CRDB yatoa msaada kwa familia iliyopata watoto watano Muhimbili
Muktasari:
- Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Delilah Kimambo, amesema akaunti zilizofunguliwa zitasaidia kuratibu misaada kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali zinazotaka kuisaidia familia hiyo.
Dar es Salaam. Benki ya CRDB imewafungulia akaunti watoto watano waliozaliwa kwa wakati mmoja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), huku kila mmoja akiwekewa Sh1.5 milioni, ikiwa ni sehemu ya msaada kwa familia ya Simon Benjamin Mkwizu na mkewe Victoria waliobarikiwa kupata watoto hao.
Msaada huo umetolewa siku sita baada ya Victoria kujifungua watoto hao katika hospitali hiyo, ambapo pia benki hiyo imewafungulia akaunti wazazi wao, kumpatia mama mtaji wa biashara na kumkabidhi baba bajaji mpya kwa ajili ya kuimarisha kipato cha familia.
Akikabidhi msaada huo leo Juni 19, 2025, Ofisa Uendeshaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile, aliwapongeza madaktari, wauguzi na wataalamu wa afya wa Muhimbili kwa kazi kubwa waliyoifanya kuhakikisha mama na watoto hao wanakuwa salama.
“Huduma iliyotolewa na Hospitali yetu ya Taifa Muhimbili inaonyesha kiwango cha juu cha taaluma, kujitolea na uzalendo wa wataalamu wetu katika kutunza na kuokoa maisha ya mama na mtoto. Tunawashukuru kwa mchango wao mkubwa katika kuhakikisha familia hii inapata faraja na matumaini mapya,” amesema Mwile.
Amesema benki hiyo imeona umuhimu wa kuisaidia familia hiyo kutokana na ongezeko la majukumu lililosababishwa na kuzaliwa kwa watoto watano kwa wakati mmoja.
Kupitia kitengo chake cha Youth Banking, CRDB imewafungulia watoto hao akaunti za Junior Jumbo na kuweka Sh1.5 milioni kwa kila mmoja, huku kitengo cha udalali wa hisa (Brokerage) kikinunua hisa zenye thamani ya Sh500,000 kwa kila mtoto.
Mbali na watoto hao, mama yao amefunguliwa akaunti ya Malkia na kuwekewa Sh2.5 milioni, ambapo Sh1.5 milioni zimewekwa kwenye akaunti huku Sh1 milioni zikitarajiwa kumkabidhiwa kwa ajili ya kukuza biashara yake.
Kwa upande wa baba wa familia hiyo, ambaye ni ofisa usafirishaji (dereva bajaji), amefunguliwa akaunti ya Imbeju inayolenga kuwawezesha wajasiriamali, pamoja na kukabidhiwa bajaji mpya iliyokatwa bima kamili ili kumsaidia kuongeza kipato na kukidhi mahitaji ya familia yake iliyoongezeka ghafla.
Aidha, benki hiyo imewakatia bima ya afya ya kiwango cha juu mama na watoto wote watano, huku baba huyo akitarajiwa kunufaika na mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha kupitia programu ya Imbeju inayotekelezwa chini ya CRDB Bank Foundation.
Mwile amesema benki hiyo inaamini maendeleo ya Taifa huanzia kwa mtoto, ndiyo maana imeendelea kuwekeza katika huduma za kifedha zinazowalenga watoto, vijana na makundi mengine ya wananchi.
“Tunawahamasisha wazazi kufungua akaunti kwa watoto wao, kuweka akiba na kujenga utamaduni wa kujitegemea tangu wakiwa wadogo,” amesema.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mkwizu ameishukuru Muhimbili kwa huduma wanazoendelea kuwapatia watoto wake tangu walipozaliwa wakiwa na uzito mdogo.
Amesema watoto hao wanaendelea vizuri katika chumba cha uangalizi maalumu cha watoto wachanga huku afya zao ikiimarika siku hadi siku.
“Kwa upande wa Benki ya CRDB nasema mmefanya jambo kubwa sana, mlichokifanya ni sawa na kumpatia maji mtu mwenye kiu jangwani. Mimi na familia yangu tunawashukuru sana na tupo tayari kuwa mabalozi wenu,” amesema Mkwizu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Delilah Kimambo, amesema akaunti zilizofunguliwa zitasaidia kuratibu misaada kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali zinazotaka kuisaidia familia hiyo.
“Wapo wengi wanaotaka kusaidia familia hii, akaunti za watoto zitasaidia wale wanaotaka kutoa msaada wa muda mrefu, huku akaunti ya mama ikirahisisha upatikanaji wa fedha za matumizi ya kila siku,”amesema Dk Kimambo.
Amesema watoto hao wamefikisha siku sita tangu kuzaliwa kwao na wanaendelea kuonyesha maendeleo mazuri kiafya, huku baadhi ya vifaa maalumu vya matibabu walivyokuwa wakivitumia vikiondolewa kutokana na kuimarika kwa hali zao.
Alhamisi ya Juni 18, 2026 gazeti hili liliandika kuhusu gharama za kuwalea watoto hao na lilimnukuu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Daniel Nkungu akisema familia hiyo inahitaji msaada.
Dk Nkungu alisema familia hiyo inahitaji msaada mkubwa wa kifedha na kisaikolojia ili kukabiliana na changamoto za kulea watoto watano waliozaliwa kabla ya wakati.
"Mama anahitaji ushauri nasaha na uangalizi wa karibu. Mwili wake umepitia mabadiliko makubwa wakati wa ujauzito na sasa anakabiliwa na jukumu la kuwalea watoto watano huku akiendelea kupona mwenyewe," alisema.
Alisema mama huyo anahitaji mwongozo kuhusu lishe bora, muda wa kupumzika na msaada wa kihisia, mambo ambayo yanahitaji rasilimali za kifedha pamoja na upendo kutoka kwa jamii.
"Ni wajibu wetu sote pamoja na Serikali kuisaidia familia hii ili iweze kukabiliana na changamoto za kulea baraka hii waliyopewa," alisema.
Akizungumzia hilo la gharama, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi wa MNH, Dk Living Colma amesema kwa wastani mtoto mmoja atahitaji makopo matano ya maziwa ya watoto kwa mwezi, kwa kuwa maziwa ya mama pekee huenda yasitoshe.
Ili kutosheleza mahitaji ya maziwa kwa watoto wote watano kwa mwezi, amesema familia italazimika kununua makopo 25, ambayo wastani wa bei ya kila kopo ni Sh30, 000 hivyo jumla zitatumika Sh750, 000.
Sambamba na hayo, Dk Colman amesema watoto hao wanaweza kuhitaji nepi takribani 300 kila mmoja kwa mwezi, sawa na nepi 1,500 kwa wote watano. Gharama ya nepi pekee inaweza kuzidi Sh500, 000 kwa mwezi.
Aidha, gharama za mavazi, makazi na kupata watu wa kusaidia malezi zinatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na mahitaji ya kuwahudumia watoto hao.
Pia, baba wa watoto hao, Simon Mkwizu alisema uzazi huo ni furaha, lakini ni changamoto kwa familia kwa upande mwingine, akisisitiza atahitaji msaada kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki.
"Tunashukuru Mungu kwa baraka hii, lakini kulea watoto watano kwa wakati mmoja kunahitaji msaada kutoka kwa ndugu, jamaa na watu wenye mapenzi mema," alisema.
Alisema yeye ni dereva wa bajaji huku mkewe akiwa mama wa nyumbani na kwa hali yao ya kiuchumi hawatamudu gharama zote za kulea watoto hao peke yao.