DC Lijualikali aagiza Lema kukamatwa

Muktasari:

  • Lema amesema hakuna kauli ya kuua japokuwa ipo ile ya kutaka wanaume wamuoe ili aache kuwasumbua wananchi kwenye eneo hilo.

Dodoma. Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Peter Lijualikali ameagiza Jeshi la Polisi kumsaka popote alipo na kumkamata Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, ili ahojiwe kwa alichoeleza “kutoa kauli za uchochezi” kwenye mkutano wa hadhara Oktoba 24, 2023.

 Katika video ambayo inasambaa kwenye mitandao ya kijamii, Lema anahamasisha wanaume wa Kijiji cha Korongwe Asilia, wamuue Mtendaji wa kijiji chao kwa madai ya kuwasumbua wananchi.

Hata hivyo Lema amezungumzia video hiyo kuwa, hakuhamasisha kitu kama hicho na asingeweza kutoa kauli kama hiyo badala yale aliwaambia wanaume wamuoe mtendaji huyo ili asiwasumbue jambo ambalo amejitetea kwa kusema “lugha za kisiasa.”

Kwenye video hiyo, Lema akiwa na baadhi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa Chadema katika Vitongoji vya Forodhani na Fipa, Kata ya Korongwe, anaonekana kutamka neno ambalo limetafsiriwa na Mkuu wa Wilaya kuwa ni kutaka wanaume wamuue mtendaji anayewasumbua.

Lijualikali amesema haiwezekani kiongozi mwenye ushawishi mkubwa wa watu aachiewe kutamba kwa kauli hiyo ambayo imesababisha taharuki kwa wananchi na Mtendaji huo ambaye kwa sasa maisha yake yako shakani, huku kiwango cha utendaji kikishuka.

“Namuagiza OCD wa Nkasi, kuchukua hatua za kisheria mara moja kumuita kokote aliko Godbles Lema ili afike Nkasi akafanyiwe mahojiano kuhusu kauli yake ya kichochezi ya kuhatarisha hali ya usalama wa mtendaji huyo katika eneo letu na kukwaza juhudi za wananchi kufanya shughuli za maendeleo,” amesema Lijualikali.

Akijibu swali ni kwa nini jambo hilo lilitokea muda mrefu lakini wamechelewa kutoa taarifa, Mkuu wa Wilaya amesema walianza kwa uchunguzi kuhusu kauli hiyo ilikuwa na maana gani na ililenga nini kitokee na kwamba wamejiridhisha haikuwa kauli nzuri.

“Lakini badala ya kutumia nafasi ya kujinadi na kujitangaza, wameigeuza fursa waliyopewa kuwa mahali ambapo wanatukana mamlaka, wanatukana viongozi wa nchi. Ukiwasikiliza vizuri, utaona wanatusi, wanakebehi, kuwabeza na kuwatweza Watanzania na nchi yetu kwa ujumla,” amesema Lijualikali.

Alipoulizwa kuhusu kauli hiyo, Lema amekiri kuwepo katika mkutano huo na kueleza alichotamka ni wananchi ‘wamuoe’ mtendaji anayewasumbua siyo kumuua na kusisitiza kuwa hawezi kutamka hivyo.

“Wambie wasikilize hiyo ‘clip’ siwezi kutoa kauli kama hiyo kwa kiongozi, nilichotamka pale ni kuwaambia kama mtendaji anawasumbua basi muoeni, lakini suala la kuua halikuwa sehemu ya hotuba yangu,” amesema Lema.

Akizungumza kwa simu, Mtendaji Daud Ismail amekiri kusikia taarifa ya vitisho kutoka kwa Lema ambaye amesababisha maisha yake kuwa mashakani na utendaji kazi wake kwa umekuwa wa hofu ukizingatia wanafanya kazi mipakani kwenye matukio mengi.

Dau amesema kiongozi kama Lema anapotoa kauli tata kwa maisha ya mtu mdogo kama yeye (Mtendaji) inatia shaka kwa kuwa anasikilizwa na wafuasi wengi hivyo huwezi kujua ndani yake kuna nini.