Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Biteko ajibu hoja za wabunge, agusia gharama za umeme

Muktasari:

  • Bunge la Tanzania limeipitisha bajeti ya Wizara ya Nishati ya mwaka 2025/26 ya Sh2.2 trilioni iliyowasilishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.

Dodoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, amejibu hoja mbalimbali za wabunge, ikiwemo suala la kukatika mara kwa mara kwa umeme na gharama za kuunganishiwa umeme kwa wananchi.

Hoja nyingine iliyotolewa na wabunge wakati wa kujadili bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2025/26 ya Sh2.2 trilioni ni vituo vya mafuta kujengwa kiholela.

Akihitimisha mjadala wa bajeti hiyo jioni ya leo, Jumanne Aprili 29, 2025, Dk Biteko amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imeanza kufanya tafiti ya gharama za huduma ya umeme nchi nzima.

Amesema kwa sasa bei ya kuunganisha umeme vijijini kote ni Sh27,000. Kwa maeneo ambayo ni vijiji-miji, Serikali inaendelea kuunganisha umeme kupitia Mpango Mahsusi wa Taifa wa Nishati.

“Kwa mwaka wa fedha 2025/26, Serikali kupitia REA (Wakala wa Nishati Vijijini) imetenga Sh40 bilioni ili kuanza kuunganisha umeme kwa bei ya Sh27,000 katika maeneo mbalimbali yenye sura ya vijiji-miji,” amesema.

Amesema Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya wastani wa asilimia 58 ya gharama za kuunganishia umeme katika maeneo ya mijini ambapo gharama halisi ni Sh546,764 lakini mwananchi hulipa Sh320,960.

Amesema hivyo Serikali hutoa ruzuku ya wastani wa Sh112 bilioni kwa mwaka kwa ajili ya kufidia gharama halisi za kuunganishia umeme.

Aidha, Dk Biteko amesema Serikali imepokea ushauri wa kuwakopesha wananchi waliounganishiwa umeme ili walipe gharama kwa awamu.

“Ushauri huu unafanyiwa kazi ili kuona namna bora ya kuutekeleza. Pamoja na juhudi hizo, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji imeanza kufanya tafiti ya gharama za huduma ya umeme nchi nzima,” amesema Dk Biteko.

Kuhusu changamoto ya kukatika katika kwa umeme, Dk Biteko amesema Serikali imekuja na mpango wa gridi imara wa kujenga vituo vya kupoozea umeme kwa kila wilaya.

Amezitaja hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kutekeleza mradi huo kuwa ni kununua viwanja kwa ajili ya kujenga vituo hivyo katika wilaya zote.

“Ujenzi wa vituo katika wilaya 14 umeanza na unaendelea. Utekelezaji utaendelea katika wilaya nyingine kwa kadri ya upatikanaji wa fedha,” amesema na kusisitiza kuwa anatambua changamoto ya kukatika katika kwa umeme na wanaifanyia kazi.

“Mwananchi anachokitaka ni umeme. Unapokatika hahitaji maneno; hata ukizungumza nini, yeye anataka umeme. Tumewasikia waheshimiwa wabunge na tunakwenda kufanyia kazi,” amesema.

Hata hivyo, amesema imebainika kuwa uharibifu wa baadhi ya transfoma zinazofungwa maeneo mbalimbali nchini unasababishwa na wizi wa nyaya za shaba (earth wire) na mafuta.

Ameomba kutumia nafasi hiyo kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za kisheria kwa wahujumu hao ili kulinda miundombinu ya umeme.

Kuhusu ujenzi holela wa vituo vya mafuta, Dk Biteko amesema Kanuni za Viwango vya Upangaji wa Miji za mwaka 2018 zilizotengenezwa chini ya Sheria ya Mipango Miji, Sura ya 355 zinaelekeza kuwe na umbali wa mita 200 kati ya kituo kimoja na kingine.

Amesema kama vituo vipo upande mmoja wa barabara, basi lazima viwe na umbali huo wa mita 200, lakini kama vituo vipo pande tofauti za barabara, umbali wa kutenganisha vituo hivyo ni barabara yenyewe.

Amesema kutokana na wasiwasi ambao umekuwa ukioneshwa na wabunge pamoja na wananchi kuhusu ongezeko la vituo vya mafuta na ukaribu uliopo kati ya kituo na kituo, Wizara ya Nishati imeanza mazungumzo na Wizara ya Ardhi ili kubadilisha kanuni hiyo.

Amesema mazungumzo hayo yanalenga kuwezesha kuongeza umbali unaotakiwa kati ya kituo kimoja na kingine kwa kuzingatia masuala ya afya, usalama, mazingira pamoja na shughuli za kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema ni kweli kulikuwa na kukatika kwa umeme katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam kutokana na kituo cha kupoozea umeme cha Mbagala kuzidiwa.

Amesema kulikuwa na transfoma yenye uwezo wa MVA 50, lakini wataalamu wao wanafanya kazi usiku na mchana kuweka transfoma yenye uwezo wa MVA 120 kwa ajili ya kuongeza ukubwa wa kituo hicho.

“Wanafanya hivyo ili wananchi wa Mbagala, Temeke, Yombo, Mkuranga pamoja na maeneo mengine ya Kigamboni waendelee kupata umeme wa uhakika.

“Kwa hiyo, niwahakikishie wabunge wanaotoka Mbagala na Temeke pamoja na Yombo, Mkuranga na Kigamboni, kazi hii imefikia mwishoni. Muda wowote kuanzia sasa transfoma hiyo itaanza kufanya kazi na tutakuwa tumepunguza changamoto ya kukatika katika kwa umeme,” amesema. Bajeti hiyo imepitishwa na Bunge.