DCEA: Bila mateja, watu wangelala milango wazi

Muktasari:

  • Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema zaidi ya asilimia 80 ya uhalifu unaofanyika kila siku Tanzania unahusisha kundi la watu wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema zaidi ya asilimia 80 ya uhalifu unaofanyika kila siku Tanzania unahusisha kundi la watu wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.

Katika mahojiano maamulu na Mwananchi hivi karibuni ofisini kwake, Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Aretas Lyimo amesema kusingekuwa na matumizi ya dawa za kulevya nchini, watu wangelala milango wazi huko mitaani.

“Hasara ni kubwa sana inayotokana na matumizi ya dawa kulevya nchini, ukiacha gharama ambazo Serikali inatumia kwenye matibabu, kiusalama hali ni mbaya. Asilimia kubwa ya waharifu duniani kote ni watumiaji wa dawa za kulevya, ndio vibaka, panya road, majambazi, ndio wakata mapanga,”amesema.

“Asilimia kubwa ya wale Panya road waliokamatwa, walikutwa wanatumia dawa za kulevya, asilimia zaidi ya 80 ya matukio yote ya uharifu yanafanywa na watumiaji wa dawa za kulevya.”