Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CWT Morogoro Vijijini yapata mrithi, Mniko akiibuka kidedea

Baadhi ya wajumbe wa kamati kuu ya utendaji chama cha walimu Tanzania Wilaya ya Morogoro Vijijini wakifuatilia jambo wakati wa uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi ya Mwenyekiti wa chama cha walimu Tanzania baada ya kifo aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Mbaruku Chipete. Picha na Juma Mtanda

Muktasari:

  • Wagombea wawili wa uenyekiti wa CWT Morogoro Vijijini wajiondoa dakika za mwisho kabla ya kura kupigwa, huku Sabato Mniko akiibuka mshindi.

Morogoro. Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Morogoro Vijijini kimepata mwenyekiti mpya baada ya mwalimu wa Shule ya Msingi Newland, Kata ya Mikese, Sabato Mniko, kushinda uchaguzi mdogo kwa kupata kura saba kati ya kura 12 zilizopigwa.

Uchaguzi huo umefanyika kwa lengo la kujaza nafasi iliyoachwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Mbaruku Chipete, aliyefariki dunia Januari 22, 2026, kwa ajali ya barabarani iliyohusisha gari na pikipiki katika eneo la Shamba la Mkonge Pangawe, kando ya barabara ya Morogoro–Dar es Salaam.

Awali, wagombea saba walipitishwa kuwania nafasi hiyo, lakini wawili kati yao, Huruma Mashambo na Keneth Myowela, walijiondoa muda mfupi kabla ya upigaji kura, na kufanya idadi ya wagombea kubaki watano.


Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi huo jana, Aprili 22, 2026, msimamizi wa uchaguzi, Jumanne Nyakirang’ani, amesema uchaguzi ulifanyika kwa utulivu na kwa kuzingatia taratibu zote.

Amesema Mniko alipata kura saba, akifuatiwa na Sharifa Nnileka aliyepata kura tano kutoka kwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Utendaji ya CWT Wilaya ya Morogoro Vijijini.

Kwa mujibu wa Nyakirang’ani, wagombea wengine watatu, ambao ni Camilius Timoth, Said Makenga na Shabani Yamlinga, hawakupata kura hata moja, hali inayoashiria kuwa ushindani mkubwa ulikuwa kati ya wagombea wawili.

“Uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, na ushindani mkubwa ulikuwa kati ya Mniko na Sharifa, ambao wameonesha kuaminiwa zaidi na wajumbe,” amesema Nyakirang’ani.

Baada ya kutangazwa mshindi, Mniko ameahidi kutetea maslahi ya walimu kwa kuzingatia katiba ya CWT na kuhakikisha haki zao zinatekelezwa kwa wakati.

Ametaja baadhi ya changamoto zinazowakabili walimu kuwa ni ucheleweshwaji wa malipo ya stahiki mbalimbali, ikiwemo nauli za likizo, malimbikizo ya mishahara pamoja na gharama za matibabu.


“Walimu wanapaswa kulipwa haki zao kwa wakati ili kuongeza morali ya kazi na kurejesha imani kwa chama chao,” amesema Mniko.

Kwa upande wake, Nyakirang’ani amemtaka mwenyekiti huyo mpya kuongoza kwa vitendo na kuepuka malalamiko yasiyo na tija, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda heshima ya chama hicho.

Ameongeza kuwa mwenyekiti wa CWT wilaya anao wajibu wa kuwa msemaji mkuu, mtetezi wa walimu na kiongozi wa vikao vyote vya chama katika ngazi ya wilaya.

Naye msimamizi msaidizi wa uchaguzi, John Kigongo, amesema mchakato mzima ulifuata ratiba rasmi, na uchukuaji wa fomu ulianza Machi 4 hadi Aprili 2, 2026.

Jumla ya watu tisa walijitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo, mmoja akijiondoa na mwingine kuondolewa kutokana na kutokidhi vigezo.

Katika nafasi ya mwakilishi wa walimu wa sekondari, Simon Machele alishinda kwa kupata kura nane dhidi ya kura nne za mpinzani wake, Emily Kilimali.