Dar waongeza polisi 300 kudhibiti panya road

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla amesema mkoa huo umeongeza askari 300 kwa ajili ya msako wa kuwakamata wahalifu maarufu 'panya road'.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla amesema mkoa huo umeongeza askari 300 kwa ajili ya msako wa kuwakamata wahalifu maarufu 'panya road'.

Makalla ameyasema hayo leo Alhamisi Septemba 15, 2022 alipokuwa akizugumza na wananchi wa Kata ya Zingiziwa mara baada ya kutembelea ujenzi wa barabara ya Chanika -Homboza.

Amesema msako wa wahalifu huo umeanza tangu jana Alhamisi na kuwaambia wazazi ambao watapotelewa na vijana wao kuanzia leo Alhamisi wakawafuate vituo vya polisi au hospitali za wilaya.

"Hawa panya road wamezaliwa na wazazi, ni watoto wetu, na kwa kuwa baadhi mmeshidwa kuongea nao sisi tutashughulika nao na tayari tumemwaga askari 300,” amesema

"Hivyo kuanzia leo naomba mzazi au mlezi ambaye hatamuona kijana wake afike vituo vya pilisi na hospitali kubwa za wilaya ikiwemo Amana Mwananyamala, Muhimbili wodi ya Mwaisela na Temeke," amesema Mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi na usalama

Hata hivyo, Makalla amesema inasikitisha ķatika matukio mawili yaliyotokea siku mbili hizo katika maeneo ya Kawe na Tabata, waliokamatwa kuhusika wengi na vijana waliotoka kutumikia vifungo vya miezi sita hadi mwaka mmoja jela.

Katika hili amesema ana imani vyombo vya sheria vitatenda haki katika kutoa adhabu kwa wale ambao makosa yao ni ya kujirudia.