Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chuo cha Bahari kukabili uhaba wa madarasa ikijenga tawi Kimbiji

Mwenyekiti wa Wakurugenzi Shirika la Bandari Zanzibar, Joseph Abdallah akikabidhi zawadi kwa mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri chuo cha Bahari Tanzania ikiwa ni kuelekea mahafali ya Desemba 6, 2024

Muktasari:

  • Wakati ufanisi wa bandarini ukitajwa kuongezeka, Chuo cha Bandari kimedhamiria kupanua wigo wa uzalishaji wataalamu wenye sifa za kufikia masoko ya kimataifa kwa kujenga chuo kikubwa eneo la Kimbiji jijini hapa.

Dar es Salaam. Wakati ufanisi katika utendaji wa bandari nchini Tanzania ukiendelea kuimarika, Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kiko mbioni kutanua huduma zake ili kuongeza wigo wa uzalishaji wataalamu watakaokuwa na sifa za kuhudumu kimataifa ikiwemo soko la umoja wa Ulaya.

Chuo hicho tayari kinatarajia kujenga tawi kubwa katika eneo la Kimbiji Kigamboni ili kuboresha huduma wanazozitoa na kuongeza viwango vitakavyofanya wahitimu wake wakubalike katika masoko ya kimataifa.

Haya ameyasema jana Jumatano, Desemba 4, 2024 katika kongamano lililowakutanisha wadau mbalimbali wa bahari na wanafunzi waliosoma chuo hicho cha bandari katika majadiliano ya pamoja kwa ajili ya maendeleo ya chuo hicho.

Akizungumza Mkuu wa chuo hicho, Profesa Tumaini Gurumo amesema kupitia jitihada mbalimbali zilizofanyika sasa chuo chao kinashuhudia ukuaji wa idadi ya wanafunzi kutoka wanafunzi 1,500 miaka mitatu nyuma hadi wanafunzi 5,100 waliodahiliwa sasa.

Hali hiyo imefanya chuo chao sasa kukabiliwa na uhaba wa madarasa ofisi na vitendea kazi vingine jambo ambalo liliwafanya kuanza kuangalia namna ya kupanuka zaidi.

“Tulianza kuangalia namna ya kupanuka zaidi kwa kutafuta eneo Kimbiji ambako tunatarajia kujenga chuo cha bahari ambacho kitaendana na sifa ya kimataifa ya chuo chetu sambamba na maono tulionayo,” amesema Profesa Gurumo.

Amesema kujengwa kwa chuo hicho sasa itakuwa ni mwanzo wa mabaharia wa Tanzania kuingia katika meli za Umoja wa Ulaya tofauti na ilivyo sasa.

“Tunataka kufikia viwango ambavyo havina ukomo ili vijana waweze kupata ajira sehemu mbalimbali ili wakuze uchumi wa nchi. Pia tumepanua wigo kwa kwenda Lindi na Mwanza na tunatafuta eneo visiwani Pemba ili tuweze kusogeza mafunzo visiwani Zanzibar,” amesema.

Amesema kukua kwa idadi ya wanafunzi ni ishara kuwa elimu ya masuala ya bahari inazidi kuwapa fursa vijana za kuchagua nini wanataka ili kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi.

Hilo litakwenda sambamba na kujibu kiu ya upatikanaji wa rasilimali watu wenye weledi ili kujenga wataalamu wa ndani ya nchi badala ya kusubiri wanaokuja wawekezaji kuja na wataalamu wao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wakurugenzi Shirika la Bandari Zanzibar, Joseph Abdallah amesema elimu inayopatikana chuoni hapo haisaidii eneo la usafiri wa majini bali pia sekta nyingine ambazo zinategemea eneo hilo.

“Bahari husafirisha mizigo mikubwa kuliko eneo lolote hivyo wataalamu wanaofanya shughuli huko wanapaswa kuwa na elimu ya kutosha na wanabeba jukumu kubwa kwa sababu endapo uzembe ukitokea na meli kuzama ni hasara kubwa kwani mali nyingi hupotea kuliko hata gari lingeanguka,” amesema Abdallah.