Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simanzi miili tisa ya waliokufa maji ikiagwa

Muktasari:

  • Walioagwa ni Winfrida Emanuel aliyekuwa anasoma darasa la awali, Abigail Peter  darasa la sita,  Abialbol Peter (awali), Morgan Emanuel (awali), Articia Emanuel darasa la tatu, Shedrack Emanuel  darasa la sita, Dylan Jeremiah, Noela Jonas (awali) na Brian Tarangie ambaye alikuwa anawaokoa watoto hao.

Arusha. Ni simanzi, vilio na majonzi. Ndivyo ilivyoonekana kwa waombolezaji, wazazi na walezi waliopoteza watoto wanane na msamaria mwema mmoja aliyejaribu kuwaokoa wanafunzi hao waliosombwa na maji walipokuwa kwenye gari la Shule ya Msingi Ghati Memorial.

Ndoto za watoto hao zilikatishwa na ajali hiyo iliyotokea Aprili 12, 2024 baada ya gari hilo lililokuwa na namba za usajili T 496 EFK, kudumbukia kwenye Korongo la Mbaashi, Mtaa wa Engosengiu, Kata ya Sinoni, Arusha.

Katika maombolezaji hayo yaliyofanyika Viwanja vya Viwanja vya Shule ya Sekondari Sinoni leo Jumapili Aprili 14, 2024,  Serikali imetoa mkono wa pole wa Sh5 milioni kwa familia ya msamaria huyo, Brian Tarangie (34) na Sh1 milioni kwa kila familia iliyopoteza mtoto kwenye ajali hiyo iliyotokea mwishoni mwa wiki.

Waombolezaji wengine wakiwamo jamaa na wananchi wa Kata ya Sinoni, walianza kuwasili uwanjani hapo saa mbili asubuhi wakisubiri kuletwa kwa miili hiyo.

Miili hiyo iliwasili uwanjani hapo saa 5:32 asubuhi na kabla ya kushushwa, walitangulia wazazi wao walioonekana kuwa na majonzi makubwa huku wengine wakipoteza fahamu.

Baada ya wazazi hao kukaa sehemu maalumu iliyokuwa imeandaliwa, miili hiyo ilianza kushushwa katika viwanja hivyo.

Wazazi hao waliposikia majina ya watoto wao yakitajwa wakati wa ushushwaji wa miili hiyo walisikika wakiwaita kwa uchungu.

Katika tukio hilo, familia mbili  zimebaki pweke baada ya kila familia kupoteza watoto wawili  pekee.

Walioagwa ni Winfrida Emanuel aliyekuwa anasoma darasa la awali, Abigail Peter  darasa la sita,  Abialbol Peter (awali), Morgan Emanuel (awali), Articia Emanuel darasa la tatu, Shedrack Emanuel  darasa la sita, Dylan Jeremiah, Noela Jonas (awali) na Brian Tarangie ambaye alikuwa anawaokoa watoto hao.

Akizungumza katika maombolezaji hayo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mhatehengerwa amewataka wazazi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki mvua zinaponyesha.

Pia, amesema wamekubaliana kwa magari ya shule zote jijini hapa kuanza kuchukua wanafunzi saa 1:30 asubuhi mvua zinaponyesha ­­­ili hata wanapopata changamoto waweze kupata msaada.

Askofu Isack Amani wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha akibariki miili ya wanafunzi nane wa Shule ya Ghati Memorial jijini Arusha waliokufa maji Aprili 12, 2024. Picha na Janeth Mushi

Mtahengerwa amesema walipopata taarifa za ajali hiyo mwishoni mwa wiki ziliwachanganya na kuwahuzunisha.

Amesema walilazimika kushirikiana na wananchi wakiwamo vijana waliokuwa eneo hilo na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hadi katika kingo ya mto mpakani mwa wilaya za Simanjiro na Arumeru kutafuta watoto hao.

Katika kipindi hiki ambacho maeneo mbalimbali yana mvua kubwa, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanachukua tahadhari pindi mvua zinapokuwa kubwa na kutokuwapeleka watoto shule.

 “Katika kipindi hiki si Arusha tu bali maeneo mbalimbali yanakabiliwa na mvua, hali ni mbaya na nitoe wito kuwa maji yanayotembea  sio ya kufanyia majaribio iwe mpita njia, bodaboda au mwenye gari, maji yanayotembea siyo ya kufanyia majaribio,”amesema Mtahengerwa.

“Wazazi katika kipindi hiki tunachoendelea kupata mvua nyingi, ukioa hali siyo nzuri usimpeleke mtoto shule,tumeshatoa maelekezo magari yote ya shule  kuanza kutembea saa 1:30 asubuhi kwa kuwa kunakuwa kumepambazuka na tunaweza kupata msaada wa haraka panapotokea tatizo.”

Awali, kabla ya kuagwa kwa miili hiyo kulifanyika ibada maalumu iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Arusha, Mhashamu Askofu Isack Amani akisema wazazi na walezi wa familia hizo wanapaswa kupokea msiba huo kwa imani  na sio kuhukumu licha ya kuwa ajali hiyo kukatisha ndoto za wanafunzi na furaha za wazazi wao huku akisisitiza utii wa sheria.

“Kwa masikitiko makubwa tumepokea taarifa hizi za ajali hii iliyokatiza ndoto za maisha za watoto hawa, furaha ya wazazi, watoto walitoka nyumbani mapema kuwahi shule ila hawakufika shule, hawa wameondolewa kwetu mapema sana poleni sana wazazi, hakuna maneno mengine zaidi ya pole,”amesema Askofu  Amani.

“Tupokee msiba huu kwa imani, siyo kuhukumu wala kukata tamaa, tumuombe Mungu awapokee. Imani ituongoze katika kupokea msiba huu, somo tunalopata katika hili ni kuchukua tahadhari kabla ya ajali kwa kuwa zipo ajali nyingi zinatokea nyumbani kwenye familia.

 “Ziko ajali za kukanyagana sana nyumbani zinatikisa, ziko ajali za ukatili wa kijinsia kwenye familia zetu watu wanafanyiana zinaacha maumivu  na majonzi makubwa, yako mengi ambayo hatusemi waziwazi ila somo la kujifunza hapa ni kujali na kutii amri za Mungu, kanuni, sheria za barabarani na mtu akikwambia punguza mwendo fanya hivyo. ”

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Mhandisi Juma Hamsini amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mkono wa pole wa Sh5 milioni kwa familia ya  Brian ambaye ni msamaria mwema aliyejitolea kuokoa wanafunzi hao kwa bahati mbaya alifariki dunia katika tukio hilo.

Waombolezaji wakiaga miili ya wanafunzi nane wa Shule ya Msingi Ghati Memorial iliyopo jijini Arusha na muokoaji mmoja waliokufa maji Aprili 12, 2024. Picha na Bertha Ismail

“Tuna mwenzetu Brian ambaye yeye alishiriki kuokoa huyu ni shujaa wetu katika Mkoa wa Arusha lakini shujaa kwa nchi yetu, tumeamini kifo hakina hodi, tumetoa mkono wa faraja kwa kila mfiwa  Sh1milioni, kugharamia maziko, lakini kwa niaba ya Rais ametoa mkono wa pole maalumu wa Sh5 milioni, kwa familia ya Brian, ”amesema Hamsini.

Shule hiyo  inayomilikiwa na Mbunge wa Tarime Mjini, Michael Kembaki ambaye pia alikuwepo uwanjani hapo, akizungumza kwa niaba ya uongozi wa shule hiyo, Mchungaji Boniphace Mkama amesema hawana lugha ya kuzungumza kwa kuwa tukio hilo limetesa  mioyo yao kwa kiwango kisichoelezeka.

“Kiukweli tuliwazoea wanafunzi hawa wanane waliokuwa wakisoma pale, Mungu atutie nguvu zaidi na sisi kama taasisi tuko pamoja nanyi familia katika msiba huu, kwa kuwa sio wenu peke yenu ni wetu sote. Tunashukuru Serikali ikiongozwa na mkuu wa wilaya ambaye kuanzia siku ya kwanza tulikuwa naye hadi tulipokamilisha kutafuta miili yote,”amesema Kembaki.

Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Iranghe amesema ni wakati wa Serikali kuangalia wanaoendesha magari ya shule kwa kuwafanyia usaili maalumu.

Pia, ametaka kikosi cha usalama barabarani kutoa mafunzo maalumu kwa madereva wa magari ya shule.

Katika ajali hiyo watu watano akiwamo dereva, mwangalizi wa watoto (matron) na wanafunzi watatu walinusurika kifo baada ya kuokolewa.


Mwanafunzi amlilia mwenzake

Mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Ghati Memorial, Rehema Elisifa amesema alikuwa rafiki wa karibu wa Abigael aliyefariki katika ajali hiyo.

Amesema rafiki yake alikuwa mcheshi na mchangamfu hasa  wanapokuwa nje ya darasa kwa kuwa wamekuwa wakicheza pamoja na kushirikiana katika mambo mbalimbali ikiwamo kupeana notisi za masomo.

"Sijui kilichotokea kwa rafiki yangu, lakini nimepoteza mtu muhimu sana, nilikuwa nacheza naye wakati mwingine tunakula na kusoma pamoja hasa pale mwalimu alipofundisha hatujaelewa tunakaa kujadili pamoja, ila Mungu ameamua kunitenganisha naye," amesema huku akilia.