Chiba kortini akidaiwa kusafirisha kilo mbili za Cocaine

Muktasari:
- Chiba anadaiwa kusafirisha kilo 2 za Cocaine, tukio analodaiwa kulitenda Juni 18, 2025 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere uliopo Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Raia wa Ubelgiji, Chiba Nkundabanyaka (45) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina cocaine zenye uzito wa kilo mbili.
Nkundabanyaka kutoka mji wa Roeselare nchini Ubelgiji, amefikishwa mahakamani hapo, leo Julai 4, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.
Mshtakiwa huyo alisomewa shtaka lake na wakili wa Serikali, Frank Rimoy mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.
Awali, kabla ya kusomewa shtaka hilo, hakimu Lyamuya alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.
Pili, shtaka la kusafirisha cocaine zenye uzito huo halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo ataendelea kubaki rumande.
Akimsomea hati ya mashtaka, wakili Rimoy alidai kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa lake, Juni 18, 2025 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere uliopo Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
Siku hiyo ya tukio, mshtakiwa anadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya cocaine zenye uzito wa kilo 2.042, kinyume cha sheria
Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka lake, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 17, 2025 itakapotajwa.
Mshtakiwa amerudishwa rumande kwa sababu kesi inayowakabili haina dhamana kwa mujibu wa sheria.