CWT yasisitiza ujenzi nyumba za walimu
Muktasari:
- CWT imeiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kuwajengea nyumba walimu ili nao wafurahie kuitumikia taaluma yao.
Rombo. Rais wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT), Leah Ulaya ameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa nyumba za walimu nchini, ili kupunguza madhila ambayo wamekuwa wakikumbana nayo pindi wanaporipoti kwenye maeneo mapya ya kazi.
Ulaya ameyasema hayo leo Machi 23,2024 wakati wa kongamano la walimu wanawake wa chama cha walimu (CWT) wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro ambapo limewajumuisha washiriki 400, lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu na kupata maarifa mbalimbali ikiwemo elimu ya malezi.
Amesema, anatamani kuona Serikali ikielekeza nguvu kubwa kwenye ujenzi wa nyumba hizo za walimu kwa kuwa wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu, hasa wanapokuwa wameripoti kwenye vituo vyao vipya vya kazi.
"Tunatamani kuona nyumba za walimu zikijengwa kama ambavyo mama yetu Samia Suluhu Hassan amekwishaelekeza, ili kupunguza ule ukata na madhila ambayo walimu wenzetu na sisi wenyewe tunayapata tunapokwenda kuripoti makazini."
"Tunaomba Serikali ielekeze nguvu kubwa kuona ni namna gani mwalimu wa Kitanzania anafurahia kutumikia taaluma yake aliyoisomea, kundi hili ndio pekee lenye uwezo wa kuandaa nchi ya leo, kesho na baadaye, tupo tayari kufanya kazi usiku na mchana kwa wakati wote kwa kushirikiana na Serikali ili kumuunga mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan."
Amesema, "tunatamani kama tunaweza kurudi mezani tukazungumza tuone namna nzuri ya kutekeleza ule mfumo wa mwalimu kujisajili na kuendelea kutoa taarifa zake mara kwa mara, kwa kuwa sio walimu wote wapo kwenye maeneo sahihi ambayo mtandao unapatikana kwa urahisi."
Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali imeongeza uwekezaji mkubwa kwenye programu ya kuboresha kada ya ualimu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu.
"Rais amefanya kazi kubwa katika sekta ya elimu, ukiangalia tangu mwaka 1961 ujenzi wa miundombinu ya elimu hapa nchini haijawahi kutokea kipindi ambacho kumekuwa na ongezeko kubwa la uwekezaji kwenye elimu, kuanzia awali hadi vyuo vikuu,"amesema Profesa Mkenda.