Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chemical, msanii msomi mshindi wa tafiti bora UDSM mwaka 2020/21

Chemical, msanii msomi mshindi wa tafiti bora UDSM mwaka 2020/21

Muktasari:

  • Mshindi wa kwanza wa tafiti bora Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) 2020/21 Claudia Lubao maarufu ‘Chemical’ amezungumzia namna alivyoweza kufikia mafanikio hayo.

Dar es Salaam. Mshindi wa kwanza wa tafiti bora Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) 2020/21 Claudia Lubao maarufu ‘Chemical’ amezungumzia namna alivyoweza kufikia mafanikio hayo.

Chemical ambaye amepata ufadhili wa kuendelea na masomo kwa hatua ya shahada ya uzamivu ‘PhD’ Chuo Kikuu cha St Andrew’s alichosoma mwana wa mfalme Prince William kilichopo Scotland, amesema amefanya vizuri licha ya kuwa na mambo mengi yanayomzunguka, ikiwamo shughuli za muziki.

Anasema amepata ufadhili huo baada ya kufanya vizuri katika shahada ya uzamili.

Chemical anayeimba muziki wa hiphop anasema wakati akisoma shahada yake ya kwanza UDSM, aliona ingekuwa vyema kusoma sanaa kwa kuwa ndicho kitu alichokipenda.

“Kozi niliyochukua ilikuwa na mambo mengi, ikiwamo uigizaji na mengine lakini nilichagua muziki. Wengi walioujua uwezo wangu wa kishule waliona kama nimepotea kwa kuwa nilikuwa nafanya vizuri huko nyuma, binafsi niliona napotea pia, lakini nilijipa moyo lazima nifanye kitu ninachokipenda ili nije kusaidia nchi yangu baadaye,” anasema wakati akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu.

Rapa huyo aliyehitimu shahada ya uzamili ya ‘Masters of Arts in Heritage Management’ anasema alivyomaliza shahada yake alirudi kufanya muziki kwa kutumia taaluma yake aliyoipata.

“Mbali na muziki, kuna miradi niliyokuwa naifanya kupitia mwalimu wangu aliyekuwa akitumia sanaa kutangaza tamaduni na muziki; na katika wasanii aliowachagua nilikuwemo,” anasema Chemical.

“Kuna siku akaniambia nimtumie vyeti vyangu, alipoviona akanipa moyo ‘mbona umefaulu vizuri kwa nini usiendelee na masters’, basi nikapata moyo wa kuendelea, hapo sasa nikasoma shahada ya Jamii na Usimamizi wa Turathi kwa maana ya urithi.”

Chemical anasema wakati wa masomo yake aliona wasomi wengi aliokuwa nao darasani walipendelea zaidi kufanya tafiti zao zinazoshikika, ikiwamo majengo, milima, hadithi, makaburi na vitu vingine.

Hata hivyo, anasema bado alikuwa na malengo ya kuendeleza sanaa ya muziki, hivyo utafiti wake akaamua kuufanya kupitia nyimbo za wavuvi.

“Kilichonisukuma kufanya utafiti huo ni kwa sababu wasomi wengi wanaangalia vitu vinavyoshikika, makaburi ya babu zetu, Kinjeketile, historia ya Mkwawa ni vitu ambavyo wamekuwa wakiviangalia wasomi wengi, lakini kuna kitu muhimu sana ambacho kipo kwa Waafrika na wamekuwa wakikithamini sana na hicho kitu ni muziki.

“Nilichokifanya nimeileta sanaa ya muziki kwenye urithi yaani usomi na ukitaka kujua hicho kitu ni muhimu sana kwa jamii ndiyo maana tafiti yangu imeonekana bora na imeshinda kwa kuwa ujumbe unafika kwa uharaka, licha ya kanuni bora nilizozitumia wakati wa utafiti wangu,” anasema.

Chemical anasema mbali ya hivyo, aliamua kusomea urithi katika kipengele cha sanaa ili kutangaza kile wanachokifanyia tafiti katika upande huo.

“Ukiangalia namna muziki unavyosambaa na vitabu, ni vitu viwili tofauti, mwalimu wangu kuna utafiti alifanya akaandika Kilwa akaupeleka ukachapishwa kwenye ‘journal’ alipeleka Unesco ambako hawakumjibu.

“Baadaye tukachukua ule utafiti kwa namna ileile ya kisomi tukaimba wimbo lakini unaoeleweka tukaupeleka tena Unesco ‘Kilwa Yetu’ upo pia YouTube. Unesco waliupenda wakatujibu na kutatupatia ufadhili tukatengeneza wimbo sasa wa Afrika ‘African Heritage’ unatumika sasa kimataifa na katika mikutano mikubwa,” anasema Chemical. Hata hivyo, anasema tatizo kubwa la tafiti nchini zimekuwa zikifanywa na kuwekwa kwenye vitabu na machapisho na haziwafikii walengwa.

“Tunafanya tafiti lakini majibu ya tafiti hayaifikii jamii husika kwa kuwa haizungumzi Kiingereza, haisomi. Mtu akishafanya tafiti inawekwa kwenye maandishi ya lugha za kigeni, vitabu au mitandaoni lakini ukitumia sanaa inawafikia kwa rahisi,” anasema.

Anatolea mfano wimbo wa Kilwa Yetu ambao kwa sasa unafahamika na jamii husika, lakini pia imesaidia kupeleka watalii katika maeneo ya Kilwa kupitia tafiti iliyofanywa na sanaa.

Hata hivyo, Chemical anasema urithi ni kitu kipana, lakini vijana wengi hawauhitaji na huona kama ni kitu ambacho kimepitwa na wakati, ingawa Wazungu wanatoka nje kuja kutafuta historia ambazo sisi hatutaki kuzisikia.

“Mtanzania lazima ujue ustaarabu wako ni muhimu. Muziki unatusaidia kuwavuta vijana ambao hawataki kuhadithiwa, kusoma basi angalau wasikie kupitia muziki,” anasema.


Muziki na shule

Chemical, aliyesoma Shule ya Msingi Coletha kabla ya kusoma sekondari ya kata iitwayo Twiga na baadaye kumalizia masomo yake ya kidato cha sita sekondari ya Nangwanda iliyopo Newala Mtwara, anasema amepitia katika vipindi vigumu kimaisha na sasa anaamini chochote kinawezekana.

Anasema ingawa wengi wanadhani amekuwa akitumia nguvu kubwa kusoma, lakini kwake haijawahi kuwa hivyo.

“Usomaji wangu kusema kweli nimesoma na watu ambao vipanga sana, sijawahi kuwa makini sana darasani ila nilipenda kufundisha wenzangu na ndipo ninaelewa zaidi, lakini kikubwa nilikuwa nachagua vya kusoma sisomi kila kitu.

“Nimesoma shule ambazo muda mwingi kulikuwa hakuna walimu, nilikuwa napenda kufundisha wenzangu. Lakini nikitaka kusoma nilihitaji muda wangu, najifungia nasoma bila mtu kuniona,” anasema Chemical.

Anasema kutokana na kazi yake ya muziki na masomo isingekuwa rahisi kufaulu, lakini aliamua kuchagua vitu anavyovipenda kuambatana navyo katika kipaji na masomo na alijitoa kwa vyote.

“Haikuwa rahisi, lakini kilichonisaidia mimi ni shauku, pamoja na changamoto zote nilipenda muziki na ninapenda taaluma, vyote nilivipa asilimia 100. Nikiwa kwenye masomo naacha muziki na nikitoka kwenye masomo nafanya muziki kwa moyo wote na hilo ndilo lililonisaidia,” anasema.

Alipoulizwa kuhusu mipango yake ya muziki, Chemical anasema hatarajii kuacha muziki na mashabiki wake watarajie mambo mengi kutoka kwake.

Chemical anasema anachokwenda kukifanya katika masomo yake ya uzamivu ni kutafiti kuhusu muziki wa Tanzania na Scotland, hivyo anaamini atakuja na suluhisho bora kwa muziki ndani ya nchi.

Ukiachana na muziki, Chemical anasema elimu ya Tanzania ina upungufu kwa kuwa wengi wanasoma vitu ambavyo hawavitumii mtaani.

Pia, anasema wengine hawasomi vitu wavyovipenda, hali inayochangia kudidimiza uchumi kwa namna moja au nyingine.

“Leo sanaa inaonekana ni uhuni, kwa sababu haijapewa kipaumbele, watoto wafundishwe vitu vitakavyowasaidia kwenye maisha, hata tukisema ajira ziongezwe si kila mtu atapata nafasi ya kuajiriwa, akienda kusoma ile miaka mitatu ajifunze elimu nyingine imsaidie kujiajiri.”

Akizungumzia malengo yake, Chemical anasema ni kuuleta muziki kwa wanataaluma ili wauheshimu na wasione wanaoimba ni wahuni.

“Kwa kupata tuzo pekee tayari niliwafanya watu waone muziki si uhuni, lakini wasomi wengi ukiwaambia kuhusu muziki wanaona wahuni wale, mwanafunzi anasoma anafanya muziki na bado nawahimiza wasanii wenzangu basi tuingie kwenye taaluma kidogo watuone wa maana na tuheshimike,” anasema.