Chato na ndoto ya kituo cha utalii iliyofifia-6

Simba akisafirishwa kwenye gari. Huyu ni mmoja wa wanyama waliotolewa katika mbuga mbalimbali za hifadhi na kupelekwa Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato. Picha na Maktaba.

Katika kufanya mapitio ya kitabu 'I am the State: A President's Whisper from Chato' kilichoandikwa na waandishi wanne nguli nchini ambao ni Absalom Kibanda, Ansbert Ngurumo, Neville Meena na Jesse Kwayu, tunamalizia na sura ya sita.

Leo tunamalizia mapitio ya sura ya sita na ya mwisho ya kitabu hicho inayoitwa ‘Fostering the tourist hub: A fading dream’.

Ingawa kuna mambo mengi yameandikwa katika sura hiyo, mapitio yake yatatazama baadhi tu ya mambo yaliyoguswa na kuyaacha yale mengine.

Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato, mwanzo, maendeleo na ufanisi wake ni mambo yaliyozungumzwa kwa kina katika sura hiyo. Usafiri kutoka Uwanja wa Ndege wa Chato au kutoka mahali pengine popote ili kwenda kutalii katika hifadhi hiyo, ni kitendawili.

Waandishi hawa wanasema kuwa kwa watalii wa ndani na hata wa nje, wanakumbana sana na shida ya kupata usafiri wa kuingia hifadhini.

Timu ya utafiti wa kitabu hicho, wakati wa utafiti wao, walikwenda Chato na kuamua kutembelea hifadhi hiyo. Lakini iliwachukua siku nane kupata usafiri wa uhakika wa kuwafikisha hifadhini.

Mbali na Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato, Rais Magufuli alianzisha Hifadhi ya Taifa ya Ibanda-Kyerwa yenye ukubwa wa kilomita za mraba 298.6; Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika iliyopo Karagwe yenye ukubwa wa kilomita za mraba 247 kuanzia mwaka 2019 iliyopo Kagera; Hifadhi ya Taifa ya Nyerere yenye ukubwa wa kilomita za mraba 30,893 iliyoko Ruvuma, Lindi, Pwani na Morogoro.

 Rais pia aliunda Hifadhi ya Taifa ya Kigosi yenye ukubwa wa kilomita za mraba 7,460 iliyopo Kigoma, Tabora na Geita pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla yenye ukubwa wa kilomita za mraba 3,865 kuanzia mwaka 2019 iliyopo Tabora.

Waandishi wa kitabu hicho wamebaini kuwa hifadhi zote mpya za kitaifa zilizoanzishwa, isipokuwa ile ya Nyerere, zilihifadhi majina asilia kutoka katika maeneo yao. Ilikuwa ni Chato pekee ambayo ilibanwa kwa Burigi.

Kitabu kimezungumzia pia Hoteli ya JS na kusema pengine ndiyo hoteli inayoongoza ya daraja la juu huko Chato, ambayo wanasema ni mali ya hayati Rais Magufuli, ambayo imeunganishwa na mbuga ya wanyama inayohifadhi wanyama walao majani.

Hoteli hiyo ilizinduliwa Desemba 25, 2017 wakati Rais Magufuli akiwa madarakani. Waandishi wanasema ingawa hakuna ubaya kwa kiongozi huyo kumiliki mali ya ukubwa huo, ni vyema ikafahamika kwamba yule ambaye mara kwa mara akijieleza kuwa ni maskini aliyetumwa na Mungu aliyejitolea kuwakomboa wanyonge, kwa hakika alikuwa na shughuli nyingi kujitengenezea utajiri.

Wamezungumzia pia kile wanachokiita Chato Zoo ambayo kimsingi inapakana na JS Hotel, iliyoanzishwa mwaka 2018. Inasemekana humo kuna aina 28 za wanyama kutoka mikoa 16 ya Tanzania. Pia, kuna aina 192 za ndege na aina 98 za miti. Zote hizi zinakaliwa katika eneo la hekta 1,235.6 za ardhi kama kilomita za mraba 12.356. Zoo imefungwa kwa ukuta kuzunguka eneo lote na imewekwa kamera za CCTV.

‘‘Hapa wanyama wote ni wa jamii ya wanyama wanaokula nyama, lakini kwa bahati mbaya, hali yao ni ya kutisha sana. Timu yetu iliona idadi ya mafuvu ya vichwa vya wanyama ambayo yanatuambia kwamba lazima wanyama wengi wamekufa,’’ wanasema waandishi.

Kitabu kinasema kulingana na mwongozaji mmoja katika mbuga ya wanyama, nyumbu wamekuwa na uhusiano wa uhasama wakati mwingine kupigana wao kwa wao hadi kufa, hususan kundi kubwa la madume.

Kwa ujumla, wanasema waandishi hao, wanyama wote hawana mvuto kwani afya zao zimedhoofu sana kiasi cha kuonyesha picha kuwa mbuga ya wanyama imetelekezwa au wanyama wameshindwa kuzoea mazingira mapya.

Wanasema miongoni mwa ndege wanaozurura kwa utukufu katika zoo ni tausi. Hawa walikuwa wakiishi katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.

Agosti 2019 Rais Magufuli alitoa tausi wanne kwa Rais Uhuru Kenyatta wa Jamhuri ya Kenya kama zawadi.

Mei 30, 2020 Rais Magufuli aliwaalika Ikulu mjini Dodoma marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na mjane wa Mwalimu Nyerere, Maria, katika hafla ambayo aliwapa kila mmoja wao tausi 25.

Kitabu hicho kinadai kuwa ilikuwa haijawahi kushuhudiwa hadharani, tausi kutoka Ikulu wakitolewa kama zawadi na Rais na kwa wingi kiasi hicho.

Ikulu iliripoti kwamba idadi ya tausi imeongezeka kutoka 403 mwaka 2015 hadi 2,260 ifikapo 2020 na kwamba kuwapa kama zawadi ni ishara ya kuwasambaza kote nchini haswa katika nyumba za serikali.

Wachambuzi wa mambo wanasema kwa vile tayari Magufuli alishapeleka tausi katika mbuga yake binafsi ya wanyama iliyopo Chato, hatua ya kuchangia watu wengine hasa marais ilikuwa ni njia ya kufifisha kashfa ya ubadhirifu wa rasilimali za Taifa.

Kwa ujumla, wazo zuri la kuwa na bustani ya wanyama kama hilo linaonekana kutofanikiwa kwani wanyama wanakufa kutokana na sababu zozote zile.

Kwa ujumla, waandishi wa kitabu hicho kilichozinduliwa Aprili 14 mwaka huu na Askofu wa Jimbo la Karagwe mkoani Kagera, Dk Benson Bagonza, wamejikita katika kuelezea mambo makubwa ambayo hayati Magufuli aliyafanya huko Chato, mahali alikozaliwa, ambayo hayakupaswa kufanywa huko.

Kwa maoni ya waandishi hao, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, Hospitali ya Rufaa ya Kanda, mbuga na hifadhi za wanyama, ni miongoni mwa vitu ambavyo havikuwa na umuhimu wowote kwa Chato bali vilipaswa kuwa angalau katika Mkoa wa Geita au Mwanza.

Waandishi wanabainisha kwamba ukandamizaji uliofanywa dhidi ya vyama vya upinzani, vyombo vya habari, jumuiya za kiraia, wasomi, na mawazo huru ulisababisha hofu ambayo nyuma yake kulikuwa na matendo mengi ya rushwa na ufisadi na kwamba sura mojawapo ya matendo ya kifisadi inashuhudiwa katika tabia na matendo ya wanyang'anyi yaliyojidhihirisha katika "miradi ya maendeleo" aliyoianzisha wilayani Chato, mahali alipozaliwa, ambayo inamtambulisha kuwa mtu wa kujikweza. Kitabu kinaonyesha namna fedha za umma zilivyotumika nje ya bajeti ya Serikali na kwamba, "Mambo yaliyotajwa katika kitabu hiki yalitendeka nchi ikiwa gizani na watu walinyamazishwa na haya yaliyoandikwa ni sehemu ndogo ya yaliyotendeka nchi ikiwa gizani."

Sura ya Sita ya kitabu hicho inamalizika kama ilivyoanza, ikielezewa kuwa kuilazimisha Chato iwe kitovu cha utalii itakuwa ni ndoto inayofifia.

Vyovyote vile, kuondoka kwa Dk Magufuli kwa njia ya kifo kumeifanya Chato isiwe kama ambavyo alikuwa ameikusudia iwe. Kwa maneno mengine, Chato haitakuwa tena kama ilivyokuwa inafikiriwa awali. Na, kulingana na kitabu hicho, miradi mingi imesimama kutokana na kifo cha Dk Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.