CUF Zanzibar wamfungulia kesi Profesa Lipumba
Muktasari:
- Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, Mussa Haji Kombo kwa kushirikiana na wanachama wengine waliofukuzwa chama hicho, wamefungua kesi ya kumshtaki Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, Mussa Haji Kombo kwa kushirikiana na wanachama wengine waliofukuzwa chama hicho, wamefungua kesi ya kumshtaki Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Kesi hiyo namba 633/2021 imefunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania na inatarajiwa kutajwa kwa mara ya kwanza Machi 14, 2022 chini ya Jaji Ephery Kisanya.
Hata hivyo, akizungumza kwa simu na Mwananchi leo Januari 22, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya amesema hana taarifa na kesi hiyo, lakini akasema “Kama wanamshitaki Profesa Lipumba, inaonesha wenyewe katiba ya chama pia hawaijui, kwasababu yeye ni mwenyekiti wa kikao tu na sio anayetoa maamuzi.”
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi jijini Dar es Salaam, Kombo ametaja sababu mbalimbali za kumfungulia kesi Profesa Lipumba ikiwemo kufanya vitendo vya uvunjaji wa katiba.
Amesema chama hicho kwa kipindi cha takribani miaka miwili kimekuwa na mambo yanayoendelea ambayo hayaleti taswira nzuri yenye kujenga taasisi zaidi ya kuidhoofisha.
“Kwa mambo hayo yanayoendelea yamenifanya mimi Mussa Haji Kombo ambaye ni muasisi wa chama cha CUF kumfungulia kesi Mwenyekiti wangu Profesa Ibrahim Lipumba.
“Sababu zilizonisukuma kufungua kesi dhidi yake ni kufanya vitendo vya uvunjaji wa katiba kwa kufanya au kusimamia kinyume na katiba ya CUF,” ameongeza.
Aliyataja maamuzi hayo ambayo aliyasimamia na kuyafanya katika kipindi cha hivi karibuni kuwa ni kuleta pendekezo la kumfukuza Abbas Juma Muhunzi kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti, kushinikiza aliyekuwa Mkurugenzi wa habari kujiuzulu nafasi hiyo na kutokuhusisha viongozi wake wa karibu katika matumizi ya malimbikizo fedha za ruzuku sh1.05 bilioni.
“Lingine ni kubadilisha Katiba ya chama kinyume na mapendekezo yaliyopitishwa na mkutano mkuu wa 2019 na mwenyekiti kukiongoza chama kama vile anaongoza familia yake na kuamua anachotaka yeye,” amesema.
Naye aliyekuwa Mjumbe Kamati ya Utendaji Wilaya Kinondoni (ambayo ilivunjwa), Juma Mahimbo amesema hawawezi kukaa kimya pale ambapo wanaona haki haitendeki katika Chama.
“Nimefukuzwa, sikubaliani na uamuzi huo na ndo maana nimeungana na hawa wenzangu kuweza kufungua kesi,” amesema Mahimbo.