Dk Mpango akerwa na gari za taka, mifuko ya plastiki
Dodoma. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema zipo kampuni za kuzoa takataka zinazoshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo, kwa sababu ya uwezo mdogo.
Hayo aliyasema jana katika Soko la Kisasa la Machinga lililopo jijini Dodoma, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani.
Makamu huyo wa Rais, alisema ifike wakati sasa, mamlaka za Serikali za Mitaa zitoe zabuni kwa kampuni zinazojishughulisha na kazi ya kuzoa taka zenye uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.
“Kwa mfano, unakuta kampuni iliyopewa zabuni ya kuzoa taka, magari wanayotumia nayo takataka. Unakuta gari liko wazi taka zinatoa harufu kali inayosababisha kero kwa wananchi. Ninavyosema hivi, watumiaji wa Barabara ya Pugu kule Dar es Salaam nadhani wananielewa vizuri, alisema Dk Mpango.
Aliongeza: “Lakini pia mnapaswa kuweka miundombinu ya uhakika ya kuzoa taka katika mitaa na maeneo ya mikusanyiko ikiwemo katika masoko, stendi na hospitali.’’
Atoa agizo mifuko ya plastiki
Wakati huo huo, Dk Mpango aliiagiza Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), kuongeza nguvu katika kuchukua hatua za kisheria kwa watengenezaji na watumiaji wa mifuko ya plastiki iliyorejea kwa kasi.
Alisema halmashauri, ziandae utaratibu wa kusimamia sheria ndogo walizojitungia.
“Natoa maelekezo kwa NEMC na mamlaka za serikali za mitaa nchini kote kusimamia na kuongeza nguvu zaidi katika utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki, hakikisheni mnachukua hatua za kisheria kwa wale wanaokiuka maagizo haya,”alisema.
Alisema kampeni ya kusitisha matumizi ya mifuko ya plastiki ya mwaka 2019, ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa lakini inasikitisha matumizi ya mifuko hiyo yameanza kurudi tena.
Alisema inakadiriwa kila mwaka dunia inatumia mfuko bilioni 500 ya plastiki, huku asilimia 10 ya takataka zinazozalishwa zikitokana na plastiki.
Alisema sehemu kubwa ya taka hizo zinaishia kwenye maziwa, mito, bahari, jambo alilosema lisipodhibitiwa litawafanya wavuvi katika miaka ijayo kuvua plastiki badala samaki.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maji na Mazingira, Jackson Kiswaga alishauri Serikali kuanza kutoa zawadi kwa kushindanisha watu mbalimbali katika utunzaji wa mazingira nchini ili kuongeza hamasa kwenye eneo hilo.
“Inasemekana hadi kufikia 2030 tuitakuwa na wakimbizi milioni 140 ambao wanahamahama barani Afrika kwa hiyo tuna wajibu mkubwa wa kutunza mazingira,”alisema Kiswaga.
Makamu Mwenyekiti wa Machinga mkoani hapa, Christian Msumari alishauri Serikali kuunda kamati ndogo itakayowashirikisha wao na wadau, lengo likiwa ni kushughulikia migogoro na upangaji wa machinga.