Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kibaha yajipanga kukabiliana na ongezeko la wanafunzi 2028

Matukio mbalimbali uzinduzi Wa jengo la vyumba vitatu shule ya Sekondari Picha ndege Manispaa ya Kibaha. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani imeanza utekelezaji wa miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu kukabiliana na ongezeko la wanafunzi litakalotokana na mabadiliko ya mfumo wa elimu mwaka 2027, huku vyumba 33 vya madarasa vikiwa tayari vimekamilika na mipango ya kuongeza vingine ikiendelea.

Kibaha. Manispaa ya Mji wa Kibaha mkoa wa Pwani imeanza maandalizi ya kuboresha miundombinu ya elimu kufuatia mabadiliko ya mfumo wa elimu utakaoanza mwaka 2027, hatua inayotarajiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wa sekondari mwaka 2028.

Akisoma taarifa leo Aprili 21, 2026 kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, Wazo Mwang’onda, Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Kibaha, Theresia Charles amesema ongezeko hilo litasababisha upungufu wa vyumba vya madarasa 174, matundu ya vyoo 518 na madawati 9,155.

Amesema halmashauri imeanza kuchukua hatua kwa kujenga vyumba 33 vya madarasa kwa gharama ya Sh726 milioni ambavyo tayari vimekamilika, huku mpango ukiwa ni kujenga vyumba vingine 120, matundu ya vyoo 259 na kutengeneza madawati 4,578 kwa gharama inayozidi Sh3 bilioni.

“Tunajiandaa mapema kuhakikisha mabadiliko ya mfumo wa elimu hayailetei Manispaa changamoto ya uhaba wa miundombinu, bali yanakuwa fursa ya kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wetu,” amesema Theresia.


Taarifa hiyo iliwasilishwa mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Sekondari Picha ya Ndege, mradi uliogharimu Sh66 milioni.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwang’onda amesema serikali imelenga kuboresha elimu nchini kwa kuimarisha miundombinu, kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuongeza ubora wa ujifunzaji.

Matukio mbalimbali uzinduzi Wa jengo la vyumba vitatu shule ya Sekondari Picha ndege Manispaa ya Kibaha. Picha na Sanjito Msafiri

“Miradi hii inapaswa kutekelezwa kwa wakati ili kuendana na mahitaji yanayokuja na kuhakikisha wanafunzi watakaoanza kidato cha kwanza mwaka 2028 wanapata mazingira bora ya kujifunzia,” amesema Mwang’onda.

Akizungumzia hatua hiyo, mdau wa elimu, Rehema Mathayo amepongeza juhudi za Manispaa ya Kibaha katika kuanza mapema maandalizi ya kukabiliana na ongezeko la wanafunzi, akisema ni hatua muhimu ya kuimarisha ubora wa elimu.

“Maandalizi haya yanaonesha utayari wa kukabiliana na changamoto kabla hazijatokea. Uwekezaji katika madarasa, vyoo na madawati ni msingi wa mazingira bora ya kujifunzia na unaunga mkono dhamira ya serikali ya kuboresha elimu nchini,” amesema Rehema.