Dereva wa pikipiki afariki, ‘helmet’ yatajwa

Baadhi ya waombolezaji mjini Kibaya wakiwa katika makaburi kumzika Mohamed Yusufu (26) aliyepoteza maisha kwa ajali ya pikipiki. Picha na Mohamed Hamad

Muktasari:

  • Ni baada ya kupata ajali ya pikipiki na kutumbukia korongoni akiwa eneo la Kaloleni Kiteto kisha kulaliwa na pikipiki na kupoteza maisha.

Kiteto. Dereva wa pikipiki Mohamed Yusuph (26), mkazi wa Kaloleni, wilayani Kiteto, mkoani Manyara, amepoteza maisha kwa kunyongwa na kamba ya kofia ngumu ya pikipiki (helmet), baada ya kupata ajali na kutumbukia korongoni.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkaoani Manyara, ACP George Katabazi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Novemba 17, 2023; huku akisema marehemu alikuwa peke yake wakati akiendesha pikipiki.

Amesema tukio hilo limetokea Novemba 16, 2023 eneo la Kaloleni Kiteto wakati marehemu akitoka katika moja ya makazi yao kuelekea mjini Kibaya.

"Marehemu alikuwa anatoka kwenye kambi yao ndogo ambako huwa wanaishi kuelekea mjini Kibaya akiwa na pikipiki akiendesha kisha kutumbukia korongoni Novemba 16.2023 jioni bila kujulikana mpaka hii leo Novemba 17, 2023 alipoonwa na watu na kutoa taarifa," amesema ACP Katabazi

Akizungumza na Mwanchi Digital, Amos Charles ambaye wa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kaloleni: "Mohamed tulikuwa naye alitoka nyumbani kwa baba yake Azizi akapitia hapa akanipigia simu akasema Amos kamba iko wapi nikamwambia angalia kwenye chumba cha pili hapo akachukua kamba akaenda zake shambani Mirerani kuchukua mkaa,”

“...alirejea saa 12 jioni na kutukuta tukiwa na baba yake, wakashusha mkaa wakaingiza ndani, baada ya hapo aliondoka tena na pikipiki yake na ambapo ndiyo inaonekana alipata ajali ya kutumbukia katika korongo na kupoteza uhai wake,” amesema Amos

Kwa upande wa Moses Lukumay, mmoja wa majirani wa marehemu amesema: "Tumekuta kijana ameanguka, pikipiki imemlalia mguu shingo imeelekea kwenye korongo kwa hiyo tunasikitika sana, wanasema kuanzia saa 11 ndio alipotea na kwamba element ndiyo ilichangia kumuua."

Ndugu jamaa na marafiki wa karibu wa marehemu huyo wamezungumzia tukio hili kuwa limewasikitisha sana kwani waliagana naye na wala hakuugua

"Ni juzi tu ndio ilikuwa harusi yake... kwa hiyo tumesikitika sana, harusi yake tulikula kweli kweli watu walikula wali wa kushiba, watu wengi wamepokea kifo hiki kwa huzuni sana kwa sababu hili tukio marehemu amefariki kwa ajali ya pikipiki imekutwa imemlalia na kufa," amesema Hassani Chomadudu jamaa wa marehemu

Kwa kweli hili tukio hata sisi viongozi wa chama tumesikitika sana kwa sababu kijana huyu alikuwa mdogo sana tumepoteza nguvu kazi ya Taifa na hata familia yake wamepoteza mtu muhimu," amesema Luis Marting

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kaloleni, Shabani Sendalo amesema baada ya kupata taarifa alienda eneo la tukio na kushuhudia ajali hiyo akisema imeumiza mioyo ya walio wengi.

"Ni ajali ya pikipiki, alikosea barabara akaingia kwenye shimo tulivyoenda tulimkuta kwenye shimo hapo tumeona kuwa helement ndio imemnyonga alivyoanguka na siku zake zimefika tunamshukuru Mungu,” amesema Sendalo Mwenyekiti wa Mtaa wa Kaloleni.