Dereva wa basi lililoua wanafunzi wanane Arusha apandishwa kizimbani

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Mshtakiwa alikamatwa Aprili 12, 2024 asubuhi na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za kusababisha ajali iliyouwa wanafunzi wanane wa Shule ya msingi Ghati Memorial, baada ya basi kusombwa na maji ya mafuriko.

Arusha. Dereva wa basi la Shule ya Msingi Ghati Memorial lililouwa wanafunzi wanane baada ya kusombwa na maji jijini Arusha, amepandishwa kizimbani akikabiliwa na mashtaka manane likiwamo la kuua bila kukusudia.

Dereva huyo, Lukuman Hemed amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha, leo Jumanne Aprili 16, 2024 mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Sheila Mamento.

Hata hivyo, kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 30, 2024 itakapokuja tena kwa ajili ya kutajwa  baada ya mawakili wawili wa upande wa Jamhuri wakiongozwa na Amina Kiamba kusema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Hata hivyo, mawakili hao wamepinga mshtakiwa asipatiwe dhamana kwa madai kuwa usalama wake uko mashakani kwa sababu bado watu wana hasira naye.

Awali, hakimu alipokuwa akiahirisha kesi hiyo, alisema dhamana iko wazi kwa mshtakiwa.

Hakimu Mamento alimuuliza mshtakiwa kama anaridhia pingamizi hilo, alikubali na kupelekwa gereza la Kisongo hadi Aprili 30, 2024.

Ajali hiyo ilitokea Aprili 12, 2024 saa 12 asubuhi, baada ya gari hilo aina ya Toyota Hiance namba T 496 EFK alilokuwa akiendesha Hemed likiwa na watu 13 kutumbukia kwenye korongo na kusababisha wanafunzi hao kufariki baada ya kusombwa na maji.

Katika ajali hiyo, watu watano waliookolewa wakiwa hai akiwemo mshtakiwa, mwalimu mwangalizi wa watoto na wanafunzi watatu.