Siasa za uadui zinavyoathiri vyama vya upinzani nchini

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (kulia) akiwa na viongozi wenzake wa chama chake na ACT-Wazalendo wakitoka katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Godbless Lema na katikati ni Kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Ukifuatilia siasa za upinzani tangu kurejea kwa mfumo huo mwaka 1992 utagundua upinzani wa vyama vya upinzani vyenyewe kwa vyenyewe umechangia kuvidhoofisha, kujenga chuki na uadui na kuvipunguzia imani kwa wananchi.

Dar es Salaam. Ukifuatilia siasa za upinzani tangu kurejea kwa mfumo huo mwaka 1992 utagundua upinzani wa vyama vya upinzani vyenyewe kwa vyenyewe umechangia kuvidhoofisha, kujenga chuki na uadui na kuvipunguzia imani kwa wananchi.

Chadema walipotangaza kutoshiriki chaguzi kutokana na kile walichodai ni rafu za chama tawala, waliibuka viongozi wengine wa vyama vya upinzani na kuwaponda, huku wakisema wao watashiriki.

CUF walipogomea uchaguzi wa marudio wa Machi 20, 2016 baada ya ule wa awali ambao CUF kilielekea kupata ushindi kufutwa, vyama vingine zaidi ya 10 vilishiriki na kuponda msimamo wa wapinzani wenzao.

ACT-Wazalendo hivi karibuni kilipotangaza kupinga uteuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina vyama vingine vya upinzani vilijitokeza kupinga.

Kimsingi upinzani wanaofanyiana wapinzani unagawa wananchi ambao baadhi wanaamini vipo vinavyotumika na chama tawala na vingine vinatetea masilahi ya wananchi.

Dhana hizi wakati mwingine zimechangia kudhoofisha upinzani na kuonekana hauna umoja na msimamo. Pale vinaposhirikiana hupata mafanikio kama yaliyoonekana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Wivu, chuki na hasira zilizojengeka au kwa kupandikizwa au kiasili miongoni mwa vyama vya siasa vya upinzani vimesababisha kila kukicha kuwe na malumbano ya viongozi na makada wake.

ACT-Wazalendo walipozindua jengo la ofisi yao mpya wanawakejeli Chadema kuwa wana miaka 30 lakini hawana ofisi nzuri zinazoendana na hadhi ya chama kikuu cha upinzani, CUF nacho kinasemwa hakina jipya bali kimebakia jina.

Chadema kikifanya kitu kizuri kinabezwa na wapinzani wenzao. Wanachama na viongozi wa vyama hivi hawaishi kutengeneza uadui na chuki inayoondoa dhana nzima ya demokrasia ya vyama vingi inayolenga kukuza wigo wa wananchi kuchagua chama au mtu wanayemtaka.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe siku chache zilizopita alisema vyama vya siasa vinapaswa kuachana na siasa za chuki, bali vijielekeze kwenye siasa za kujenga umoja wa kivyama na kitaifa.

“Ukimuona mtu yupo katika chama kingine sio adui yako, bali hujafanya wajibu wa kutosha wa kumshawishi ajiunge na chama chako. Kuna tabia inajengwa ya watu ndani ya chama kujiona sisi ndio Chadema wale wa vyama vingine ni wajinga na watu wabaya, sio sawa, ili chama kikue na kushinda kinahitaji watu na wapigakura”.

Kauli hii ya Mbowe ni somo kwa wafuasi wa chama chake na vyama vingine, kiongozi huyu ana ushawishi mkubwa ndani na nje ya Chadema.

Chadema kimejijengea jina na heshima kubwa kwa kukuza vijana wengi ambao baadhi yao ni viongozi serikali, CCM, vyama vya upinzani na taasisi nyingine.

Miongoni mwao ni David Silinde, David Kafulila, Moses Machali, Juliana Shonza, Mtela Mwampamba, Peter Lijualikali, Pauline Gekul waliokuzwa na Chadema.

Tofauti na wenzake, Zitto Kabwe aliyekulia pia Chadema na kushika wadhifa wa unaibu ukatibu mkuu bara yeye alifukuzwa, lakini hakuhamia CCM, badala yake alijiunga na ACT-Wazalendo Machi 21 mwaka 2015 ambapo hivi sasa ni kiongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar.

Baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema walikuwa wanaona ni fahari kushambulia wanasiasa wa vyama vingine na kukiona chama chao na viongozi ni bora zaidi.

Kuanzia 2015 baada ya John Magufuli (hayati) kuingia madarakani aliwanyofoa baadhi ya wanasiasa kutoka Chadema na vyama vingine vya upinzani na kuwapa vyeo kwenye Serikali yake, hivyo kuwazindua wapinzani.

Wabunge, madiwani na makada wa Chadema walihamia CCM na kuendelea na nyadhifa zao, hali iliyoonyesha hata upinzani kuna watu makini.

Kimsingi vyama vinatofautiana sera na itikadi, ni jambo la kawaida hivyo si sahihi kwa chama fulani kujiona ni bora zaidi kuliko za vyama vingine.

Wanaoweza kuondoa siasa za chuki, uadui na mivutano ni wanachama na viongozi wenyewe kwa kuwahimiza wanachama wao na viongozi wa ngazi za chini kubadilika katika mbinu za kufanya siasa, wataweza kuwavutia wapigakura wengi zaidi.

Baadhi ya watu pia waliaminishwa upinzani ni watu wa vurugu na harakati, hivyo kuogopa kuwaunga mkono.

Hivi karibuni akiwa katika ziara ya kukagua shughuli za chama, Mbowe ambaye ni mbunge wa zamani wa Hai, mkoani Kilimanjaro alisema kuna viongozi wazuri wapo vyama vingine vya siasa, akisema mtu kuwepo Chadema asijione ni mtakatifu.

“Inawezekana katika jamii yetu wapo watu kwenye vyama vingine wana watu wazuri, kazi yenu kama chama ni kujenga ushawishi kwa sababu chama ni watu. Asitokee kiongozi wa chama akafunga milango kwa watu kutoka vyama vingine kuingia Chadema.

“Chama cha siasa ni watu, ukijifungia kwenye chama chako wewe, mkeo na mwanao hicho chama kitabaki hivyo hivyo kwa miaka 20 au 30 ijayo. Chadema imekua kwa sababu sera yangu ni kufungua milango kwa yeyote anayekuja,” alisema Mbowe.

Mbowe aliwaambia Chadema kama wanataka kujenga Taifa la Tanzania, lenye nguvu, mshikamano na umoja, lazima waanze kuonyesha umoja ndani ya chama hicho. Alisema Chadema hakiwezi kuwa chama kuhubiri ubinafsi, kuwatenga Watanzania wengine.

“Viongozi wa Chadema wakati wote jengeni chama cha kuunganisha watu, sio kuwatenga watu, msiwahukumu wengine kwa misimamo yao kubaki katika vyama vingine. Fanyeni kazi ya kuwashawishi ili waone umuhimu wa kuja tukijenge Chadema itakayopendwa na kuunganisha watu wote, hatujengi chama cha matusi wala kudhalilisha, bali fursa ya demokrasia,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu, alisema hafurahishwi na namna mivutano inavyoongezeka miongoni mwa vyama vya siasa vya upinzani

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya alisema Mbowe amezungumza ukweli na kauli yake inaashiria umoja miongoni mwa vya upinzani lakini ni vema baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wakaacha kujiona wao ndiyo bora kuliko wengine

“Wanajiona wao ndio kila kitu, wanajua kuongea na kutetea Watanzania, suala hili ndilo lililoiua Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi)” “Ndivyo kiongozi anavyopaswa kuwa namuunga mkono kwa hatua hii kwa sababu inaashiria dalili nzuri kwa vyama vya upinzani,” alisema Sakaya aliyewahi kuwa mbunge wa Kaliua mkoani Tabora akiungwa mkono kwa tiketi ya Ukawa

Kaimu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini aliungana na viongozi wenzake kwa kumshukuru Mbowe, akisema kumekuwa na usugu wa suala kwa baadhi ya watu kushambuliwa wenzao pindi wanapotoa maoni tofauti na mitizamano yao.

“Kumekuwa na tabia ya kurushiana vijembe na matusi haina afya”