Wadau: Kaza 'kamba' vifungashio plastiki, elimu itolewe mashuleni
Muktasari:
- Katika kuadhimisha siku hiyo, ambapo Manispaa ya Moshi imeshirikiana na Chama cha ushirika wa akiba na mikopo cha ELCT ND Saccos, kufanya usafi, kupanda miti na kutoa elimu ya athari za plastiki kimazingira na kiafya, wadau wameona bado nguvu zinahitajika katika udhibiti wa vifungashio vya plastiki.
Moshi. Serikali imetakiwa kuweka nguvu kudhibiti uzalishaji na uingizaji wa vifungashio vya plastiki, kama njia kuzuia uchafuzi wa mazingira nchini, sambamba na kutoa elimu hiyo kuanzia shule za msingi ili kujenga uelewa mpana juu ya suala hilo.
Rai hiyo imetolewa leo Juni 5,2023 na wadau wa mazingira wakati wa ufanyaji usafi katika Stendi Kuu ya Mabasi mjini Moshi, na upandaji wa miti ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani yenye kauli mbiu ‘Pinga uchafunzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki.’
Katika kuadhimisha siku hiyo, Manispaa ya Moshi imeshirikiana na Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha ELCT ND. Ambapo kwa pamoja walifanya usafi, kupanda miti na kutoa elimu ya athari za plastiki kimazingira na kiafya.
Akizungumzana Mwananchi Digital, Makamu Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Kilimanjaro, Hassan Rajabu amesema: “Ili kuweza kudhibiti mifuko na vifungashio vya plastiki, Serikali inapaswa kuweka nguvu ya udhibiti viwandani au mipakani kwa ile inayotokea nje ya nchi, kwa kuwa maeneo hayo ndiyo chanzo cha usambazaji.”
Habibu Lema ambaye ni Makamu Mwenyekiti Jumuiya ya Watumia Maji Mto Rau, amesema: “Plastiki ni adui mkubwa wa vyanzo vya maji na kwamba ipo haja kwa serikali kuendelea kutoa elimu na kuongeza nguvu ya udhibiti ili kuhakikisha inatokomea kabisa.”
Kwa upande wa Agness Bilago Mwanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Uhuru iliyopo mjini hapa, anaona iko haja kwa Serikali kutoa elimu ya mazingira na madhara ya plastiki kuanzia shule za msingi, ili kujenga kizazi chenye uelewa kitakachokuwa mstari wa mbele kukemea na kuzuia uchafuzi wa mazingira.
"Taka za plastiki zina madhara makubwa sana kwenye mazingira na hata kiafya, Serikali iweke mkazo kwenye masomo ya Mazingira ili kuwajenga watoto kujua umuhimu wa kutunza mazingira, lakini pia itolewe elimu ya urejelezaji wa chupa za plastiki kwa matumizi ya baadae, ili mtu anaponunua maji au bidhaa nyingine, atambue pa kuiweka na si kuitupa mtaani,” ameshauri.
Hata hivyo, Mkuu wa Divisheni ya Maliasili na uhifadhi Mazingira Manispaa ya Moshi, Uhuru Mwembe amesema katika masoko bado kuna vifungashio vya plastiki vinavyoingia kutoka nchi jirani na kwamba wanaendelea na jitihada za kutoa elimu na kuidhibiti.
"Manispaa ya Moshi hatuna viwanda vingi vinavyozalisha taka za plastiki lakini kuna mifuko midogomidogo ya plastiki ambayo inaingia kutoka nchi za jirani lakini tunapambana nayo, na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi watumie vifungashio na vibebeo ambavyo vimethibitishwa na TBS na baraza la mazingira".
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa ELCT ND Saccos, Monica Mlay amesema wamepanda miti zaidi ya 200 katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Moshi, lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira.
"Leo siku ya mazingira tumepanda miti zaidi ya 200 ikiwemo ile ya vivuli na matunda katika manispaa ya Moshi, nitoe wito kwa wananchi kupanda miti katika maeneo mbalimbali ikiwemo majumbani na hata maeneo ya wazi, ili kuweza kulinda na kuhifadhi mazingira ambayo kwa sasa yameonekana kuharibiwa," amesema Mlay.