Dereva afariki dunia, watatu wajeruhiwa ajali ya lori Njombe
Muktasari:
- Gari lililokuwa linaendeshwa na Adriano Samweli (40), mkazi wa Kibondo mkoani Kigoma, limepata ajali na dereva huyo kufariki papo hapo baada ya kushindwa kulimudu gari hilo.
Njombe. Mtu mmoja ambaye ni dereva amefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa kufuatia ajali ya gari aina ya Fuso kutumbukia korongoni katika Kijiji cha Igumbilo, Kata ya Lupila, Wilaya ya Makete mkoani Njombe.
Ajali hiyo imetokea baada ya dereva kushindwa kulimudu gari lake na hatimaye likatumbukia kwenye korongo na kusababisha kifo chake, huku watu wengine watatu waliokuwemo kwenye lori hilo wakijeruhiwa.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Juni 9, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo huku akitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni dereva kushindwa kulimudu gari hilo kabla ya kutumbukia kwenye korongo hilo lenye mteremko na kona kali.
Kamanda huyo ameeleza kuwa ajali hiyo imetokea usiku wa kumkia Juni 8, 2024 katika Kijiji cha Igumbilo wilayani humo ambapo gari hilo likiwa limebeba mzigo wa viazi huku likiwa na watu wanne.
Kamanda Banga amefafanua kuwa gari ambalo lilikuwa linaendeshwa na Adriano Samweli (40), mkazi wa Kibondo mkoani Kigoma ambaye alifariki papo hapo baada ya kushindwa kulimudu gari hilo.
“Gari hilo lilikuwa na mzigo wa viazi kutoka eneo la Lupila likielekea Dar es Salaam ambapo alipofika kwenye mteremko, gari hilo lilimshinda dereva anaitwaye Adriano na kutumbukia korongoni, dereva alifariki hapo hapo,” amesema kamanda huyo.
Kamanda Banga ametaja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Ridhiki Shabani (38) mkazi wa Kibondo mkoani Kigoma, Emmanuel Abdudi (28) na Abdudi Ibrahim (30) wote wakiwa wakazi wa Ludembwe.
Amesema kuwa baada ya ajali hiyo kutokea majeruhi hao walipata majeraha sehemu mbalimbali za miili yao na kupatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Lupila huku hali zao zikiwa zinaendelea vizuri na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika kituo hicho.
Hata hivyo, Kamanda Banga ametoa wito kwa madereva wageni kuchukua tahadhari kutokana na mkoa huo kuwa na milima na miteremko mikali ikiwa ni pamoja na kuwatumia madereva wenyeji wanapokuja kuchukua mizigo ili kuepusha matukio ya ajali.
“Mfano, ajali hii inaonyesha ilikuwa ndiyo mara ya kwanza kwa dereva kuja mkoani Njombe, hajui vizuri mazingira ya huku, hivyo niwaombe madereva kama ambavyo mtu anenda Dar es Salaam anakuwa mgeni, anaogopo kugongwa, anagodi dereva mzoefu, basi hata wanapofika huku wanaweza kufanya hivyo na anapofika katika eneo zuri anaweza kuendelea na safari yake,” amesisitiza Banga.
Hata hivyo, taarifa za awali za mganga mfawidhi wa Kituo cha Afya Lupila, Dk Isack Lulindi amethibitisha kupokea majeruhi watatu waliopatiwa matibabu na tayari wameruhusiwa kwenda nyumbani. Pia, wamepokea mwili mmoja wa marehemu ambao umehifadhiwa katika kituoni hicho.