Daraja la Sangatini laanza kujengwa

Muktasari:
- Tanroads waanza ujenzi wa daraja la Sangatini linalounganisha wilaya za Kigamboni na Mkutanga eneo la Pemba Mnazi.
Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa amesema Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), imeanza ujenzi wa daraja la Sangatini lenye thamani Sh 2.9 bilioni inalounganisha wilaya hiyo na Mkuranga mkoani Pwani.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo leo Januari 7, Fatma Nyangasa imeeleza ujenzi huo utachukua miezi 12 hadi kukamilika kwa mujibu wa mkataba na mkandarasi Ngenda Constructions Ltd atakayetekeleza mradi huo.
Katika taarifa hiyo, ilieleza kuwa Nyangasa alibainisha hayo alipotembelea eneo la mradi na kusema kuanza kwa ujenzi wa daraja hilo ni hatua kubwa katika kuboresha miundombinu inayosaidia kuunganisha wilaya hizo mbili.
"Rais Samia Suluhu Hassan anatupatia fedha zaidi kwenye kuboresha miundombinu, kukamilika kwa daraja hili kutasaidia wananchi kwa shughuli za kiuchumi na upatikanaji wa huduma za kijamii."
"Wakazi wengi wa upande wa Mkuranga wanapata huduma za kijamii wilayani hapa Pemba Mnazi, hadi sasa maandalizi ya eneo la kazi, vifaa, barabara za mwingiliano na ujenzi wa nguzo msingi vimefanyika," amesema Nyangasa.
Kwa mujibu wa Nyangasa, ujenzi wa daraja hilo umeanza Oktoba 3 mwaka 2021 na mkandarasi anatakiwa kuukabidhi ifikapo Oktoba 2 mwaka huu.
Naye Mkuu wa Idara ya Mipango wa Tanroads, Elisony Mweladzi amesema matarajio mradi huo kukamilika kabla ya muda wa mkataba iwapo hakutakuwa na changamoto ya mvua kubwa kunyesha