Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chama cha Wabuddha chazipa msaada familia 250 Dar

Wakazi wa Chamazi wakikabidhiwa msaada wa mafuta, mchele unga na sukari kutoka kwa chama cha Wabuddha Tanzania.

Muktasari:

  • Familia zapata msaada, zaeleza kupata nafuu ya maisha kupitia Siku ya Uhisani ya Wabuddha Tanzania.

Dar es Salaam. Tabasamu imetawala kwa familia zenye uhitaji Dar es Salaam baada ya kupata nafuu ya maisha kupitia msaada wa mahitaji muhimu uliotolewa na Chama cha Wabuddha Wachina Tanzania.

Familia hizo 250 zimepokea mchele, unga wa mahindi, unga wa ngano, mafuta ya kupikia na sukari ikilenga kupunguza changamoto za maisha kwa familia hizo na kuwaletea matumaini mapya ikiwa ni ‘Siku ya Uhisani ya Wabuddha Tanzania: Baraka kwa Wote’, iliyofanyika katika Shule ya Kimataifa ya Bodhi, iliyopo Chamazi, Dar es Salaam.

Shughuli hiyo iliyoandaliwa na chama hicho kwa lengo la kuendeleza huduma za kijamii, kusaidia familia zenye uhitaji na kueneza maadili ya huruma, upendo na mshikamano katika jamii.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo jana Jumapili, Juni 28, 2026 mkazi wa Chamazi, Rahab Abdi alishukuru akisema ni msaada muhimu katika kipindi hiki kigumu alichonacho.

"Mie mgonjwa sina kazi, wazazi wala mume nahitaji zaidi huduma ya afya, pia niendelee kununua dawa," alisema.

Mkazi wa Chamazi Vigoa, Hija Omary alikiomba chama hicho kuwasaidia katika misaada mingine ikiwemo shule pamoja na kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu.

Kitogo Kitimbe kutoka Vigoa alisema msaada huo uzidi kuwa wa mara kwa mara kutokana na hali ya maisha aliyonayo.

Aidha, mbali na ugawaji wa misaada, shughuli hiyo ilijumuisha maonesho ya sanaa na utamaduni, hotuba za viongozi mbalimbali pamoja na maombi ya kuombea amani, maendeleo na ustawi wa jamii.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa chama hicho, Venerable Master Xianhong, alisema mafundisho ya Buddha yanahimiza huruma, shukurani na kushirikiana.

Alisema kusaidia wengine ni njia ya kujenga jamii yenye amani na maendeleo, na kwamba furaha ya kweli hupatikana pale watu wanaposhirikiana na kusaidiana.

"Tuzidi kuhimiza wananchi kuendeleza maadili ya wema, kuheshimiana na kusaidiana bila kujali tofauti za kabila, utamaduni au dini," alisema.

Kwa mujibu wa waandaaji, huu ni mwaka wa tisa mfululizo kwa jamii ya Wabuddha wa Kichina nchini Tanzania kushiriki katika shughuli za misaada ya kijamii.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wenyeviti wa Kata ya Chamazi, Jones Katunzi amekiomba chama hicho kuangalia namna ya kuzisaidia familia hizo huduma ya matibabu hasa kuwapatia bima za afya, kwa sababu katika kata hiyo kuna wazee zaidi ya 1,000 wanaohitaji bima ya afya.

Naye, Mwalimu Mkuu wa Shule ya LongQuan Bodhi, Jane Shao alisema   mbali na misaada hiyo pia kinajengwa kituo kitakachowafundisha vijana wa Kitanzania ujuzi na stadi za kazi mbalimbali, chenye uwezo wa kuchukua vijana 200 kitakachoanza kazi mwakani.