Dar wataka magari ya taka yawe kama ambulance

Mojawapo ya magari yanayobeba takataka na kwenda kutupa dampo.

Muktasari:

Ni kilio cha makandarasi wa uzoaji taka jijini humo wanaotaka magari hayo yasibughudhiwe barabarani.

Dar es Salam.Makandarasi wanaozoa taka katika Jiji la Dar es Salaam, wametaka magari yanayozoa taka yasibughudhiwe barabarani kama ilivyo kwa magari ya kubeba wagonjwa 'ambulance'.

Ombi hilo limetolewa leo Jumatatu, Januari 15, 2024 na Mwenyekiti wa makandarasi wa kuzoa taka jijini humo, Methew Andrew alipokuwa akitoa wasilisho lao kwenye mkutano mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert  Chalamila na watendaji wa Serikali kuhusu tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko.

Andrew amesema moja ya changamoto wanazokutana katika uzoaji taka,  ni pamoja na kusimamishwa mara kwa mara na askari wa usalama barabarani.

"Tunaomba magari haya yaangaliwe kama ambulance, yasibughudhiwe kwa kuwa kazi  inayofanywa ni ya kutoa huduma ya afya kwa wananchi," amesema mwenyekiti huyo.

Ukiachilia mbali usumbufu wa askari wa barabarani, Andrew amesema miundombinu ya kuingia katika dampo la Pugu Kinyamwezi sio rafiki, hivyo kushauri njia mbadala ya kuingia katika dampo hilo.

Ameeleza wakati wakiwa kwenye foleni ya kusubiri kumwaga taka kutokana na ubovu wa miundombinu, mtaani taka zinazidi kuongezeka hivyo hushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

"Kunapotokea tatizo la taka kutozolewa kwa wakati,  tunaonyooshewa vidole ni sisi makandarasi. Wanaanchi hawajui kuna ubovu wa miundombinu ya barabara au nini wanachotaka ni taka ziondolewe," amesema Andrew.

Akielezea hali ya uzalishaji na uzoaji taka ulivyo kwa jiji hilo, Andrew amesema tani 4,000 hadi 5,000 huzalishwa, huku uzoaji ukiwa ni wastani wa asilimia 40 hadi 47.

Pia wameomba kupewa mikataba mirefu ya kufanya kazi ili iwe rahisi kwao kukopesheka na benki  na hivyo  kununua magari mengi zaidi kuliko ilivyo sasa.

Baadhi ya wakazi wa jiji hilo, wakizungumzia hali ya taka, walisema sio nzuri. Nemensi Kiria, amesema licha ya kulipa tozo za taka, zinaweza kuchukua hadi mwezi bila ya kuzolewa.

Zaina Ibadi, mkazi wa Buguruni, amesema kuna haja ya kuwekwa kwa madampo ya muda katika mitaa, ili inapotokea taka zimejaa majumbani, watu wajue wapi pa kwenda kuzitupa.