Hospitali ya Chato, eneo gumu wagonjwa kufika-4

Muktasari:

  • Sura ya nne ya kitabu 'I am the State: A President's Whisper from Chato' inawaelekeza wasomaji wake kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato, ikibainisha ilivyo vigumu kwa wagonjwa kuifikia.

Sura inaanza kwa kuweka historia fupi ya waliowahi kuwa marais wa Tanzania tangu uhuru na kinachowatofautisha na Dk John Magufuli, aliyekuwa rais wa tano.

Marais hao ni Julius Nyerere (1961-1985), Ali Hassan Mwinyi (1985-1995), Benjamin Mkapa (1995-2005) na Jakaya Kikwete (2005-2015).

Kitabu kinasema sifa kuu mbili zinamtenga Rais Magufuli na watangulizi wake, kwamba alikuwa rais aliyeongoza kwa muda mfupi zaidi (2015-2021) na aliyeonyesha waziwazi upendeleo, akilenga kujenga na kuboresha makazi yake alikozaliwa kwa njia ambayo haijawahi kuonekana hapo awali.

Siku zote akiwa amehangaishwa na miradi mikubwa na nia ya kuibadilisha Chato kutoka kitongoji hadi jiji la kisasa, katika kufanya hivyo, alipata wazo la kujenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa mjini Chato.

Mantiki ya kuanzishwa kwa mradi huu ilifafanuliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu katika hotuba yake kwa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Maendeleo ya Jamii Januari 2020.

Alisema hospitali ya rufaa ya Serikali Kanda ya Ziwa ilikusudiwa kuhudumia idadi ya watu inayozidi kuongezeka, inayokadiriwa kufikia milioni 15 katika Kanda ya Ziwa Victoria.

Waandishi wa kitabu hicho—Absalom Kibanda, Ansbert Ngurumo, Neville Meena na Jesse Kwayu—wanahoji kwa nini ijengwe hospitali ya rufaa huko Chato wakati Kanda ya Ziwa Victoria inajivunia kuwa na hospitali nyingine ya kisasa ya rufaa ya jijini Mwanza?

Katika kitabu hicho, waandishi hao wanasema Kanda ya Ziwa inajumuisha mikoa sita ya utawala; Kagera, Geita, Simiyu, Mwanza, Shinyanga na Mara ambapo ukiangalia umbali kutoka kila mkoa huoni sababu ya hospitali hiyo kujengwa Chato.

Wakipima umbali kwa gari kutoka kila mikoa hiyo, wamekuta kwamba Chato iko kilomita 221 kutoka Bukoba (Kagera), kilomita 171 kutoka Geita (mkoani), kilomita 319 kutoka Shinyanga, kilomita 357 kutoka Bariadi (Simiyu), kilomita 129 kutoka Mwanza na kilomita 259 kutoka Musoma (Mara).

Kwa umbali huo wameona pia Chato iliyoko pembezoni mwa Ziwa Victoria, iko karibu na Kagera kuliko hata makao makuu ya mkoa wake wa Geita.

Ndipo waandishi hao wakajiuliza, wagonjwa katika mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa wanapaswa kusafiri kilomita ngapi ili kupata huduma za matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Chato?

Hivyo, wakasema katika hali ya kawaida na kwa matumizi sahihi ya hekima ya uongozi, uanzishwaji wa hospitali ya Kanda ya Ziwa kijiografia ungewekwa Mkoa wa Mwanza, lakini, wanasema, hicho hakikuwa kipaumbele cha Magufuli.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akikagua baadhi ya vifaa vya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya  Chato.Picha na Maktaba

Kitabu kinabainisha kuwa kwa muda mrefu, Kanda ya Ziwa imekuwa ikihudumiwa na Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.

Bugando, iliyoteuliwa kuwa hospitali ya rufaa, ni ya Kanisa Katoliki, lakini ina utaratibu maalumu na Serikali kuhudumia sehemu ya mahitaji yake.

Utaratibu huo pia umewekwa na KCMC (Kilimanjaro Christian Medical Centre) mkoani Kilimanjaro, ambayo ni ya Wakfu wa Msamaria Mwema wa Kanisa la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Hii ina maana kwa viwango vyote, kama haki ingalikuwapo, hakuna namna ambayo Chato ingeishinda Mwanza kama mahali pazuri kwa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa.

Waandishi hao wanaandika kuwa kwa kuzingatia makadirio ya idadi ya watu kwa mujibu wa Ripoti ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, mtu anaweza kujiuliza ni kwa vipi Chato ilipata upendeleo kuliko Mwanza, Kagera na Mara, kutokana na wingi wa watu?

Pia, wanaandika waandishi hao, kwa kuzingatia miundombinu inayounganisha Kanda ya Ziwa, hakuna namna inayoweza kuipendelea Geita, achilia mbali Chato ambayo iko umbali wa takribani kilomita 120 kutoka makao makuu ya mkoa.

Katika marejeo yake, kitabu kinaandika kuwa taarifa zinaonyesha kuwa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Chato ulianza Septemba 18, 2017. Na wakati Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, alipokuwa katika ziara rasmi nchini Tanzania, alikutana na mwenyeji wake Rais Magufuli nyumbani kwake, Chato.

Miongoni mwa kazi nyingine zilizotangazwa, Rais huyo aliweka jiwe la msingi la Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato Januari 11, 2020.

Rais Nyusi alisafiri kwa ndege kutoka Msumbiji moja kwa moja hadi Chato, ambako shughuli zote za ziara ya kiserikali zilifanyika, ikiwa ni pamoja na mazungumzo rasmi na mwenyeji wake kuhusu masuala ya uhusiano kati ya nchi mbili na ushirikiano wa kijamii na kiuchumi.

Na wakati Rais Nyusi akiliweka jiwe hilo, Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima alisema hospitali hiyo itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa takribani milioni 14 kila mwaka na kwamba itahudumia wananchi kutoka Kagera, Kigoma, Tabora, Rukwa, Geita, Mwanza na Shinyanga.

Baada ya kuipitia hotuba ya Waziri wa Afya, waandishi wa kitabu walihitimisha kwamba “waziri huyo alitaka kuufurahisha umma.”

Waandishi hao waligundua kuwa Waziri Gwajima alisema ni watu takriban milioni 14, huku mtangulizi wake, Ummy Mwalimu, akitoa taarifa kwa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Maendeleo ya Jamii, akisema kuwa “uamuzi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato, ulitokana na idadi kubwa ya watu inayoongezeka eneo la Kanda ya Ziwa ambao ni takriban milioni 15.”

Waandishi hawa walipitia tovuti ya Wilaya ya Chato inayozungumzia uwezo wa hospitali hiyo kuwa itakuwa inahudumia wagonjwa kati ya 700 na 1,000 kwa siku. Hiyo inamaanisha wagonjwa 365,000 kwa mwaka kwa kiwango cha juu.

Hata hivyo, waandishi hao wanasema timu yao ya uchunguzi ilibaini kuwa kuanzia Jumatano hadi mwisho wa wiki, hospitali inaonekana kama kituo kilichofungwa.

Timu yao ilifanikiwa kuhesabu wastani wa wagonjwa 20 kwa siku wanaofika na kuondoka na vitanda vingi katika wodi vilikuwa tupu kuanzia Jumatano hadi Ijumaa.

Timu ya waandishi hao ilizungumza na muuguzi wa hospitali ambaye alisema "wagonjwa wengi wa Chato wanapendelea Hospitali ya Wilaya ya Chato. Ni chaguo lao. Wamezoea. Tena, wengine wanaweza kudhani kuwa hii ni ghali."

Kitabu hicho kinahitimisha sura yake ya nne kikisema “Licha ya kuwa hospitali ya rufaa inapaswa kushughulikia magonjwa makubwa tofauti na hospitali za wilaya na mikoa, katika Hospitali ya Rufaa ya Chato inaonekana bado haijaanza kutoa huduma hizo kwa wananchi. Jengo ni karibu tupu; ni baadhi tu ya wafanyakazi wanaoonekana karibu.”


Usikose kufuatilia kesho tukifanya mapitio ya sura ya tano inayoelezea “Chato ya Kushangaza: Alichokifanya Museveni; Alichokisema Mkapa”.