Chanzo cha mwenyekiti CCM Tabora kufariki akiwa ofisini

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi

Muktasari:

  • Wakasuvi alikuwa mwenyekiti wa CCM mkoa mwenye umri mkubwa

Tabora. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi amefariki dunia ghafla akiwa ofisini kwake mkoani humo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Februari 22,2024, kwa njia ya simu, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Tabora, Iddy Mambo amethibitisha kifo cha kiongozi huyo wa chama na kusema mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete mkoani humo.

Mambo amesema mwenyekiti huyo amefariki akiwa ofisini kwake wakati akisuburia ugeni wa Mwenyekiti wa Jumuiya Wazazi CCM Taifa, Fadhil Maganya, aliyetarajiwa kuanza ziara yake ya chama mkoani humo.

“Ni kweli kabisa Mzee wetu, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ametutoka, muda kama saa 8:30 mchana, ameamka leo akawa anadai kwamba hajisikii vizuri, lakini akaja ofisini kwa maana tulikuwa na shughuli ya kumpokea mwenyekiti wa wazee Taifa ambaye alikuwa na ziara ya siku nne katika mkoa wetu.

“Wakati tunasubiria pale basi akasema alikuwa ana changamoto anasikia jasho linamtoka kwa wingi na hajisikii, kwa hiyo akabaki ofisini kwa ajili ya kutusubiria. Sisi tulivyokwenda kumpokea mwenyekiti wa wazazi Taifa, nikapigiwa simu kwamba mzee wetu anaumwa kwa hiyo nilivyoenda kumchukua kwa ajili ya kumpeleka hospitalini tukiwa njiani bahati mbaya kumbe alikuwa ameaga dunia,” amesema Mambo.

Mwenezi huyo amesema Wakasuvi ambaye alikuwa mwenyekiti wa CCM mkoa mwenye umri mkubwa, atakumbukwa kwa uzalendo ndani ya chama, uwezo wa kusimamia na kutopenda uonevu jambo linalotajwa kumfanya adumu kwenye siasa za chama hicho.

“Nadhani ziara haitokuwepo kwa mujibu wa itifaki za chama chetu, kwa sababu watu wote tuko kwenye majonzi, tunaratibu shughuli za mazishi ya mpendwa na kiongozi wetu.  Alikuwa ni mtu mwema sana kwa sababu amekisaidia chama kwa muda mrefu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Louis Bura akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Buriani, amesema uongozi wa mkoa huo umeitisha kikao cha dharura na familia ili kupanga taratibu za mazishi yanayotarajiwa kufanyika nyumbani kwake eneo la Mabama wilayani Uyui mkoani humo.

“Niliposikia taarifa za kifo chake nilienda hospitalini kujiridhisha nikakuta ni kweli ni yeye amefariki na mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Kitete. Tutatoa taarifa za mazishi kadri tunavyojaaliwa,” amesema Bura.

Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora ya Kitete, Mark Waziri, amekiri kumpokea mwenyekiti huyo na kusema baada ya vipimo kufanyika ilibainika alikuwa ameshafariki kabla ya kufikishwa hospitalini hapo.

“Kutokana na historia yake inaonekana alikuwa na shinikizo la damu la kupanda ambalo ndilo linadhaniwa kusababisha kifo cha mwenyekiti huyo. Mwili wameuhifadhi vizuri ukisubiria maziko,” amesema Dk Waziri.

Mkazi wa Uyui mkoani humo, Hassan Ahmed ameeleza kusikitishwa na kifo cha kiongozi huyo, huku akidai alikuwa aliamini kuwa nguvu kazi ya taifa ni vijana hivyo chama hicho tawala kiwekeze nguvu kwa vijana ili kuwa na taifa imara.