Vijana wapewa ‘mchongo’ kwenye uhifadhi wa mazingira

Ofisa Mazingira Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Fanuel Kasenene akifafanua jambo wakati wa kongamano maalum la kuadhimisha siku ya mazingira lililofanyika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) Mwanza. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

Wilaya ya Nyamagana imejiwekea lengo la kupanda miti zaidi ya milioni 1.5 kila mwaka ikiwa ni moja ya mikakati ya kuhifadhi na kulinda mazingira.

Mwanza. Vijana nchini wametakiwa kuchangamkia fursa za kujiajiri kupitie eneo la uhifadhi wa mazingira badala ya kukaa mitaani huku wakilalamika kukosa ajira.

Wakizungumza wakati wa kongamano maalum la kuadhimisha siku mazingira duniani lililofanyika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (Saut) jijini Mwanza Juni 5, 2023, wadau wa mazingira wametaja upandaji wa miti ya mbao na maua ya kibiashara na urejeshaji wa taka ngumu kwa kutengeneza bidhaa kuwa miongoni mwa fursa za ajira zilizopo kwenye eneo la uhifadhi wa mazingira.

Wakizungumza kwenye wamesema vijana wanatakiwa kufikiria na kuja bunifu mbalimbali zenye lengo za kubadilisha taka kuwa bidhaa ili kuleta tija kwa jamii kwa ujumla.

Akifafanua, Ofisa Mazingira Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Fanuel Kasenene ametaja eneo lingine lenye fursa kuwa ni vikundi vya kukusanya na kuondoa takataka mitaani.

‘’Kwa siku, vikundi vya vijana vinaweza kuingiza Sh80, 000 kwa kukusanya tani moja ya takataka mitaani na kuifkisha dampo. Hili ni eneo ambalo vijana wanatakiwa kuja na mawazo ya ubunifu kuhusu namna gani watasaidia kupunguza takataka mitaani,’’ amesema Kasenene.

Meneja Miradi kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Usimamizi wa Mzingira na Maendeleo (EMEDO), Arthur Mgema amezishauri taasisi za elimu nchini kuanzisha vitengo maalum vya elimu kwa umma namna ya kudhibiti na kuondoa takataka mitaani.

“Suala la uhifadhi na usafi wa mazingira liwe ni miongoni mwa masomo muhimu katika hatua zote za elimu kuanzia shule za msingi hadi elimu ya juu,’’ amesema Mgema.

Ofisa Tawala Wilaya ya Nyamagana, Magreth John amesema pamoja na elimu kwa umma kuhusu uhifadhi wa mazingira, Serikali pia inatekeleza kampeni ya kupanda miti ya mbao, matunda na mauaji katika maeneo yote ya umma huku lengo likiwa ni kupanda zaidi ya miti milioni 23 ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo.

‘’Wilaya ya Nyamagana tumejiwekea lengo la kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka,’’ amesema Magreth

Amesema kila mtu kuanzia ngazi ya kaya, taasisi binafsi na za umma watahimizwa kupanda na kutunza miti katika maeneo yao.