DED Igunga afariki ajalini Mbeya

What you need to know:

  • Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Fatuma Latu na watu wengine wawili amefariki dunia baada ya kupata ajali ya gari katika eneo la Inyala mkoani Mbeya.

Tabora. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Fatuma Latu na watu wengine wawili amefariki dunia baada ya kupata ajali ya gari katika eneo la Inyala mkoani Mbeya.

Ajali hiyo imetokea leo Jumatano, Septemba 14, 2022 wakati akiwa anatoka kwenye kikao cha Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) jijini Mbeya.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Igunga, Lucas Bugota amesema kuwa walikuwa wote kwenye safari lakini kwenye magari tofauti.

"Mi ndio naelekea huko kwani wao walikuwa nyuma yetu, yaani ndio hivyo tumepata msiba" amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Dk Rashid Chuachua amethibitisha kutokea kwa ajali na vifo hivyo katika eneo la mteremko mkali wa mlima Inyala eneo la pipe line Wilaya ya Mbeya.

''Nimepata taarifa kuna ajali imetokea sasa naelekea eneo la tukio mpaka sasa kuna vifo vya watu watatu akiwepo Ded Igunga, dereva wake na utingo wa lori ''amesema.

Amesema kuwa Mkurugenzi wa Igunga na dereva wake walikuwa wanatokea Mkoani Mbeya ambako alikuja kwenye kikao cha Alat wakirejea kituo chake cha kazi.

Mashuhuda wa ajali hiyo wamedai kuwa chanzo cha ajali hiyo ni lori kufeli breki na kugonga magari mawili kwa nyuma yaliyokuwa yakielekea barabara kuu ya Mbeya kwenda jijini Dar es Salaam.

Zamda Mickdad amesema kuwa akiwa katika eneo hilo alisikia mlio wa kishindo na walikokimbilia eneo la tukio walikuta moja la gari likiwa limelaliwa juu na kulikuwepo na watu wawili ndani.

''Eneo hilo ni kama lina shida maana hazipiti siki mbili lazima magari ya mizigo yafeli breki na kusababisha ajali mbali zinazogharimu maisha ya watanzania ''alisema.

Ajali hiyo imetokea ikiwa ni siku tatu zimepita baada ya Makamu wa Rais Dk Philip kutoa maagizo kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuanza ukaguzi wa magari ya mizigo katika eneo hilo.