Prime
Safari ya uzazi wa watoto wengi na nafasi ya Tanzania
Dar es Salaam. Furaha, mshangao na matumaini vilitawala katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Juni 13, 2026, wakati Victoria Mkwizu, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, alipojifungua watoto watano kwa njia ya kawaida.
Ni tukio ambalo si tu limeandika historia mpya kwa familia hiyo, bali pia limeiweka Tanzania kwenye ramani ya matukio adimu ya uzazi duniani.
Mama huyo amejifungua watoto wote hao kwa njia ya kawaida.
Akinukuliwa na gazeti hili toleo la leo (Juni 18, 2026), Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Muhimbili, Dk Rachel Mhaville amesema kuzaliwa kwa watoto hao ni tukio la nadra na kipekee lililohitaji usimamizi wa karibu kutoka kwa timu ya wataalamu wa fani mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa mama na watoto.
Katika ulimwengu wa tiba, ujauzito wa watoto watano kwa wakati mmoja huhesabiwa kuwa miongoni mwa ujauzito wenye hatari kubwa zaidi.
Kila hatua, kuanzia ufuatiliaji wa ujauzito hadi kujifungua na malezi ya awali ya watoto wachanga, huhitaji umakini mkubwa wa wataalamu wa afya.
Ndiyo maana mafanikio ya Muhimbili ya kuhakikisha mama na watoto wote watano wanazaliwa salama yamepokewa kama ushahidi wa maendeleo ya huduma za afya nchini na uwezo wa wataalamu wa Kitanzania kukabiliana na changamoto kubwa za kitabibu.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, mimba za watoto wengi huongeza hatari ya kujifungua kabla ya wakati, watoto kuzaliwa na uzito mdogo, matatizo ya mfumo wa upumuaji pamoja na changamoto nyingine zinazoweza kuhatarisha maisha ya mama na watoto.
Hata hivyo, changamoto kama hizo zimewakuta watoto hao wa Victoria Mkwizu kama anavyonukuliwa na gazeti hili jana, mkuu wa wadi ya watoto wachanga wa Muhimbili, Dk Martha Mkony kuwa watoto hao walizaliwa wakiwa na uzito wa kati ya gramu 800 na kilo 1.7.
Dk Mkonu amesema kutokana na watoto hao kuzaliwa kabla ya kukomaa kwa ujauzito, kulihitajika uangalizi maalumu, hasa ukizingatia mmoja wao alipata changamoto ya kupumua.
“Akapewa dawa ya kukomaza mapafu Jumapili (Juni 14) na kuanzia hapo wamekuwa wakiendelea vizuri na wanaangaliwa kwa karibu na wauguzi na madaktari na hali zao za afya na mama yao zinaridhisha na wanaweza kutumia maziwa ya mama,” amesema.
Matukio duniani
Katika baadhi ya matukio duniani, changamoto hizo zimewahi kusababisha vifo vya watoto au mama wakati wa kujifungua.
Hali hiyo ndiyo inayofanya tukio la Muhimbili kuwa la kipekee. Mafanikio hayo yamewezekana kutokana na maandalizi ya kina yaliyohusisha madaktari bingwa wa uzazi na magonjwa ya wanawake, madaktari wa watoto wachanga, wauguzi pamoja na vitengo maalumu vya kuhudumia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.
Kwa kiwango hicho, Muhimbili imejiunga na kundi la hospitali chache duniani zilizofanikiwa kusimamia salama uzazi wa watoto watano kwa wakati mmoja huku mama na watoto wote wakibaki salama katika hatua za awali baada ya kujifungua.
Akizungumzia hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Muhimbili, Dk Rachel Mhaville amesema kuzaliwa kwa watoto hao ni tukio la nadra na kipekee lililohitaji usimamizi wa karibu kutoka kwa timu ya wataalamu wa fani mbalimbali, ili kuhakikisha usalama wa mama na watoto.
Baba wa watoto hao, Simon Mkwizu amesema mara ya kwanza waligundua kuwa Victoria alikuwa na ujauzito wa watoto wanne alipofikisha miezi mitatu ya ujauzito baada ya kuhudhuria kliniki katika Kituo cha Afya Malecela, Tabata.
"Baadaye tulipelekwa Hospitali ya Amana kwa ufuatiliaji zaidi kabla ya kuhamishiwa Muhimbili," amesema.
Kwa upande wake, Victoria amesema alilazwa Muhimbili Mei 13 baada ya kuhamishwa kutoka Hospitali ya Amana na tangu wakati huo alikuwa chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari na wauguzi.
Rekodi ya dunia inashikiliwa na Mali
Wakati Tanzania ikisherehekea kuzaliwa kwa watoto watano, rekodi rasmi ya dunia bado inashikiliwa na Halima Cisse wa Mali.
Mei 4, 2021, Halima aliwashangaza wengi baada ya kujifungua watoto tisa kwa wakati mmoja katika kliniki ya Ain Borja mjini Casablanca nchini Morocco.
Watoto hao, wasichana watano na wavulana wanne, waliingia katika Kitabu cha Rekodi za Guinness kama kundi la kwanza la watoto tisa kuwahi kuzaliwa na wote kuendelea kuishi.
Marekani na kisa cha “Octomom”
Kabla ya rekodi ya Halima Cisse, dunia ilivutiwa na simulizi ya Nadya Denise Doud-Suleman wa Marekani, maarufu kama “Octomom”.
Mwaka 2009, Nadya alijifungua watoto wanane kwa wakati mmoja katika Jimbo la California.
Watoto wote walinusurika na kuendelea kuishi, jambo lililomfanya kuwa mama wa kwanza katika historia ya kisasa kujifungua watoto wanane na wote wakaendelea kuishi.
Australia rekodi Iliyoambatana na maumivu
Historia pia inaonesha kuwa mwaka 1971, Geraldine Brodrick wa Australia alijifungua watoto tisa katika Hospitali ya Royal Hospital for Women mjini Sydney.
Tofauti na ilivyo leo, teknolojia na huduma za afya za wakati huo hazikuwa zimefikia kiwango cha sasa. Watoto wote walifariki dunia ndani ya siku sita baada ya kuzaliwa, jambo lililoacha simulizi ya huzuni katika historia ya uzazi wa watoto wengi duniani.
Watoto watano walioitikisa dunia
Miongoni mwa matukio maarufu zaidi ya kuzaliwa kwa watoto watano ni lile la Dionne Quintuplets nchini Canada mwaka 1934.
Wasichana hao watano walikuwa kundi la kwanza la watoto watano katika historia ya kisasa linalojulikana kuishi baada ya kuzaliwa.
Umaarufu wao ulivuka mipaka ya Canada na kuvutia mamilioni ya watu duniani, kiasi cha kugeuka alama ya kihistoria katika masuala ya uzazi wa watoto wengi.