Lema ataja sababu ya umasikini wa Watanzania

Mbenge wa zamani wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akihutubia wakazi wa Jiji la Mwanza katika eneo la dampo katika mkutano wa hadhara. Picha na Mgongo Kaitira

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema umasikini uliopo Tanzania unatokana na utawala uliopo na si mpango wa Mungu.

Amesema wimbi la vijana kutooa na wengine kuzaa na kupeleka watoto kwa mama zao wakalelewe chanzo ni ugumu wa maisha.

Lema ameyasema hayo leo Jumatatu, Oktoba 23, 2023 kwenye mkutano wa hadhara wilayani Kalambo mkoani Rukwa ikiwa ni muendelezo wa Operesheni +255 Katiba mpya inayoendelea Nyanda za juu Kusini.

“Mama ana miaka sabini ana watoto sita kwasababu kijana amewapeleka nyumbani baada ya kushindwa kulea, aliyesababisha hali hiyo sio Mungu ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dubai ni jangwa inapokea zaidi ya watalii milioni 20 kila mwaka, hawana mbuga za wanyama, wala maziwa kama Tanzania, sisi tuna hifadhi nyingi, maziwa, milima lakini hatuna zaidi ya watalii milioni moja kwa mwaka,’’ amesema.

Amesema kwa nchi ya  Ufaransa utalii  ni mtaji wao  na kwa mwaka wanapokea watalii milioni 80 kwa mwaka, lakini Tanzania yenye vivutio vikubwa kama milima, hifadhi na mapomoromoko ya maji hali ya wananchi sio nzuri.

Pia, Lema ametolea mfano Taifa la Israel ambalo ni jangwa lakini ni nchi ya kwanza kuuza matunda katika soko la dunia akiilinganisha na Tanzania yenye ardhi nzuri, lakini watoto wanatembeea bila viatu na uwepo wa idadi kubwa ya watu wasio na elimu ya juu.

Katika hatua nyingine, alisema viongozi wa Chadema wanapitia mateso mengi kutokana na kutafuta maisha mazuri ya watoto, wajukuu na vitukuu wa Taifa la Tanzania

“Tangu nimeanza siasa nimepelekwa polisi zaidi ya mara 150, mwaka 2015 hadi 2020 nimeenda mahakamani  miaka mitano mfululizo kila mwezi mara nne, tumetishiwa kuuawa, tumeteswa, tumepigwa na tumetishwa,” amesema

Kwa upande wake, aliyekuwa Mbunge wa viti maalum, Upendo Peneza amesema CCM hawataki kukosolewa wala wananchi kusikia namna ambavyo wanairudisha nyuma Tanzania

“Pamoja na rasilimali nyingi zilizopo nchini, Serikali haitoi elimu na afya yenye kuridhisha kwa wananchi, wanafanya hivyo ili waendelee kuwatawala, hakuna haja ya kuendelea kuwepo kwa Mpango wa kunusuru Kaya Masikini (Tasaf) kutokana na rasilimali tulizonazo,” alisema

Kutokana na hali hiyo, Upendo aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi za upatikanaji wa Katiba mpya akiwasisitiza kiongozi yeyote wa Chadema atakayeteuliwa kugombea nafasi ya ubunge wahakikishe wanamuunga mkono na kudhibiti wizi wa kura.

“Uamuzi ni wa kwetu na cha kuanzia tuanze kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa niwaombe viongozi wa Chadema wateueni viongozi ambao watakuwa tayari kuwasiaidia wananchi wao na sio wale wanaowatesa wananchi kupitia Tasaf,” amesema

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati kuu ya Chadema, Patrick Ole Sosopi amesema baada ya CCM kusema Chadema ndio wanachelewesha maendeleo wilayani Kalambo na kushika maeneo yote ya uongozi walitaraji wilaya hiyo ingekuwa mfano wa kuigwa kwa maendeleo.

“Nilitegemea Serikali haitogawa tena fedha za Tasaf kwa wananchi baada ya kushika nafasi zote za uongozi, sikutegemea kukutana na  maisha magumu ya wananchi, viongozi wote ni wa CCM lakini maisha ya Watanzania bado ni magumu, huwezi kutofautisha sura ya mzee na kijana,” amesema.

Olesosopi amewataka wananchi wasidanganywe tena kuchagua viongozi kiholela kwani wao ndio wanapitia maisha magumu.

Amewaomba wananchi wa Kalambo kuanza kuchukua kadi za kidigitali za Chadema na kupuuza upotoshaji kwamba watakapochukua kadi hizo wataondolewa Tasaf

“Tunahitaji mjiunge na Chadem, tumekuja na programu inaitwa Chadema digitali, tunajiandikisha kwenye mtandao kwa Sh2,500, zoezi hili ni muhimu sana tutakapopata idadi ya watu kamili uchaguzi unapofika tunafahamiana,” amesema.