Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dawasa yapita nyumba kwa nyumba kukagua upatikanaji maji

Muktasari:

  • Baadhi ya maeneo ambayo huduma ya maji haijarejea ikiwamo Mburahati, Kigogo, Tabata, Temeke, Kiwalani Dawasa imebainisha yatapata maji usiku wa leo.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Majisafi na Usafi Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), leo Alhamisi Julai 3, 2025 imefanya ziara ya nyumba kwa nyumba katika baadhi ya mitaa jijini humo ikilenga kukagua hali ya upatikanaji wa huduma ya maji ambayo ilikosekana kwa saa 12 kupisha matengenezo kwenye mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini Julai Mosi, 2025.

Matengenezo hayo yalisababisha ukosefu wa maji katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam na mkoa wa Pwani.

Dawasa ilitangaza ukosefu wa huduma ya maji kwa saa nane, hata hivyo, matengenezo yalikamilika kwa saa 10 na huduma hiyo kurejea tangu jana usiku kwenye baadhi ya maeneo.

Hata hivyo, maeneo mengine yameripotiwa kuendelea kutopata maji, changamoto ambayo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Dawasa, Everlasting Lyaro amesema hadi usiku wa leo Julai 3, 2025 huduma itakuwa imerejea katika maeneo yote.

Amesema maeneo mengi huduma ya maji imerejea, huku machache ikiwamo ya Mburahati, Kigogo, Tabata, Temeke, Kiwalani na maeneo mengine machache ndiyo hayajapata huduma hiyo.

"Timu yetu ya ufundi ipo site (kazini) kuhakikisha huduna inarejea kwenye maeneo yote," amesema Lyaro.

Akizungumzia ziara ya nyumba kwa nyumba katika mitaa mbalimbali ya Dar es Salaam, Lyaro amesema Dawasa imeweka utaratibu wa kutembelea mtaani na kuona hali ya huduma, hasa baada ya kukamilika kwa matengezo yaliyosababisha kukosekana kwa huduma ya maji Julai Mosi.

"Julai Mosi, tulitangaza kukosekana kwa huduma kwa saa nane kutokana na matengenezo ambayo wenzetu wa Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) walikuwa wakiyafanya.

"Mitambo iliyoathirika katika matengenezo hayo ni wa Ruvu Juu na Ruvu Chini ambayo inalisha asilimia 91 ya wakazi wa Dar es Salaam,” amesema.

Amesema baada ya kukamilika kwa matengenezo yaliyofanyika kwa saa 10, Dawasa iliwasha mitambo ya maji baada ya saa 12 na maeneo mengi kuanza kupata maji, isipokuwa machache ambayo hadi jioni ya leo kwa mujibu wa Lyaro, nayo yatakuwa yamepata huduma hiyo.

"Niwahakikishie wananchi wa Dar es Salaan na Pwani leo (Julai 3) maeneo yote huduma itakuwa imerudi katika hali ya kawaida," amesema.


Walichokisema wananchi

Katika ziara hiyo ya Dawasa iliyofanyika katika maeneo ya Mwananyamala na Msasani ikilenga kujiridhisha kama wananchi wanapata huduma ya maji na kusikiliza kero zao, wananchi wengi walikiri kupata maji kwa siku mbili mfululizo, huku wakiomba huduma hiyo iwe endelevu.

Mkakata Abdul ambaye ni mjumbe wa kamati ya mtaaa wa Kambangwa aliyemwakilisha mwenyekiti wa mtaa huo, Rehema Mwakyusa amesema baada ya matengenezo ambayo walitangaziwa na Dawasa maji yamerejea tangu jana.

"Hadi sasa (leo Julai 3, saa 10 jioni) hayajakatika isipokuwa yanatoka machafu si meupe, lakini huduma ipo, si kama kipindi cha nyuma tulikuwa tunakaa hadi siku nne bila maji, tunachokiomba hii iwe endelevu tusirudi tulipotoka," amesema.

Akifafanua kuhusu maji kutoka machafu, Lyaro amesema Dawasa inatibu maji kwa viwango, kamwe haiwezi kupeleka maji machafu kwa wananchi.

"Kinachotokea, mfano Julai Mosi, hakukuwa na maji kwa zaidi ya saa 12 kwenye Bomba, hivyo kuna vitu viwili, cha kwanza ni upepo ambao tunatakiwa kuutoa ili kuondoa ile hali ya mwananchi anapofungua koki kusikia mlio wa hewa na si maji.

"Pili ni bomba lilikuwa kavu muda mrefu kwa hiyo katika muda huo limepitisha vitu vingi, hivyo tunaposukuma maji kwa wananchi huenda laini yake iliingiliwa au ni chafu, hizi zinakuwa ni kesi moja moja, hata hivyo anayekutana na changamoto hii anatakiwa airipoti Dawasa tukasafishe laini yake," amesema.

Mkazi mwingine wa Mwananyamala, Afia Ibrahim amesema hali ya upatikanaji maji kwa sasa inaridhisha tofauti na huko nyuma.

"Huko nyuma ilikuwa tunakaa siku nne hadi tano bila maji na yakitoka basi yanatoka machafu, lakini kwa siku mbili hizi, jana na leo tunashukuru yanatoka," amesema.

Mkazi wa Msasani, Ahmed Khalfan amesema eneo hilo hakuna huduma ya kuuziwa maji kwenye ndoo, hivyo inapotokea hayatoki basi uombe msaada jirani aliyehifadhi maji akusaidie au uagize ya madumu ambayo moja huuzwa Sh 2000.

"Hatukuwa na maji kwa siku kadhaa, jana walipita mafundi wa Dawasa mtaani na kutueleza wamekuja kukagua huduma ya maji, tuliwaeleza changamoto yetu, wameturekebishia na tangu usiku wa jana (Julai 2) hadi leo maji yanatoka," amesema.

Mkazi mwingine wa eneo hili, Latifah Ahmed Masoud amesema awali walikuwa wakikosa huduma ya maji kwa siku tano kwa wiki, lakini sasa yanatoka na kutamani huduma hiyo iwe endelevu.