Sh586 milioni yawezesha watoto 120 kielimu

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kali (wa pili kulia) akikabidhi begi la shule kwa mmoja wa wanafunzi wanaonufaika na ufadhili wa elimu wakati wa hafla ya kuadhimisha Siku ya Familia Duniani iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

Katika kundi hilo, watoto 23 wamefaulu mitihani ya darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza huku wengine watatu wakifauli mitihani ya kidato cha nne na kuchaguliwa kuendelea na kidato cha tano na sita.

Kigoma. Penye nia pana njia! Huo ndio usemi unaofaa kutumika baada ya watoto 26 kutoka mazingira magumu mitaani na familia duni waliopata ufadhili wa masomo kufaulu na kufanikiwa kuendelea na elimu ya sekondari katika hatua tofauti.

Katika kundi hilo, watoto 23 wamefaulu mitihani ya darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza huku wengine watatu wakifauli mitihani ya kidato cha nne na kuchaguliwa kuendelea na kidato cha tano na sita.

Mafanikio ya watoto hao 26, ambao ni kati ya watoto 120 wanaopata ufadhili, ni matokeo ya Shirika la Maendeleo ya Vijana (Kividea) Mkoa wa Kigoma kuwekeza zaidi ya Sh586 milioni katika ufadhili wa masomo kwa watoto wanaotoka familia duni na wanaoishi mazingira hatarishi mitaani.

Akizungumza mjini Kigoma leo Mei 15, 2023 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Kividea, Babu Steven amesema mradi huo unafadhiliwa na Shirika la terre des hommes schweiz (tdhs).

Amesema wanufaika katika mradi huo unaohusisha wavulana 60 na wasichana 60 ni watoto kutoka Kata za Uvinza, Ilagala, Kazuramimba na Nguruka Halmshauri ya Uvinza na Kigoma Ujiji.

‘’Pamoja na mahitaji ya kielimu, mradi huu pia unahusisha huduma za afya kwa watoto kukatiwa Bima ya Afya, kuhamasisha na kuwashauri wazazi na walezi kuchangia mahitaji mengine muhimu ikiwemo chakula na malazi,’’ amesema Babu

Mmoja wa watoto wanaonufaika kupitia mradi huo mwenye umri wa miaka 13 (jina linahifadhiwa) amesema ufadhili huo umemrejeshea ari na matumaini ya kufikia ndoto yake kieliumu kimaisha yaliyofifia baada ya wazazi wake kuingia kwenye mgogoro uliosababisha watengane.

"Kitendo cha wazazi wangu kutengana siyo tu ilitishia kukatisha ndoto yangu kielimu, bali pia iliniingiza kwenye maisha magumu kwa kuanza kuzunguka mitaani kutafuta vibarua vyenye malipo duni kwa lengo la kupata fedha za kujihudumia mahitaji muhimu,” amesema mtoto huyo

Amesema akiwa mitaani ambako wakati mwingine alilazimika kuomba msaada kutoka kwa watu wenye mapenzi mema, ndipo alipokutana na wafanyakazi wa shirika la Kividea ambao walimshawishi kurejea shuleni kwa ahadi ya kumsaidia mahitaji muhimu.

‘’Namshukuru Mungu sasa naendelea na masomo na ninafanya bidii siyo tu kufaulu, bali pia kufikio mafanikio na malengo yangu kielimu na kimaisha ili baadaye niisaidie familia yangu,’’ amesema mtoto huyo

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kali aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye katika maadhimisho hayo amewataka wazazi na walezi kote nchini kutimiza wajibu wao wa kutunza, kulea na kuwahudumia watoto kuanzia ngazi ya familia hadi jamii.

"Watoto wanaoishi katika mazingira magumu mitaani ni matokeo ya vitendo vya familia na jamii kushindwa kutimiza wajibu wa malezi na makuzi. Baadhi yao hujikuta wakifanyiwa vitendo vya ukatili. Ni vema kila mzazi na mlezi kutimiza wajibu katika malezi ya watoto,’’ amesema Kali

Amewataka wazazi na walezi kujenga tabia ya kuzungumza kwa uwazi na watoto wao kuhusu mambo hatarishi katika ustawi na makuzi yao.

‘’Wazazi tufuatilie mienendo ya watoto wao kuanzia nyumbani, mitaani hadi shuleni kufahamu aina ya marafiki, watu wanaowazunguka au kuambatana nao, maeneo wanayotembelea ili kubaini vitendo wanavyofanya au kufanyiwa na kuingilia kati kabla mambo hayajaharibia,’’ ameshauri Mkuu huyo wa wilaya

Mbagazi Mussa, mkazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ameiomba Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma kuanzia ngazi ya familia na jamii kama njia ya kukabiliana na kutokomeza vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia.

‘’Binafsi elimu kuhusu vita dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia niliyoipata kupitia maadhimisho ya leo imenifungua macho katika ulinzi, malezi na makuzi ya watoto. Elimu ya aina hii inatakiwa kuwa endelevu na ishuke hadi ngazi ya familia ambako ndiko vitendo vingi hutokea,’’ amesema Mbagazi