DC: Wakulima Kiteto tengenezeni uongozi kuepuka migogoro

Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mbaraka Batenga akiongea na wakulima na wafugaji . Picha na Mohamed Hamad

Muktasari:

  • Wakulima huwa mnanipa tabu sana mimi nikitaka kuwapata haswa mkiwa na migogoro inaniwia  vigumu kuitatua.

Kiteto. Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mbaraka Batenga amesema anapata changamoto kubwa anapotaka kutatua migogoro ya ardhi wilayani humo kutokana na wakulima kutokuwa na uongozi unao julikana.

Batenga ameyasema hayo Leo jumatano Mei 24.2023 akizungumza na wakulima na wafugaji kuwa ni rahisi kupata uongozi wa wafugaji lakini sio wakulima

"Sasa hii migogoro ya ardhi namna ya kuitatua ni kukutana...haswa wakulima ambao huwa hawana uwakilishi makini kutoka juu mpaka chini huwa wananipa tabu sana namna ya kuwapata," amesema na kuhoji.

"Uwakilishi wenu umekaaje? Ukitaka uongozi wa wafugaji ni rahisi kuupata lakini ninyi wakulima kuwapata ni changamoto… nikienda kata ya Matui napata kiongozi gani? Kwa hiyo kama mna uongozi wenu mniletee ili Wilaya tupate pakuanzia."

DC Batenga amesema hata shida katika kupata viongozi wa wafugaji, kwani mfumo wao wa uongozi umekaa vizuri na wana heshimiana sana kwani wanaishi kwa rika.

"Sasa nizungumze hapa na mnielewe viongozi wa mila...wafugaji mpo hapa, kuna tabia za watu kulazimisha kulisha mifugo kwenye mashamba ya watu...nitumie neno kulazimisha yaani watu wanakuja wanalazimisha ngombe lazima ale shamba la mtu hapana," ameonya.

DC huyo amewata wafugaji hao kuwakataza vijana wao wanaowapa mifugo kuchunga, kutobariki zoezi hilo na kwamba wawaonye kuwa na tabia ya kuthamini mali za watu wengine.

Ameseam kikawaida wafugaji wana desturi ya kuishi kama wako kwenye grupu moja la (whatsapp) na kuwataka watumie utaratibu huo kuonyaa vijana wao kuacha tabia ya kulazimisha kuchunga mifugo kwenye mashamba ya watu.

"Haya ni maisha ya watu unavyopenda mifugo yako ndio hivyo hivyo mkulima anavyopenda shamba lake...kwa bahati mbaya sana mwaka huu mtu alishakula hasara mapema sana amebakiza kidogo sana kile kidogo alichobakiza mtu anasukumia mifugo humo ndani hapana…muwaonye  vijana," amesisitiza

"Usimkabidhi mtu mifugo kwenda kuchunga wakati hujamwambia hili...na matokeo yake wanashambuliwa wengine wanapozuia mifugo isiingie shambani na kibaya zaidi baada ya tukio wanakimbia ," alizungumza kwa uchungu

Kwa upande wake Ngayoni Ole Lebakari kiongozi wa mila Kiteto amekiri kuwa migogoro ya ardhi Kiteto ni tatizo na kuahidi kuongea na wafugaji

"Tutakaa na wafugaji kuongea nao alichosema DC naye ajue pia wakulima wamelima kila mahali sasa sisi tukachunge wapi watuachie nyanda za malisho kupunguza migogoro," amesema.

Mbaruku Chambali mwakilishi wa wakulima Kiteto amesema tatizo la Kiteto wafugaji ndio wenye ardhi kubwa...wao ndio wauzaji na pia ni wakulima wakipata fedha wananunua ngombe zaidi sasa watachunga wapi wakati eneo wameuza mengine wanalima," amesema Mbaruku.