Bara.

Akizungumzia suala la kujiuzulu kwa mteule huyo, Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Abdulla Juma Mabodi alisema chama kilimpa haki yake ya kugombea lakini hakiwezi kuingilia masuala ya kifamilia.

“Tuliingia kwenye uchaguzi, chama kilimpa haki yake ya kikatiba kugombea kwa hiyo ameandika barua ya kujiuzulu pia nayo ni haki yake, maana hakuna ajuaye masuala ya familia kuliko mhusika mwenyewe,” alisema Mabodi.


Mbunge mteule afunguka

Alipotafutwa na Mwananchi Faki alisema sababu kubwa ya kujiuzulu katika nafasi hiyo ni kutokana kupata vitisho vingi vya maisha kutoka kwa watu aliodai ni wapinzani wake, hivyo familia ikamshauri kuachana na suala hilo.

Alisema familia yake alikuwa nayo bega kwa bega tangu mchakato mzima wa kugombea katika jimbo hilo lakini baada ya vitisho hivyo, imeogopa.

“Nimeeleza wazi kwamba ni matatizo ya kifamilia, mimi mwenyewe nimetishiwa sana, natumia ujumbe, hata kwenye mitandao ya kijamii vitisho vilisambaa lakini mbaya zaidi kuna watu wamenifuata moja kwa moja. Baada ya kuona mambo haya yakiendelea, mama yangu mazazi ameogopa sana na ndiye ameweka shinikizo la mimi kuachia nafasi hii, baba huyo tulikuwa pamoja na msimamo wa kuendelea lakini imefika hatua nikaona ngoja tu niacha kwa sababu ya usalama wa wangu na familia yangu,” alisema.

Advertisement