Dk Bashiru awataja tena Nape, Bashe

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema licha ya mchango mkubwa alioutoa kwa chama hicho, mbunge wa Mtama, Nape Nnauye anahitaji kupikwa, kusikilizwa, kuaminiwa na kusimamiwa.

Mbali na Nape, pia amemtaja mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe akisema ni miongoni mwa vijana waliopitia katika Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wakati mfumo wa kuandaa viongozi ukiwa umekufa.

Dk Bashiru alikuwa akizungumza jana katika mahojiano maalumu na Tido Mhando kupitia kituo cha televisheni cha ZBC2 kuhusu Muungano uliotimiza miaka 55.

Mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alizungumzia pia umuhimu wa vijana kuandaliwa kupitia mifumo ya chama.

Julai 28, 2018, akizungumza na wanachama wa CCM mjini Nzega, Dk Bashiru alisema kuwa Nape na Bashe ni watukutu wanampa wakati mgumu kutokana na udadisi wao wa mambo mbalimbali wawapo bungeni, jambo linalowafanya mawaziri wafikiri kwa kina kabla ya kutoa majibu na maamuzi.

“Nawafahamu wabunge hawa kuwa ni watukutu kwelikweli, wadadisi kwelikweli, lakini wanapishana, kwa kuwa Nape ni mdadisi na mtukutu ambaye joto lake ni kali, hivyo kazi yake ni kupoza,” alisema.

Jana, Dk Bashiru alisema kati ya mambo ambayo CCM haiyafanyi kwa muda mrefu kwa sasa ni pamoja na kuwaandaa viongozi wao na alirejea historia akisema awali chama hicho kilikuwa na vyuo vya kuandaa makada na viongozi kabla ya kurejeshwa serikalini.

“Sasa Umoja wa Vijana ambao ulikuwa ndiyo tanuru la vijana, likakosa hiyo faida ya vijana kuandaliwa. Sasa kina Bashe na Nape wametokea Umoja wa Vijana kipindi ambacho maandalizi yao yalikuwa yanasuasua, kipindi ambacho umoja wa vijana ukageuzwa chombo cha wagombea kujipima umaarufu wao, hasa wagombea urais,” alisema Dk Bashiru.

Alisema, “bahati mbaya chama kikawa mbali na vijana wale na bahati mbaya vijana ni watukutu, wakati wote akili inachemka. Ndivyo Bashe na Nape walivyopatikana, walitokea Umoja wa Vijana, wakaaminiwa, wakapewa nafasi za uongozi wakaenda wakawa wabunge kwa hiyo ule udadisi wao ukaonekana una usumbufu fulani.”

Huku akimtolea mfano Nape, Dk Bashiru alisema vijana hao wanahitaji kusikilizwa, kuwaandaa, kuwaamini na kuwasimamia kama wanakwenda kinyume na taratibu, huku akisema wana mchango mkubwa katika chama hicho.

“Mtu kama Nape Nnauye amekuwa mwenezi wetu jasiri kabisa wa kutetea chama, lakini kwa kweli anahitaji kupikwa. Kwa hiyo nilipokuwa nasema siyo kwamba nilikuwa nakubaliana nao kila kitu. Kwa hali ilivyo kwa kweli ni kati ya watu kwa maoni yangu wana mchango mkubwa,” alisema Dk Bashiru.

Alisema ili kuwaandaa viongozi chama hicho kina mpango wa kujenga vyuo vya itikadi na uongozi ambavyo ni pamoja na chuo kitakachoshirikisha nchi sita na vyama vya ukombozi wa Afrika.

Muungano

Kuhusu Muungano, Dk Bashiru licha ya kuunga mkono muundo wa Serikali mbili, alisema bado Taifa linatakiwa kuwa na mjadala wa Katiba kwa ajili ya kujenga mfumo wa kisiasa unaofaa.

Alisema kwa muda mrefu suala hilo limekuwa likijitokeza na aliitaja Tume ya Jaji Francis Nyalali, Kamati ya Jaji Robert Kisanga na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba akisema mjadala wa Muungano bado haujahitimishwa.

“Kwa hiyo jambo hilo halijahitimishwa, lakini kwa maoni yangu mimi bado muundo wa sasa umethitisha umadhubuti wake na uhimilivu wake kwa kiwango ambacho wasiwasi uliopo unadhibitika na Watanzania wanazidi kuwa wana umoja zaidi kuliko idadi ya Serikali,” alisema Dk Bashiru.

“Kwa hiyo si tu mjadala wa Katiba ili tubadilishe aina ya Muungano, lakini mjadala wa kuhusu aina ya mfumo wa kisiasa unaotufaa na umuhimu wa uchumi unaotufaa.”

Maalim Seif na ACT Wazalendo

Kuhusu mpasuko ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), Dk Bashiru alisema walishtushwa na kambi ya aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kuhamia ACT Wazalendo.

“Ndiyo, tulishtuka zaidi kwa sababu hatukujua mabadiliko yale, baada ya CUF chama kilichokuwa na mshikamano na kilikuwa na mgogoro, na tulishtuka kwa sababu hatukuwa na utabiri,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuimarika kwa ACT Wazalendo na vyama vingi hakuitishi CCM huku akitoa mfano wa wabunge wa vyama hivyo kuhamia chama tawala.

Akijibu swali kuhusu malalamiko ya wapinzani ya kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara ilhali CCM wanafanya, alisema mikutano hiyo haijakatazwa bali kilichokatazwa ni mikutano ya operesheni.

“Kwa hiyo sijafanya mikutano ya hadhara ambayo imezuiwa. Siyo yote imezuiwa, madiwani si wote kwa sababu hatuwalazimishi, wabunge wote wakiwemo wa viti maalumu wanaruhusiwa.

“Mikutano iliyozuiwa ni ile ya operesheni, kama vile ni ya kitaifa na kuanza kuzunguka nchi nzima.”

Lowassa ndani ya CCM

Kuhusu kurejea CCM kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Dk Bashiru alisema kulikuwa na mazungumzo ya muda mrefu na alitakiwa aombe upya uanachama.

“Kulikuwa na mazungumzo kwa upande wa chama baada ya kupokea maombi yake. Na yeye hakuwa mtu wa kwanza, wapo wanachama tuliwafukuza ndani ya chama wakandika barua wenyewe wakikiri makosa yao. Vikao vilikaa wakafikiriwa, wakasamehewa na Lowassa alikuwa mmoja wao,” alisema Dk Bashiru.